Huu ndiyo ulazima wa kuwa na kikosi maalumu cha uokoaji Ziwa Victoria

Muktasari:

  • Kutokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere na kusababisha vifo vya watu 230, katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, wadau mbalimbali wametoa maoni na kutaka kiundwe kikosi maalumu cha uokoaji hususani kwenye ziwa hilo ili kukabiliana na matukio ya ajali za majini kwenye Ziwa Victoria. Wanasema kuundwa kwa kikosi hicho kunaweza kupunguza ukubwa wa maafa hasa vifo kwa kuwa waokoaji wanaweza kufika eneo la ajali kwa haraka zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mwanza. Bila shaka taifa bado linakumbuka na kusononeshwa na vifo vya watu 230 vilivyotokana na ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20, mwaka huu.
Kivuko hicho kinachodaiwa kujaza abiria na mizigo kuliko uwezo wake kilipinduka hatua chache kabla ya kutia nanga katika gati ya Kijiji cha Bwisya, Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe.
Wakati uwezo wake ni kubeba abiria 101 na tani 25 za mizigo, kivuko cha Mv Nyerere kimebainika kubeba zaidi ya watu 270 baada ya maiti 230 kuopolewa, watu 41 kuokolewa wakiwa hai huku baadhi ya wakazi wa Ukara wakijitokeza na kudai hawajaona miili ya ndugu zao wanaoaminika walikuwamo ndani ya chombo katika safari iliyosababisha ajali.
Kama ilivyokuwa kwenye ajali nyingine zilizotangulia, ajali ya Mv Nyerere imeonyesha udhaifu katika eneo la uokoaji kuanzia kwenye rasilimali watu, ujuzi, zana na vifaa.
Ukweli huu unadhihirishwa na muda uliotumika kwa wataalamu wa uokoaji, hasa wazamiaji kuwasili eneo la Bwisya kivuko kilipopinduka.
Hata kitendo cha wavuvi na wazamiaji wenyeji wanaotumia uzoefu wa shughuli za majini bila kupitia kozi maalumu kumudu kuwaokoa hai watu 40 muda mfupi baada ya ajali, kinadhihirisha kuwa pengine watu wengi zaidi wangeokolewa hai iwapo kungekuwepo vikosi maalumu na zana za uokozi jirani na eneo ilipotokea ajali.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa shughuli ya uokoaji, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Isack Kamwelwe ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano aliwamwagia sifa na pongezi wakazi wa Ukara kwa kuwaokoa hai watu 40 kabla vikosi vya uokozi kuwasili.

“Serikali inathamini na hakika inawapongeza wakazi hasa wavuvi wa Kisiwa cha Ukara waliojitolea wakitumia ujuzi na zana zao ikiwemo mitumbwi na kufanikiwa kuwaokoa hai watu 40,” alisema Kamwelwe.

Vikosi vya uokoaji

Igawa wapo wanaoweza kubisha, lakini ajali ya Mv Nyerere imedhihirisha kuwa licha ya kuwa na vikosi kadhaa vya ulizni na usalama katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini ama havina wataalamu wajuzi wa uokozi au hawana zana na vifaa.

Hii inadhihirishwa na ukweli kwamba wengi wa waliokuwa kwenye vikosi vya uokoaji walitokea Makao Makuu ya Jeshi Kikosi cha Wanamaji jijini Dar es Salaam na Zanzibar. Wataalamu hawa wa uokoaji kutoka Dar es Salaam na wenzao wa Chama cha Waogeleaji Zanzibar waliwasili kuanzia siku ya pili hadi ya tatu tangu ajali ilipotokea.

Kuwasili kwao si tu kuliongeza kasi ya uokoaji na uopoaji wa miili ya waliokufa kwenye ajali hiyo, bali pia walifanikisha kukigeuza na kukivutia ufukweni kivuko hicho kilichokuwa kimepinduka juu chini.

Chama cha waogeleaji Mwanza

Mwenyekiti wa Chama cha Waogeleaji Zanzibar, Fakhi Mmbarouk anasema chama chake kinakusudia kushirikiana na wadau wengine kutoa elimu kwa umma kuhusu kuanzishwa kwa chama cha waogeleaji mkoani Mwanza.

Akizungumza na Mwananchi, Mmbarouk aliyekuwa mmoja wa viongozi wa vikosi vya uokoaji katika ajali ya Mv Nyerere, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona pengo linalotokana na kukosekana kwa waogeleaji wenye utaalamu, elimu na ujuzi mkoani Mwanza.

“Baada ya operesheni hii nimepanga kurejea Mwanza kushirikiana na viongozi na wadau wengine kuhamasisha na kuanzisha mafunzo na kozi maalumu ya wazamiaji pamoja na kuunda chama cha wazamiaji Mwanza,” anasema Mmbarouk.

Mwogeleaji huyo aliyejizolea sifa wakati wa operesheni ya uokoaji katika ajali ya Mv Nyerere kwa jinsi alivyojituma na kuhamasisha wenzake, alisema kuundwa kwa kikosi na chama cha wazamiaji Mwanza kutasaidia uokoaji katika matukio ya dharura na hata kuundwa kwa vikosi na vyama hivyo hadi ngazi ya wilaya.

