Vijana 200 wapewa elimu ya ufugaji kuku, umeme jua

Muktasari:

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri kwa kufanya ujasiriamali.

Singida. Zaidi ya vijana 200 kutoka wilaya ya Mkalama, Singida, wamepewa mafunzo ya ufugaji kuku kibiashara  na ufundi umeme wa jua.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri kwa kufanya ujasiriamali.

Vijana hao 450, wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 27   kutoka kata za Mwangeza, Iguguno na Kinampundu katika Wilaya Mkalama  walipata mafunzo hayo ili kuwapa mbinu za ujasiriamali na ubunifu katika   biashara.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulikia uimarishaji huduma za afya (HAPA), Patrick Mdachi, alisema lengo ni kuwasaidia vijana ili waweze kutatua changamoto mbalimbali za ajira.
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka chuo cha VETA Mjini Singida, Charles Malongo, aliitaka jamii hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa, kufanya kazi kwa weledi ili waweze kufikia malengo yao.
Shirika la HAPA linaloendesha shughuli zake Mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Tabora na Singida, linakusudia kuwafikia vijana 2,000 nchi nzima, kupitia mradi wa fursa za ajira kwa vijana, kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la nchini Uholanzi (SNV).