Wednesday, May 1, 2013

Watendaji wabebeshwa ‘zigo’ la migogoro ya ardhi D’Salaam

Dodoma. Watendaji wa mitaa, kata na wenyeviti wa mitaa wametajwa kuwa ni chanzo cha migogoro ya ardhi katika maeneo mengi ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.

Tuhuma hizo ziliibuliwa na Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa (CCM) ambaye alisema, watendaji hao wamekuwa wakiuza maeneo ya wazi na wakati mwingine kuhalalisha maeneo yaliyo mipakani pindi wananchi wanapouza huku wakijua si maeneo yao halali.

Katika swali la msingi Mwaiposa alitaka kujua ni lini Serikali itaona umuhimu wa kwenda kuonyesha mipaka katika  maeneo ya Nzasa, Msitu wa Kazimzumbwi, Kitunda na ardhi ya Jimbo la Ukonga ambayo yamekuwa na mgogoro wa muda mrefu.

Mbunge huyo pia alihoji Serikali ina mpango gani wa kutatua migogoro ya ardhi katika Kata za Msongola, Pugu, Kivule na Majohe.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri alikiri kuwapo na migogoro katika maeneo hayo ambayo inatokana na mwingiliano wa mipaka.

Mwanri alisema tayari Ofisi ya Waziri Mkuu ilishaliona jambo hilo na iko mbioni kulipatia ufumbuzi kwa kuagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  na Wizara ya Maliasili na Utalii kukutana kwa pamoja na Manispaa ya Ilala na Kisarawe ili waunde tume ya kuchunguza mgogoro huo.

“Hata hivyo, ili kuondoa utata huo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala katika bajeti yake ya 2013/14 imeweka kipaumbele na kutenga Sh280 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa, kati ya fedha hizo Sh70 milioni zitajenga Shule ya Msingi Pugu Kajiungeni ili kuondoa utata huo,” alisema Mwanri.

Kuhusu Watendaji wanaouza maeneo ya watu alizitaka mamlaka husika kuwaondoa mara moja kwani hawana sifa tena za kuwa viongozi.

Dar es Salaam ni miongoni mwa mji mwenye migogoro mingi ya ardhi kutokana na wingi wa watu wanaohamia pamoja na amendeleo yaliyopo.
Hata hivyo hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profess Anna Tibaijuka alitoa agizo la kuhakikisha maeneo yote ambayo viwanja bado viko wazi yanapimwa na kugawiwa huku wataalamu wa mipango miji wakihusishwa moja kwa moja kwa lengo la kuepusha migogoro ya mara kwa mara  na ujenzi holela.

-->