“Zanzibar tayari tumefanikiwa sana katika kuhamasisha na kuunda vyama vya waogeleaji, lakini kwa Mwanza nimegundua jambo hili bado ni geni licha ya ukweli kwamba ni mkoa unaopakana na Ziwa Victoria,” anasema.

Meli mpya, kikosi cha uokoaji, utii wa sheria

Akizungumza wakati akihojiwa nyumbani kwake Kijiji cha Bwisya-Ukara, Mtoroki Masena (75) aliyepoteza mke na mtoto katika ajali ya Mv Nyerere alitoa maombi matatu kwa Serikali ili kudhibiti matukio ya ajali za majini.

Kwanza, anaiomba kusimamia kwa karibu usalama wa safari za majini kwa kuimarisha vitengo vya uokoaji ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi zake zinazohusiana na uokoaji, kwa kuwajengea watendaji uwezo wa kitaalamu na kuwapa zana na vifaa vya kisasa.

Kutokana na upekee wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Masena anaiomba Serikali kuhakikisha mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Geita inayopakana na Ziwa Victoria kuwa na vikosi maalumu vya uokoaji majini.

“Sina nia ya kulaumu, lakini nadhani watu wengi zaidi wangeokolewa iwapo mkoa wa Mwanza ungekuwa na kikosi maalumu cha uokoaji ambacho kingewahi kufika eneo la tukio badala ya kuwasubiri waogeleaji kutoka Dar es Salaam na Zanzibar,” anasema Masena.

Ombi lingine la Masena ambalo ni maalumu kwa ajili ya wakazi wa Kisiwa cha Ukara ni Serikali kuongeza idadi ya safari kati ya gati ya Bwisya na Bugatola kutoka nne za sasa (mbili kwenda na mbili kurudi) hadi angalau nane (nne kwenda na nne kurudi) kwa siku.

“Hii itaondoa tatizo la watu kujazana kwenye kivuko kama ilivyotokea kwenye Mv Nyerere iliyopakia watu zaidi ya uwezo wake kwa sababu kila mmoja alikuwa akilazimisha kuingia kwa hofu ya kukosa usafiri endepo asingeingia humo,” anasema.

Kwa upande wa wananchi, Masena anashauri kila mmoja awe mlinzi wa usalama wa maisha yake kwa kutii sheria bila shurti ikiwemo kuacha kupanda chombo cha usafiri kilichojaza abiria kupita uwezo wake.

“Wananchi tutii na kulinda sheria kwa kuacha kujazana kwenye vivuko na boti zinazotumika kusafirisha abiria na mizigo ndani ya Ziwa Victoria, kila mmoja awe mlinzi wa usalama wa maisha yake. Tunapoona uvunjifu wa sheria tuzuie au kutoa taarifa kwa vyombo vya dola,” anashauri Mzee Masena.

Katika ajali hiyo, Masena alimpoteza mke wake, Buhinda Mtoroki (64) aliyefunga naye ndoa miaka 45 iliyopita. Wawili hao walioana mwaka 1973.

Pamoja na mke, Masena pia alimpoteza mtoto wake, Nyanjira Mtoroki (43) aliyekuwa mmoja wa wafanyabiashara wa mbogamboga ambaye alikwenda kufuata bidhaa katika gulio la Bugorola linalofanyika kila Alhamisi.

Kivuko kipya Ukara

Wakati wakiendelea kuomboleza vifo vya wapendwa wao waliokufa katika ajali, wakazi wa Kisiwa cha Ukara wamepata matumaini mapya ya kuondokana na adha ya usafiri baada ya Serikali kutangaza uamuzi wa kujenga kivuko kipya, kikubwa na chenye uwezo zaidi ya Mv Nyerere.

Akizungumza na wakazi wa Kisiwa cha Ukara alipofika kushiriki ibada ya mazishi ya Kitaifa ya baadhi ya waliokufa katika ajali ya Mv Nyerere, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kwamba kivuko kipya kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 50 za mizigo na abiria zaidi ya 300.

Kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka kina uwezo wa kubeba tani 25 na abiria 101.

“Rais John Magufuli ameagiza tenda ya ujenzi wa kivuko kipya itangazwe mara moja, wakati kivuko kipya kikijengwa, Serikali itahakikisha wakazi wa Ukara wanaendelea kupata huduma ya usafiri kupitia vyombo vingine vya umma,” alisema Waziri Mkuu.

Pamoja na Mv Nyerere, wakazi wa Ukara, kisiwa cha pili kwa ukubwa baada ya kile cha Ukerewe wilayani humo, wanategemea usafiri wa boti ndogo ndogo za injini na makasia kama njia kuu ya usafiri kwenda na kurudi kwenye visiwa vingine.

Wilaya ya Ukerewe ambayo pia ni kisiwa ina jumla ya visiwa 38, kati hivyo, 34 ni vya makazi.