Mradi wa gesi Kilwa ‘kuzaa’ hospitali ya kisasa ya kimataifa

Ramani ya hospitali hiyo

Muktasari:

Mradi huo una gharama kubwa pia utafanywa na wageni ambao wana utalaamu wa miaka mingi katika biashara ya gesi duniani.

WASWAHILI husema, ‘mgeni njooo , mwenyeji apone’.
Usemi huu una maana nyingi, lakini mojawapo ni ile ya kuona kwamba mara nyingi mgeni afikapo, ujio wake huwa zawadi hata kwa wenyeji.
Kwa Watanzania ,wengi wao wanaposafiri kwenda kutembelea jamaa zao ni kawaida yao kubeba zawadi.


Utaratibu huu unaweza kushabihiana na utakaotokea katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ambako imegundulika gesi.
Kampuni ya Statoil kutoka Norway ikishirikiana na Exxon Mobil iligundua gesi katika Visiwa vya Zafaran na Lavan vilivyopo Kitalu 2, Ukanda wa Pwani ya Tanzania, hususan Pwani ya Kilwa.


Mradi huo una gharama kubwa pia utafanywa na wageni ambao wana utalaamu wa miaka mingi katika biashara ya gesi duniani.


Kutokana na ujio wa wageni hao, Watanzania hususan wakiwamo wakazi wa Kilwa, Lindi na Mtwara kwa jumla hawana budi kupata faida za moja kwa moja na zingine zisizo za moja kwa moja. Miongoni mwa faida zisizo za moja kwa moja ni gesi hiyo kutumika kutengeneza umeme utakaopatikana kwa uhakika na kuuzwa kwa wananchi wote.


Hata hivyo, ujio wa mradi huo kwa upande mwingine una faida kwao kutokana na kutoa ajira ambayo itazingatia uwezo.
Je wakazi wa Halmashauri ya Kilwa watapata faida gani ya kudumu kutokana na gesi hiyo?
Hili ndilo swali ambalo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Adoh Mapunda anasema walijiuliza baada ya kufika kwa wageni hao.


Mapunda anasema madiwani, watendaji na mkuu wa wilaya walikaa na kutafakari kwa kina juu ya faida ya kudumu itakayoonekana wilayani mwao kutokana na ujio wa mradi wa gesi.
“Sisi tulikataa kauli za kusaidiwa madawati kwenye shule zetu, ama kupewa dawa kwenye hospitali na zahanati zetu


Hii ni kwa sababu tuna uwezo nazo, badala yake tukabuni mradi mkubwa wa kimataifa ambao utakuwa na faida ya kudumu kwa Kilwa na taifa kwa ujumla”, anasema.
Anafafanua kwamba mradi huo ni ujenzi wa hospitali ya kimataifa itakayolingana na ile ya Apollo nchini India ambayo viongozi mbalimbali duniani hukimbilia kwenda kutibiwa.
Hospitali ya aina hiyo itajengwa na mwekezaji na itaendeshwa na taasisi nyingine ya kimataifa huku halmashauri ikiwa na hisa za kupata gawio la kila mwaka kutokana na faida.


‘’Tulizungumza na wawekezaji, Statoil , kwamba watujengee hospitali ya aina hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa tiba kwa viongozi wakiwamo marais wa Afrika na wakuu wa kampuni mbalimbali Afrika zikiwamo kampuni za uwekezaji katika gesi , madini na hata usafirishaji na wafanyabiashara wa nchi mbalimbali,’’ anafafanua.


Mapunda anasema mpango huo unatekelezwa kupitia utaratibu uliopo kwenye mikataba kwa wawekezaji kuhusu uwajibikaji na ushiriki katika masuala ya kijamii, Social Co-operation Responsibility (SCR).


Anasema tayari Statoil imetenga Sh18 bilioni kuanza ujenzi wa hospitali hiyo mjini Kilwa wakati wowote kuanzia mwaka huu. Anafafanua kuwa michoro ya hospitali hiyo ipo tayari na imechorwa kama lilivyokuwa jengo la kifalme yaani Kasri lililojengwa eneo la Kilwa Kisiwani enzi za Sultan wa Kiarabu aliyekuwa akimiliki kisiwa hicho.


‘’Tunatarajia kwamba taasisi ya kimataifa ya Aga Khan Foundation ndiyo itakayoendesha hospitali hii kwa kiwango cha kimataifa . Tulikaa na kuzungumza pande zote tatu, yaani Kilwa, Statoil na Aga Khan Foundation na kukubaliana kuanzisha hospitali hiyo, hivyo tuna imani itaendeshwa kama ile ya Apollo,’’ anasisitiza Mapunda.


Anasema hospitali hiyo itaajiri madaktari mabingwa kutoka ndani na nje ya nchi, itakuwa na wafanyakazi wataalamu , pamoja na wahudumu ambao wengi watatoka Halmashauri ya Kilwa.


Kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Kilwa inatoa wito kwa wakazi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili malengo hayo yatimie.


“Hospitali hiyo itaongeza majengo mengi ya kisasa yakiwamo makazi ya wafanyakazi, hivyo ni jukumu la wakazi wa Kilwa kujiandaa kwa kulima mazao mengi na kujenga nyumba za kisasa,’’ anahamasisha


Hadi sasa, Kilwa ina hospitali mbili, vituo vya afya vitano na zahanati 43, anaeleza mkurugenzi huyo.