Njaa inavyoongeza utoro kwa wanafunzi wa kimasai,Wahadzabe na Wabarbeig

Muktasari:

  • Kwa kawaida huu ni muda wa mapumziko ya chakula cha mchana, lakini wanafunzi zaidi ya 30,000 wa shule za msingi 52 katika wilaya hizi kwa mujibu wa takwimu za halmashauri za wilaya, hawapati chakula cha mchana.

Yapata saa saba mchana, wanafunzi wa jamii za Kimasai, Kihadzabe na Kibarbeig wa Shule ya Msingi Kilimatinde, Meserani Juu, Matala wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha wapo katika makundi chini ya miti huku wengine wakicheza.

Kwa kawaida huu ni muda wa mapumziko ya chakula cha mchana, lakini wanafunzi zaidi ya 30,000 wa shule za msingi 52 katika wilaya hizi kwa mujibu wa takwimu za halmashauri za wilaya, hawapati chakula cha mchana.

Baada ya mapumziko, wanafunzi wanarejea darasani bila kula. Utulivu unakosekana na baadhi wanaanza kutoroka kurudi nyumbani kutokana na kushikwa na njaa.

Jonasi Sombe, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Kilimatinde, anasema kipindi cha mchana hawaelewi masomo kutokana na njaa na inawalazimu wengine kutoroka.

“Walimu wanafundisha lakini hatuelewi kama asubuhi kutokana na njaa. Tunaomba Serikali kusaidia kurejesha chakula katika shule yetu, kwani hata wazazi wameshindwa kuchangia kutokana na ukame,”anasema.

Wanafunzi wanataabika kwa sasa licha ya kuwa mwaka mmoja uliopita walikuwa wakinufaika na upatikanaji chakula cha mchana shuleni kupitia mpango wa chakula shuleni uliokuwa unaratibiwa na Serikali na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).

Mpango huo, kwa mujibu wa baadhi ya walimu wakuu, ulilenga kujenga lishe bora kwa wanafunzi, afya ya mtoto na kuwavutia wanafunzi kwenda shule.

Kwa kiasi kikubwa mpango huu, ulifanikiwa kuondoa utoro shuleni na kuongeza usajili na viwango vya ufaulu hadi kufikia wastani wa asilimia 86.

Upatikanaji huo wa chakula pia ulikuwa motisha kwa wanafunzi kupenda kuhudhuria masomo, hasa kutokana na jamii hizi za pembezoni kuathiriwa na mila na desturi kutopenda elimu.

Lakini pia kupatikana kwa chakula cha mchana kuliwaondolea adha ya kwenda shuleni asubuhi, kurudi nyumbani mchana kwa ajili ya chakula na kurudi shuleni, kwani jamii hizi zinaishi mbali na maeneo ya shule na kuna wanafunzi wanalazimika kutembelea takriban kilomita nne kwenda na kurudi shule.

Lakini kuanzia Januari 2016 Serikali ilipojiondoa kuchangia chakula katika shule za kutwa na kumalizika mpango wa chakula shuleni uliokuwa ukidhaminiwa na WFP, hali imebadilika.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini katika wilaya za Monduli na Karatu, umebaini utoro umefikia zaidi ya asilimia 30 kwa siku na baadhi ya wanafunzi tayari wameacha shule.

Katika wilaya hizi kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya na Kaimu Mkurugenzi halmashauri Karatu, Papaking Kaai, jumla ya shule 52 zenye wanafunzi zaidi ya 30,000 (wastani wa wanafunzi 600 kila shule) zimeshindwa kutoa chakula cha mchana.

Sababu zilizochangia, ukosefu wa chakula ni wazazi kugomea kuchangia kutokana na uelewa mdogo wa tamko la elimu bure, umaskini na walimu na viongozi wa Serikali kushindwa kushawishi michango.

Wilaya ya Monduli

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kilimatinde, Protisla Shirima anasema kukosekana chakula cha mchana kumekuwa na athari nyingi katika shule yake, utoro umeongezeka hasa vipindi vya mchana na uelewa wa wanafunzi unapungua.

Anasema kwa wastani kila siku wanafunzi zaidi ya 70 wanashindwa kufika shule huku wanafunzi zaidi ya 20 wakiwa wakitoroka vipindi vya mchana.

Mwalimu Shirima huku akionyesha barua za wito kwa wazazi kufika shuleni kujadili elimu, anasema imekuwa ni vigumu wazazi kuitikia wito.

“Kwa kupitia kamati za shule, tumeita vikao vya wazazi zaidi ya mara tano bila ya mafanikio. Hawafiki sasa tunaomba Serikali isaidie watoto wapate chakula,” anasema Shirima ambaye shule yake ina jumla ya wanafuzi 401 wakiwamo wasichana 275.

