Wazalishaji vifaa wawalia wabunge kuwasaidia soko

Muktasari:

  • Hayo yalibainishwa kwenye ziara ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipotembelea viwanda vya chuma, nondo, bomba na vifaa vya plastiki vya kampuni ya Lodhia Group Ltd iliyopo.

Kisarawe. Wazalishaji wa vifaa vya ujenzi nchini wamelalamikia matumizi ya vifaa kutoka nje katika utekelezaji miradi inayoendelea maeneo tofauti.

Hayo yalibainishwa kwenye ziara ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipotembelea viwanda vya chuma, nondo, bomba na vifaa vya plastiki vya kampuni ya Lodhia Group Ltd iliyopo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sailesh Pandit aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa changamoto hiyo inavikabili viwanda vingi vya ndani jambo linalochangia kupungua kwa ajira kutokana na uzalishaji kuwa mdogo.

“Uwezo wetu ni kuzalisha mita 50,000 za nondo kwa mwezi lakini tunazalisha asilimia 15 pekee kwa kuwa hakuna soko. Nimeajiri watu 1,300 kwa uzalishaji huu suala la kupunguza wafanyakazi haliepukiki,” alisema Pandit.

Akijibu changamoto hizo, naibu waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alisema kuanzia sasa Serikali itawaelekeza washauri wa ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa miradi kuangalia bidhaa za ndani zinazoweza kutumika.