Wanahisa Vodacom waridhia hisa za Rostam Aziz ziuzwe

Muktasari:

  • Zaidi ya asilimia 88 ya wanahisa wa Vodacom Tanzania wamekubali kuuzwa kwa hisa za kampuni ya Mirambo Holdings inayomilikiwa na Rostam Aziz.

Dar es Salaam. Wanahisa wa Vodacom wameikubalia kampuni ya Vodacom Group kununua asilimia 25.25 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni ya Mirambo Holdings inayomilikiwa na Rostam Aziz.

Ridhaa hiyo imetolewa kwenye mkutano mkuu wa dharura uliofanyika leo, Novemba 14 jijini Dar es Salaam na kutangazwa na mkaguzi wa ndani wa hesabu za fedha, Alvin Kajula.

Kajula amesema asilimia 88.18 ya wanahisa wa kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano nchini wamekubali kufanyika kwa mauzo hayo yatakayoipa umiliki mkubwa zaidi kampuni ya Vodacom Group.

Kuanzia leo, Vodacom Group itakuwa inamiliki asilimia 74 ya hisa za Vodacom Tanzania na zinazobaki zikienda kwa wanahisa wengine.

Hii ni mara ya pili kwa Rostam kuuza hisa zake alizokuwa anamiliki kwenye kampuni ya Vodacom. Mara ya kwanza alifanya hivyo mwaka 2014 alipouza asilimia 17.2 kwa Dola 240 milioni.

Ingawa haijafahamika thamani ya mauziano hayo lakini kumbukumbu zinaonyesha Rostam alikuwa anamiliki kiasi cha zaidi ya Dola 200 milioni (takriban Sh460 bilioni).

Ikiwa na zaidi ya wateja milioni 13 waliosajiliwa Vodacom Tanzania, ni ya pili kwa kuchangia mapato na faida ya Vodacom Group ikiwa nyuma ya Afrika Kusini ambako kuna zaidi ya watumiaji milioni 23.

Agosti mwaka jana, Vodacom iliorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na kuifanya kuwa pekee iliyotekeleza Sheria ya Epoca inayozitaka kampuni zote za mawasiliano nchini kuorodhesha walau asilimia 25 ya hisa zake sokoni hapo.

Mpango wa Vodacom Group kununua hisa za Vodacom Tanzania ilibainishwa tangu Februari mwaka jana na sasa utaratibu umekamilishwa.

Mei 4, Tume ya Ushindani wa Biashara Tanzania (FCC) ilitoa tangazo la mpango wa Vodacom Group kununua hisa za Vodacom Tanzania na kuruhusu yeyote anayepinga mpango huo kuwasilisha hoja zake.

Rostam Aziz, mfanyabiashara mkubwa na bilionea, ni mwanasiasa ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Igunga kabla hajastaafu nafasi za uongozi za kisiasa.