Mwalimu Martin Kaaya anasema shule hiyo tangu mwaka 2010, ilikuwa katika mpango wa kupata chakula kupitia shirika la kimataifa la WFP.

Anasema shirika hilo lilikuwa linatoa chakula cha mchana hadi mpango huo ulipositishwa mwaka 2014 na baada ya hapo wazazi na Serikali waliendeleza mradi huo.

“Mwaka 2015 tuliweza kuendelea kutoa chakula lakini tangu mwaka 2016 tumekwama kutokana na tangazo la elimu bure sasa wazazi hawachangii lakini pia kuna ukame katika kijiji chetu,”anasema.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kilimatinde, Nyangusi Sevite anakiri shule ya Kilimatinde kukwama kutoa chakula, lakini anasema kumechangiwa na ukame.

“Misimu miwili hatujapata mvua sasa hata kama tukilazimisha wazazi kuchangia chakula watapata wapi, tunajitahidi hata kutumia nguvu lakini inashindikana,”anasema.

Kilomita 40 kutoka katika Shule ya Kilimatinde, wanafunzi wa Shule ya Meserani Juu wilayani Monduli nao wanapitia changamoto.

Mwalimu wa shule hii, Fredrick Kimario anasema wameshindwa kutoa chakula kutokana na uchangiaji kukwama.

Anasema suala hilo linaathiri taaluma kwa kuwa wanafunzi wengi wanaishi mbali na shule umbali wa zaidi ya kilomita nne, hivyo kwenda shule asubuhi na kurudi nyumbani jioni na njaa ni tatizo.

Anasema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 687 wakiwamo wa kike 420 walijitahidi kufikisha katika kamati ya shule hoja ya uchangiaji chakula imekuwa vigumu kutekelezwa.

“Hali sio nzuri, utoro umeongezeka hata ufundishaji nyakati za mchana umeathirika sana kutokana na uelewa mdogo wa wanafunzi,” anasema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Meserani juu, Ngimasirwa Seraani anakiri Shule ya Meserani Juu wanafunzi wanakosa chakula.

Seraani ambaye pia ni kiongozi wa mila ya Kimasai maarufu kama Laigwanani, anasema tangazo la Serikali la elimu bure, halikueleweka kwa wazazi wengi na hivyo wakaamini hakuna michango ya chakula.

Diwani wa kata hiyo, Loti Tarakwa anasema tatizo hili ni kubwa wameanza kuhamasisha uchangiaji kupitia sheria ndogo za halmashauri na makubaliano ya vijiji.

“Tatizo la elimu bure wananchi walipokea vibaya na wakashindwa kuchanga, lakini pia hata shule zikawa hazina bajeti ya chakula sasa tunahamasisha uchangiaji, nyumba kwa nyumba na tutawakamata wanaogoma kuchanga na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria,”anasema.

Katika Shule ya Msingi Losingirani, iliyopo Wilaya ya Monduli, mwalimu mkuu msaidizi, Njumali Mollel anaeleza pia nao wamekwama kutoa chakula.

Anasema licha ya kupata kibali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri lakini wazazi wamegoma kuchangia.

Mwenyekiti wa kamati ya Shule ya Losingirani, Paulo Kavieti anasema uelewa mdogo wa jamii ya kifugaji imesababisha kukwama kwa uchangiaji chakula shuleni.

Kavieti anasema kuna wanasiasa wanaeleza Serikali ilitangaza elimu ni bure hivyo michango yote imefutwa, hivyo imekuwa vigumu katika uhamasishaji.

Karatu nako ni yaleyale

Wilaya ya Karatu ni moja ya wilaya ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mitihani, lakini kwa sasa viwango cha ufaulu vimeanza kushuka kutoka wastani wa asilimia 80 hadi 60 kutokana na wanafunzi kukosa chakula.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu, Papaking Kaai anasema kati ya shule 111 ni shule 72 zimeweza kutoa chakula huku shule 39 za vijijini ambazo wanafunzi wengi wa wabarbeig na Wahadzabe wakikosa chakula.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yamaweega, Qyubati Chagula iliyo zaidi ya kilomita 120 kutoka Karatu mjini, anasema wazazi kutothamini elimu ni moja ya matatizo makubwa ambayo yanawakabili.

Anasema wazazi wanapenda watoto wao, waende kuchunga mifugo na wasisome na hivyo hata wakati wa mitihani imekuwa ni kazi kubwa kuwapata watoto.

“Mwaka jana watoto waliofanya mtihani wa darasa la saba walikuwa ni watatu tu na safari hii tayari kuna wanafunzi watatu wameacha shule darasa la saba,” anasema.

