Dk Kigoda avunja Bodi TBS

Dk Abdallah Kigoda.

Muktasari:

“Tumekwenda Hong Kong na akatupeleka katika ofisi feki na tulipombana akasema kuwa aliomba kwa muda kuitumia ofisi hiyo,” alisema Filikunjombe.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda  ameivunja Bodi ya  Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili  kutekeleza nia ya wizara hiyo ya kuboresha utendaji kazi wenye tija na ufanisi katika shirika hilo.

Uamuzi wa kuvunjwa kwa bodi hiyo umekuja miezi sita baada ya Dk Kigoda kuitaka bodi hiyo kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege ili kupisha taratibu za kisheria ikiwamo suala la uchunguzi kufanyika dhidi yake.

Akizungumzia uamuzi huo, Dk Kigoda amesema umetokana na bodi hiyo kutokuwa na tija na ufanisi kama ilivyotarajiwa.

“Shirika hili ni nyeti sana kwa taifa, hivyo ni lazima tuimarishe bodi ili kuhakikisha inafanya kazi kama inavyotarajiwa na wananchi,” alisema Dk Kigoda.

Alisema kuwa pamoja na wizara kutoa maagizo ya awali yaliyoitaka bodi kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi, bado bodi ilishindwa kufanya kazi kwa tija na ndiyo maana wizara imechukua uaumuzi wa kuvunja bodi hiyo.
“Tutahakikisha bodi mpya inapatikana haraka ili kutokwamisha shughuli za shirika hili nyeti,” alisema Dk Kigoda.

Bodi hiyo imevunjwa miezi michache baada ya kuapishwa mwezi wa tatu mwaka huu na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyrill Chami,

Waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo iliyovunjwa ni mwenyekiti wa bodi Oliver Mhaiki, Donald Chidomu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Rashidi Salimu kutoka Wizara ya Viwanda Zanzibar, Dk Bertha Maegga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Odilo Majengo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.

Wengine ni Profesa Ntengwa Mdoe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Peter Mahunde kutoka Shirika la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Mariki kutoka Tume ya Ushindani, Suzi Leizer kutoka shirikisho la mashirika madogo na ya kati (SMEs) na Elpina Mlaki kutoka Wizara ya Fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu atepoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa wizara hiyo takribani miezi sita iliyopita, Dk Kigoda aliiagiza TBS kumsimamisha kazi Ekelege kutokana na kuibuka kwa mjadala mkali bungeni juu ya utendaji kazi wa shirika hilo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe ilimtuhumu Ekelege baada ya  kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye mpango wa TBS kukagua bidhaa nje ya nchi.

Filikunjombe alieleza kuwa waligundua madudu baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China. “Tulikwenda Hong Kong na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini anachokifanya Mkurugenzi (Ekelege) huko nje.”  

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kamati, Ekelege aliwapeleka katika ofisi hewa ambayo baadaye waligundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari.

“Tumekwenda Hong Kong na akatupeleka katika ofisi feki na tulipombana akasema kuwa aliomba kwa muda kuitumia ofisi hiyo,” alisema Filikunjombe.

Ziara ya kumsafisha Ekelege
Mara baada ya Ekelege kusimamishwa kazi Mei mwaka huu kuna ujumbe mwingine ulitembelea  nchi zilizokuwa zikidaiwa kuwa hazikuwa na ofisi za TBS na kueleza kuwa madai hayo sio ya kweli.

Ujumbe huo wa watu wanne ambao ulijumuisha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Masharika ya Umma, Muhammed Mgimwa ilifanya ziara hiyo katika nchi za Japan na China kuazia Mei 6 hadi Mei 14 mwaka huu.
Ujumbe huo ulieleza kuridhishwa na kazi nzuri ambayo inafanywa na mawakala wa TBS waliopo katika nchi mbalimbali ikiwamo Japan na China.

Wajumbe wengine waliokuwa katika msafara huo, ni Mwenyekiti wa Bodi ya TBS, Oliver Mhaiki, Ekelege na Mdhibiti wa Ubora wa TBS, Kezia Mbwambo.

Mbali ya kutembelea Japan pia timu hiyo ilitembelea Uswisi na Ufaransa ambako walikagua kampuni zinazofanya kazi ya uwakala kwa niaba ya TBS katika maeneo hayo.

Ujumbe huo katika ripoti yake ambayo ilitolewa na gazeti hili ulieleza  wazi kuwa kila maeneo waliyotembelea walikutana na viongozi wa makampuni hayo na kutembelea karakana na maabara na kwamba walishuhudia kazi ya ukaguzi wa magari yaliyotumika ikifanyika kwa ufanisi.

Baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari yaliyotumika nchini Japan timu hiyo ilitoa maoni yake ikieleza kuridhishwa  utaratibu huo na kwamba unafaa kuendelea kwa manufaa ya nchi.