Kliniki inayohama ilivyosaidia kupunguza vifo vya wajawazito Mtwara

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Dk Kumalija Gasper mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mpango wa elimu kwa umma, hasa kwa akina mama kuhusu umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki.

Licha ya kukabiliwa na upungufu wa watumishi 211 wa kada mbalimbali katika sekta ya afya, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara imefanikiwa kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Dk Kumalija Gasper mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mpango wa elimu kwa umma, hasa kwa akina mama kuhusu umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki.

Dk Gasper anataja mbinu nyingine iliyofanikisha kupunguza vifo vya wajawazito vinavyotokana na matatizo ya uzazi kutoka 146 kwa wajawazito 100, 000 waliojifungua wilayani humo mwaka 2015 hadi kufikia vifo viwili mwaka jana (2017), kuwa ni huduma ya afya, hasa kliniki na chanjo kwa wajawazito na watoto inayohama kutoka kijiji kimoja hadi kingine.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

“Tunatumia huduma ya kuhamahama kama moja ya njia ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi wa sekta ya afya; hii inatuwezesha kuwafikia wananchi huko vijijini na kuwahudumia,” anaeleza Dk Gasper.

Anasema kwa kwenda vijiji, wataalamu wa afya wanapata fursa ya kuwahudumia, kuwapima wajawazito na kubaini viashiria vya hatari ili kuchukua hatua mapema.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa sekta ya afya, mwaka 2016, halmashauri hiyo iliandikisha vifo vya wajawazito 73 kati ya wajawazito 100, 000.

Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) 2007-2017 ulilenga kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 578 hadi kufikia 175 kwa kila vizazi hai 100, 000.

Pia, ulilenga kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 112 hadi 45 kwa watoto 1, 000 waliozaliwa hai.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni, Dk Gasper anasema idara yake pia inayo magari manne ya wagonjwa kwa ajili ya huduma za dharura katika zahanati zake 26 na vituo vya afya vitatu.

Pamoja na mafanikio hayo, upungufu wa watumishi na umbali wanaotembea wananchi kwenda na kurudi kwenye maeneo yenye huduma ni kati ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya katika halmashauri hiyo inayopatikana kusini mwa Tanzania.

Upungufu wa watumishi

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Dk Kumalija Gasper halmashauri hiyo ina watumishi 163 pekee kati ya 374 wanaohitajika, na hivyo kufanya upungufu kuwa watumishi 211.

“Baadhi ya watumishi hulazimika hufanya kazi mfululizo bila kupumzika; hii inaweza kushusha kiwango cha ubora wa huduma kutokana na uchovu,” anasema Dk Gasper.

Zahanati ya Madimba ni mfano hai katika suala la upungufu wa watumishi kutokana na kuwa na watumishi wanne pekee ambao ni mganga, muuguzi mkunga, mama afya na muuguzi mmoja.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Madimda, Mohamed Mussa anasema hata huyo mganga mmoja aliyepo kwenye zahanati upatikanaji wake ni wa nadra kutokana na kuongezewa kitengo kingine cha ukoma na kifua kikuu.

“Tumetoa taarifa kwa mamlaka za juu kuhusu suala hili lakini hakuna ufumbuzi hadi sasa,” anasema Mussa.

Sharifa Khamisi, mkazi wa Kijiji cha Mtendachi anasema kuna wakati wanalazimika kushinda kutwa nzima kusubiri huduma kutokana na wahudumu kuelemewa, hasa muuguzi anapokuwa mmoja baada ya mwenzake kupata dharura ya ugonjwa, kwenda likizo au safari.

Muuguzi azidiwa kazi

“Mwezi wa Desemba mwaka jana (2017), nilibaki mwenyewe nikiwahudumia wagonjwa baada ya mwenzangu kwenda likizo na mwingine kuwa na majukumu mengine ukiachana na daktari ambaye anapatikana mara moja moja,” anasema Veronica Haule, muuguzi msaidizi katika zahanati ya Madimba

Anasema kwa kipindi hicho chote, alifanya kazi za daktari, mkunga, kupokea na kuandikisha wagonjwa, kugawa dawa, kuchoma sindano, kufunga vidonda, kutoa chanjo na kuwapima wajawazito wa watoto wanaofika kliniki.

