Kumbi za starehe, michezo zafungwa kunusuru uchumi Zambia

Rais wa Zambia, Edgar Lungu

Muktasari:

Rais wa Zambia, Edgar Lungu amemwomba Mungu kuinusuru nchi yake dhidi ya kuendelea kuporomoka kwa thamani ya fedha nchini humo, huku mamlaka husika zikichukua hatua zaidi kukabiliana na halihiyo.

Lusaka , Zambia. Rais wa Zambia, Edgar Lungu amemwomba Mungu kuinusuru nchi yake dhidi ya kuendelea kuporomoka kwa thamani ya fedha nchini humo, huku mamlaka husika zikichukua hatua zaidi kukabiliana na halihiyo.

Serikali ya nchi hiyo imetangaza kufungwa kwa kumbi zote za burudani huku mechi zote za mpira zikiahirishwa kupisha siku maalumu ya kuliombea taifa.

Kiongozi huyo alitangaza hatua hiyo wiki iliyopita baada ya thamani ya fedha kuanguka kwa asilimia 45 dhidi ya Dola ya Marekani. Hali hiyo ilisemekana kuchangiwa na kuanguka kwa bei ya madini ya shaba ambayo ni tegemeo lake kuu la kiuchumi.

Bei za vyakula pia zimepanda pia uzalishaji wa umeme umepungua kutokana na kiwango kidogo cha maji katika Ziwa Kariba. Ziwa hilo linategemewa kwa uzalishaji wa umeme.

Kwa mujibu wa Shirika la Utafiti la Bloomberg Service, thamani ya Kwacha imeshuka zaidi dhidi ya Dola ya Marekani katika nchi zote 155 ilizozifanyia utafiti.

“Mungu wetu amesikia vilio vyetu. Ametusamehe dhambi zetu na tuna imani kuwa ataiponya nchi yetu kutokana na changamoto hii kubwa ya kiuchumi,” alisema Rais Lungu wakati alipokuwa akilihutubia watu zaidi ya 5,000. Marais wa zamani, Kenneth Kaunda na Rupiah Banda pia walihudhuria hafla hiyo.

“Hatupaswi kutafuta upenyo wa kisiasa kutokana na changamoto zetu .zinazotukabili kwani wanaoumia ni watu wetu” alisema Rais Lungu.