Mradi wa Bilioni 42 utakavyotatua kero ya maji jijini Mbeya

Maofisa wa Mbeyauwsa wakiwa kwenye moja ya chanzo cha maji yanayotumika kwa sasa jijini Mbeya. Maji hayo hayatoshelezi mahitaji ya wananchi katika jiji hilo. Picha na Lauden Mwambona

Muktasari:

Wengi wanaoga baada ya kuamka na hatimaye wanaoga baada ya kurudi kutoka kazini, nyakati za jioni.

Bila shaka haipo kanuni wala sheria inayoelekeza watu wanatakiwa kuoga mara ngapi kwa siku, lakini wengi hususan watumishi wamezoea kuoga walau mara mbili kwa siku.

Wengi wanaoga baada ya kuamka na hatimaye wanaoga baada ya kurudi kutoka kazini, nyakati za jioni.

Kwa maeneo ya joto kama mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara na huko Zanzibar wakazi wake wanaweza kuoga hata zaidi ya mara mbili huku wakisema ‘wanajimwagia maji mara moja kupoza joto mwilini.

Ni hivyo hivyo sehemu za mikoa ya Mbeya, Morogoro, Mwanza, Kigoma wapo wanaoweza kuoga mara tatu au zaidi kupoza joto kwenye miili yao kama upatikanaji wa maji ni mzuri.

Lakini wapo watu wengi ambao wanalazimishwa kuoga mara moja hata kama wana hamu ya kuoga mara mbili au nne kwa siku.

Miongoni mwa watu wanaolazimishwa kuoga mara moja ni wakazi wa Jiji la Mbeya ambalo nalo lina miezi ya baridi na mingine ya joto kali.

Kutokana na taarifa za kuwapo watu wengi wanaooga mara moja kwa siku, nalazimika kutembelea mitaa na kaya kadhaa ili kujua ukweli.

Ni saa 5:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri, napita katika mitaa ya Gombe, Uyole hadi Igawilo jijini Mbeya.

Siku ya pili kwa muda huohuo naendelea kukata mitaa ya Veta, Mlima James, Forest Mpya, Ilemi hadi Kata ya Isanga, lengo la safari yangu ni kutaka kujua ukweli wa taarifa kwamba wakazi wengi wa jijini hapa wanaoga mara moja kwa siku.

Nikiwa Mtaa wa Gombe nakutana na mwanaume aliyejitambulisha kwa jina la Paul James (51) ambaye namuuliza kuhusu hoja yangu ya kujua kama wengi wanaoga mara moja.

James anasema kwamba ni kweli na kusisitiza hata yeye mara nyingi akiamka asubuhi haogi hadi jioni wakati wa kwenda kulala.

“Asubuhi nanawa zangu mikono, uso na miguu huku nikipiga mswaki kabla ya kwenda kwenye shughuli zangu za biashara, lakini huwa naoga kuanzia saa 2:00 usiku na kuendelea nikiwa nimesharudi nyumbani,’’ anasema James huku akinifafanulia sababu ya hali hiyo.

Naye Cairo Kyomola wa Uyole anasema kwamba asilimia kubwa ya wakazi wa Mbeya wanaoga mara moja kwa siku na kufafanua kwamba hata yeye yupo katika mtindo huo kwa miaka mitano sasa.

Kyomola anajieleza kwamba analazimika kuoga mara moja kutokana na tatizo ambalo linawakumba watu wengi wa mitaa yake na kunidokeza chanzo cha tabia hiyo.

Nikiwa Mtaa wa Uyole muda wa mchana wa jua kali, nakutana na watu wengi wakiwamo watoto ambao kwa kweli mwonekano wao ni wale wanaooga mara moja kila baada ya siku mbili na wengine wa kuoga mara moja kwa wiki.

“Je utaoga saa ngapi?” Namuuliza mtoto wa miaka 12 (jina linahifadhiwa) ambaye anajibu kwamba ataoga usiku kabla ya kwenda kulala.

Majibu kama hayo pia yalipatikana maeneo ya Ilemi na Isanga huku wakazi wote hao wakitoa sababu ya kuoga mara moja kwa siku kwamba inasababishwa na tatizo la uhaba wa maji.

Uhaba wa maji katika Jiji la Mbeya ni mkubwa kiasi cha kusababisha kuwapo kwa mgawo wa maji.

“Mgao wa maji upo siku nyingi kwa mfano katika Kata ya Isyesye wanapata maji kuanzia saa 12:00 alfajiri hadi saa 3.30 asubuhi kila siku,’’ anasema Alfa Mwaluswa wa eneo la Madukani.

Mwaluswa ambaye ni fundi mwashi anasema kwamba mgao huo umesababisha wakazi wengi kuishi na ndoo, mapipa au madumu ya maji vyumbani huku wakibana matumizi ya maji kwa njia mbalimbali zikiwamo za kupunguza kuoga.

