Ulega: Hakuna sababu ya kuagiza samaki nje

Muktasari:

  • Akizungumza na gazeti hili jijini hapa jana, naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kiwango cha samaki kinachozalishwa nchini ni tani 350,000 wakati mahitaji ni tani 750,000 kwa mwaka.

Dodoma. Wakati kila mwaka tani 22,000 za samaki zinaagizwa kutoka nje ya nchi, Serikali imesema hakuna sababu kwani uwezo wa kuzalisha kitoweo hicho cha kutosha upo.

Akizungumza na gazeti hili jijini hapa jana, naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kiwango cha samaki kinachozalishwa nchini ni tani 350,000 wakati mahitaji ni tani 750,000 kwa mwaka.

“Tunaagiza tani 22,000 kila mwaka lakini hakuna sababu ya kuagiza kiwango hicho tunao uwezo wa kuzalisha,” alisema.

Alisema tayari kuna mkakati wa Serikali na Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) katika kuikuza sekta hiyo.

Naye kaimu mkurugenzi wa TADB, Japhet Justin alisema tayari wametoa mikopo katika mikoa mbalimbali ikiwamo Morogoro na Arusha ikiwa ni hatua za awali.