Anasema ili kukabiliana na tatizo la chakula, shule imempata mfadhili mama wa kizungu, ambaye ana taasisi ya Dolfi & Gil Maunda jirani na shule hiyo ambaye amekuwa akiwapa msaada wa mahindi ya makande.

“Tangu katikati ya Agosti, mfadhili hayupo hivyo wanafunzi hawali lakini anarudi mwezi wa tisa katikati tunatarajia ataendelea kutupa mahindi ya makande,”anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bwawani Wilaya ya Karatu, Stevin Irambo anasema utoro ulifikia asilimia 12 kutokana na kukosekana chakula lakini tangu waanze kutoa chakula utoro umepungua.

“Shule hii iliwahi kuwa katika mpango wa kupatiwa chakula na Shirika la WFP tangu mwaka 2012 hadi 2014 baada ya WFP kujiondoa utoro ulirejea shuleni, lakini ilipofika mwaka 2017 tulianza kujipanga kuomba wazazi kuchangia chakula,” anasema.

Sheria, sera kuhusu suala la chakula shuleni

Sera ya elimu ya 2014 inaeleza kuwa Serikali itahakikisha kuwa huduma muhimu zikiwamo za chakula bora, majisafi na salama, na afya zinapatikana katika shule na vyuo.

Serikali katika sera ya elimu, inaahidi kuwepo kwa mazingira bora na yenye usalama katika utoaji wa elimu na mafunzo nchini.

Sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inawataka wazazi na walezi kuwa na wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba watoto wanaandikishwa na kwenda shule, wanafuatiliwa maendeleo yao shuleni, watoto wanasikilizwa na kupewa muongozo na mafunzo.

Pia, tamko la elimu bure kupitia waraka waraka namba 5 wa mwaka 2015 na ufafanuzi namba sita wa waraka huo, unaeleza wajibu wa Serikali na wajibu wazazi kununua sare za shule na michezo, madaftari na kalamu, kugharimia chakula kwa wanafunzi wa kutwa pamoja na matibabu ya watoto wao.

NGOs wanalitazamaje tatizo la chakula shuleni

Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma za Jamii za Pembezoni (CORDs) Lilian Lootoitai anasema tatizo la ukosefu chakula kwa shule za jamii za pembezoni ni kubwa na limeathiri tamko la elimu bure.

Anasema ili kukabiliana na tatizo hilo, shirika hilo limeanza kutoa elimu kwa kamati za shule na walimu wakuu kuwajengea uwezo wa kuitisha vikao vya kuchangisha fedha na pia kukabiliana na matatizo katika shule.

“Tumeona kama shirika hatuwezi kutoa chakula moja kwa moja kwani sio mpango endelevu, tunatoa elimu kwa kamati za shule kuweza kukusanya michango lakini pia tunasaidia kuboresha miundombinu ya shule,” anasema.

Ofisa masuala ya vijana na Jinsia wa Mtandao wa mashirika ya wafugaji nchini (PINGOS Forum), Nailejileji Tipap anasema sera ya elimu bure imekuwa na matatizo kwa jamii za pembezoni kwani ilipaswa ufanyike kwanza utafiti kuona uzuri na ubaya wake hasa kwa jamii za kifugaji na wala matunda.

“Utoro umeongezeka, ufaulu utashuka ni vyema Serikali ikarejea mpango huu ili kuhakikisha wanafunzi wanapewa chakula, kwani ni vigumu wazazi wa jamii hizi kuchangia chakula kutokana na kutothamini elimu kwa watoto wao,” anasema.

Halmashauri zatoa msimamo

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya anasema tatizo la ukosefu wa chakula katika shule 13 za wilaya yake limekuwa na athari kwa wanafunzi na anatoa wito kwa wazazi kuchangia chakula.

Anasema kati ya shule za msingi 59 katika wilaya yake ni shule 46 tu nyingi zikiwa za mjini ndio zinatoa chakula na shule 13 za vijijini zimekwama kutoa chakula.

“Naomba nitumie fursa hii, kuwashauri wazazi wajitokeze kuchangia chakula shuleni kwani ni wajibu wao kutokana na waraka wa elimu bure na nimeagiza viongozi wa serikali za vijiji na kata kusimamia jambo hili kwa kutumia sheria,”anasema.

Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Karatu, Papaking Kaai anasema shule 39 kukosa chakula katika wilaya yake ni tatizo kubwa na sasa ameagiza walimu wakuu kushirikiana na kamati za shule kutatua tatizo hilo.

Kaai ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu, anasema tatizo ni kubwa zaidi kwa shule za pembezoni na ameagiza waratibu wa elimu kushirikiana na walimu wakuu, kutatua mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuhakikisha shule zote zinatoa chakula cha mchana.