Naye Bryson Mwakitalima wa Kata ya Ilemi anasema kwamba suala la maji ni kero ya siku nyingi kwa wakazi wengi wa huko na kutoa mfano kwamba yeye analo bomba kwenye nyumba yake, lakini kwa miaka mingi sasa maji hayatoki katika bomba hilo.

“Uhaba wa maji umesababisha wengi waoge mara moja kwa siku jambo ambalo linachangia kuwapo kwa watu wanaotoa harufu mbaya,’’ anasema Mwakitalima.

Kwa ujumla upungufu wa maji unawafanya wananchi walio wengi kuyatumia kwa uangalifu mkubwa maji kidogo yanayopatikana.

Upatikanaji maji Mbeya

Takwimu za Mamlaka ya Usambazaji Majisafi jijini hapa, (Mbeyauwsa) zinaonyesha kuwa mahitaji ya maji katika jiji hilo ni meta za ujazo 48,000 kwa siku ambapo wateja wake ni 51,123.

Meneja Ufundi wa Mbeyauwsa, Ndele Mengo anasema kwamba mamlaka hiyo ina uwezo wa kuzalisha hadi mita za ujazo 51,466, lakini kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uchafuzi wa mazingira, uzalishaji unaporomoka hadi kufikia mita za ujazo 40,000 kwa siku hususan katika kipindi cha kiangazi.

“Mamlaka inawajibika kusambaza maji kwa wateja kwa muda wa saa 24, lakini ukweli hatujafikia kiwango hicho katika maeneo mengi kutokana na changamoto mbalimbali,’’ anasema Mengo.

Anafafanua kwamba pamoja na kuwa na vyanzo 13 vya maji, lakini havitoi maji ya kutosha huku maji yakizidi kupungua kwenye baadhi ya visima.

Utatuzi wa kero ya maji

Katika harakati za kuondoa kero kwa wateja wa maji, MBEYAUWSA wamelazimika kutafuta chanzo kingine cha maji ya uhakika wilayani Rungwe.

Meneja Ufundi, Mengo anasema kwamba mamlaka ililazimika kutumia zaidi ya Sh206 milioni kufanya upembuzi yakinifu kwa mradi wa kuchukua maji kutoka Mto Kiwira ambao upo umbali wa kilometa 47 kutoka kwenye chanzo hadi jijini Mbeya

“Andiko la mradi tayari limekamilika na kwa kuwa linahitaji fedha nyingi ambazo ni zaidi ya Sh 42 bilioni, mamlaka imeomba msaada Wizara ya Maji na tayari tulishapeleka andiko hilo wizarani,” anasema.

Mamlaka hiyo kwa sasa inakusanya wastani wa Sh14 bilioni kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo kutekeleza mradi huo.

Naye Meneja Uhusiano wa Mbeyauwsa, Neema Antony anafafanua kwamba mradi huo utajumuisha ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa kituo cha kuchuja maji, ujenzi wa matanki matano, njia ya maji ambayo itapita katika vijiji vya Unyamwanga, Ntokela vya wilayani Rungwe na katika vijiji vya Swaya 1 na Swaya 2 katika halmashauri ya Mbeya Vijijini.

Mradi huo ukikamilika utazalisha mita 106,000 za maji kwa siku wakati mahitaji ya maji jijini hapa ni mita za ujazo 48,000 na kwamba utasababisa watu waoge hata zaidi ya mara mbili.

Vijiji vinne kunufaika

Meneja Ufundi anasema kwamba katika mradi huo vijiji vyote vitakavyopitiwa na bomba vitapata maji ambapo vituo vya kuchota maji vitajengwa kila umbali wa mitaa 400 na kunufaisha zaidi ya wananchi 15,000 wa vijiji vyote vinne.

Mengo anapongeza uelewa wa viongozi pamoja na wananchi wote kwa jinsi walivyotoa ushirikiano katika kuelezea mradi huo ambao utakuwa chini ya ulinzi wa wananchi wenyewe.

Katibu Mkuu azungumza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alipoombwa kutoa maoni yake kuhusu mradi huo anasema kwamba bado hajaliona andiko la mradi huo lakini kama lilishatumwa litakuwa linashughulikiwa na maofisa wake.

Profesa Mkumbo anasema kwamba mradi wa Sh42 bilioni ni mkubwa kwa mamlaka peke yake kuutekeleza hivyo ipo haja kwa Wizara kusaidia kutafuta vyanzo tofauti vya fedha ili kusaidia kumaliza kero hiyo ya maji.

Wakati dunia ikiwa katika maadhimisho ya wiki ya maji ambayo leo ni kilele chake, ni imani ya wananchi wa Mbeya kwamba Serikali ya awamu ya tano itasaidia mradi huo ili wananchi hao wapate maji ya kutosha.