“Wakati mwingine tunajikuta tumechoka hadi kujikuta tunapishana kauli na wagonjwa ambao kwao jambo muhimu ni huduma,” anasema Haule.

Kuhusu kukosekana kwa nyumba ya muuguzi kwenye zahanati hiyo, muuguzi anashauri kujengwe hata nyumba moja ili muuguzi aishi eneo la kazi kwa ajili huduma za dharura kwa wagonjwa, hasa wajawazito nyakati za usiku.

“Kuna wakati naitwa kuja kuhudumia wagonjwa wa dharura, hasa wajawazito na kukuta wengine wamejifungulia nje kutokana na umbali wa ninakoishi,” anasema muuguzi huyo.

Umbali wa huduma

Wakazi wa vijiji saba vinavyounda kata ya Madimba ni mfano kutokana na baadhi yao hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 16 kwenda na kurudi kufuata huduma ya afya katika kituo zahanati pekee iliyopo Kijiji cha Madimba.

Umbali huo umeelezwa kuchangia vifo kama anavyoeleza Habiba Rashid, mkazi wa Kijiji cha Mayaya kilichopo umbali wa kilomita nane kutoka Zahanati ya Madimba, aliyepoteza mtoto kwa kukosa huduma mwaka 2012 baada ya kujifungulia njiani wakati akikimbizwa zahanati kwa kutumia usafiri wa baiskeli.

“Ilikuwa saa 12:00 jioni ya tarehe ambayo siikumbuki mwaka 2012 nilipoanza kusikia uchungu na mume wangu kunipakia kwenye baiskeli kunikimbiza zahanati ya Madimba lakini nikazidiwa na kujifungulia njia na mtoto wangu kufariki kwa kukosa huduma,” anasema kwa masikitiko Habiba.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Mayaya, Zainabu Issa, mama wa watoto wawili anasema ili kuepuka madhara ya kiafya na kujifungulia njiani, wajawazito kijijini hapo hulazimika kuhamia na kuishi kwa ndugu, jamaa na marafiki walioko Kijiji cha Madimba kusubiria siku za kujifungua.

“Wenye uwezo hujiwekea akiba ya nauli kwa ajili ya kukodisha gari au pikipiki kuwakimbiza zahanati au Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mtwara ya Ligula,” anasema Zaibabu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtendachi, Salum Muhidini anasema kutokana na changamoto hiyo kuna wakati hulazika kutoa msaada wa haraka pale unapohitajika.

“Akipatikana mama mjamzito anayehitaji huduma ya dharura napigiwa simu kama mwenyekiti hivyo nalazimika kumkimbiza Hospitali ya Rufaa Ligula kwa kutumia gari langu,” anasema Muhidini.

Vijiji vingine vinavyounda Kata ya Madimba yenye wakazi zaidi ya 13, 139, kwa mujibu wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2012 ni pamoja na Namindondi, Mngoji, Mitembe, Mitambo na Mtendachi kilichopo umbali wa kilomita tatu kutoka ilipo zahanati.

Mikakati ya halmashauri

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga anasema katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17 uliomalizika, halmashauri hiyo imefanikiwa kujenga zahanati mpya nne katika vijiji vya Makome A na B, Nanyani na Mbuo ambapo kazi ya kumalizia nyumba za waganga inakamilika ili zianze kutoa huduma.

“Tunawahimiza wananchi kutumia vikao vyao vya Serikali ya vijiji kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, ofisi na nyumba za walimu kwa kutumia nguvu zao halmashauri itawaunga mkono kulinana na vipaumbele na bajeti,” anasema Kipanga.