Nyanda, Mtanzania mwenye utata wa jinsi

Mwanaharakati wa masuala ya afya ya uzazi, Mwamba Nyanda. Picha na Florence Majani

Muktasari:

  • Hakika, Nyanda ni mwanamume anayejipenda. Kama mwanamke atakuwa hajavutiwa na uvaaji wake basi anaweza kunaswa na mwendo wake au sauti au sura yake.
  • “Mambo kaka,” nilimsalimia tulipokutana huku tukitafuta mahali pa kukaa. “Poa,” alinijibu. Hiyo ndiyo siku nilipoifahamu historia ya maisha na shughuli zake za uanaharakati wa masuala ya afya ya uzazi, mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi (VVU) na anavyojihusisha na biashara na muziki.

Kwa mara ya kwanza nilipomuona mwanaharakati wa masuala ya afya ya uzazi, Mwamba Nyanda maeneo ya Sinza, Dar es Salaam nilivutiwa na mwonekano wake, nikajawa shauku ya kutaka kukaa karibu naye. Nilifanya miadi nikafanikiwa kuonana naye.

Hakika, Nyanda ni mwanamume anayejipenda. Kama mwanamke atakuwa hajavutiwa na uvaaji wake basi anaweza kunaswa na mwendo wake au sauti au sura yake.

“Mambo kaka,” nilimsalimia tulipokutana huku tukitafuta mahali pa kukaa. “Poa,” alinijibu. Hiyo ndiyo siku nilipoifahamu historia ya maisha na shughuli zake za uanaharakati wa masuala ya afya ya uzazi, mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi (VVU) na anavyojihusisha na biashara na muziki.

Pamoja na utanashati, mvuto, uwezo wa kujenga hoja na sauti yenye ushawishi kuna kitu kinachomfanya akose raha maishani mwake. Kitu hicho si kingine bali utata wa jinsi yake.

Kwamba ingawa sauti, muonekane, mavazi na mwendo wake vyote vinamtambulisha kuwa ni mwanamume, sura yake inamuonyesha kuwa ni mwanamke. Kwamba ingawa yeye anajiona ni mwanamume kamili, jamii inayomzunguka hata baadhi ya ndugu zake wanamuona ni mwanamke.

Maisha yake tangu utotoni yamesongwa na namna ya kukabili ukweli kuhusu utata wa jinsi yake.

Kwa Kiingereza Nyanda ni ‘intersex’ yaani hali ya kibaolojia, ambapo mtu huzaliwa akiwa na viungo vya uzazi, vichocheo, tabia au mwonekano wa nje ambao haumuweki katika kundi lolote la kuwa mwanamke au mwanamume au akiwa na sifa za kibaolojia zilizochanganyika kutoka jinsi zote mbili.

Jamii imwelewe

Hivi sasa anataka jamii ikubaliane na hali halisi, kwamba yeye ni mwanamume. “Mimi ni mmoja, wapo wengi wanaopitia shida kama zangu ambazo ni ngumu zaidi, nataka niwe kioo cha jamii kwa kuwa jasiri katika mazingira haya,” anasema.

Alizaliwa miaka 26 iliyopita mkoani Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya wawili katika familia yao. Kadri alivyozidi kukua alianza kujiona yeye si mwanamke kama wazazi wake walivyokuwa wanamweka na alijiona tofauti na jina walilompa hadi akiwa na umri wa miaka sita.

“Nilianza kujisikia wa tofauti, yaani sipendi kucheza na watoto wa kike, sipendi mavazi ya kike waliyokuwa wananivalisha yaani sikujisikia mimi eti ni mtoto wa kike,” anasema.

Kadri siku zilivyokuwa zikisogea, ndivyo wasiwasi ulivyoongezeka na akijiuliza maswali, itakuwaje ukifika wakati akavunja ungo au akaota matiti? “Nilichelewa kuota matiti na hata yalipoota yalikuwa madogo sana, huwezi kuyaona, lakini nilikuwa nawaza, hivi nitabalehe?”

Hali hiyo ilimfanya awe mpenzi wa magazeti hivyo alitumia muda mwingi kusoma magazeti akidhani angesoma mahali maelezo ya dawa ya kutibu au kuzuia hedhi au kuota maziwa. Lakini hakuwahi kupata tiba hiyo.

Maisha yaliendelea huku mtihani ukizidi kuwa namna ya kutegua kitendawili cha jinsi yake na jamii ikamwelewa. Alipofikisha umri miaka 15-16, alizidi kuwa na mwonekano wa kiume, sura, sauti mpaka koromeo lake lilijitokeza kama ilivyo kwa wanamume.

Mabadiliko hayo pia yaliwapa changamoto wazazi wake. Hapo ndipo mama yake aliyefikiri mwanaye anakabiliwa na mapepo, aliamua kumchukua na kuanza kupita katika makanisa ili afanyiwe maombi.

“Ilifikia mahali hata mimi nilidhani huenda kweli nina mapepo. Ilinipa shida,” anaeleza.

Mazingira mengine magumu yalikuwa shuleni. “Hali ya shuleni ilikuwa ngumu. Nilihisi shule nzima niko peke yangu. Nakumbuka nilishawahi kusimamishwa mbele na kuadhibiwa kisa muonekano wangu,” anasema.

Mwalimu wa zamu siku hiyo aliamua kumpa adhabu kwa madai ya kujiweka kiume licha ya kwamba alikuwa anavaa sare za shule za kike. Mbali ya kuadhibiwa na walimu mara kadhaa aliingia katika mzozo na wanafunzi wenzake.

Wapo waliomwita tomboy (msichana ambaye anaonyesha hulka na tabia zinazofikiriwa kuwa za kiume kama kuvaa nguo za kiume na kushiriki kazi na michezo ya aina hiyo ambayo kwa utamaduni inafikiriwa si ya kike). Wengine walimwita dumejike na majina mengi ambayo hayakumfurahisha.

Pia, wakati mwingine alikuwa anaingia katika mabishano mazito na wenzake kuhusu suala la jinsi. “Wao wanasema kuna jinsi mbili mke na mume, mimi najaribu kuwaelimisha kuwa zipo tatu; me, ke na jinsi tata ambao huitwa dume jike. Na kuna dhana kwenye jamii kuwa wapo watu wanaozaliwa na jinsi mbili, kitu ambacho bado jamii inakosea,” anasema.

“Wengine wanasema nawachanganya. Wengine eti nawaletea mambo ya Ulaya. Wanasema hakuna watu kama hawa katika jamii wakati tafiti zipo zinaonyesha kama tupo na jinsi tunavyopata shida,” anasema.

Hata hivyo, Nyanda hakutaka kuweka wazi iwapo ana jinsi mbili.

Kukosa kazi

Jamii haikumwelewa wakati ule na hadi sasa bado haimwelewi. Mara kadhaa amefukuzwa katika nyumba za kupanga kutokana na mwonekano wake na amekuwa akikosa ajira.

“Yaani kutokana na jinsia na mwonekano hata kama nina elimu sipewi ajira, hii imenitokea mara kadhaa sitaki kutaja kampuni si vizuri, ila Mungu anawaona,” anaeleza.

Aliwahi kupeleka barua ya maombi ya kazi katika kampuni moja, akaitwa kwenye usaili, lakini baadaye wakaanza kumhoji kuhusu jinsi yake na wala si masuala ya kazi aliyoomba. Baada ya hapo, hakuitwa tena.

“Kwingine nikiomba kazi wanaishia kusema kweli ninafaa, nina vigezo vyote lakini hawawezi kuniajiri kutokana na utambulisho na muonekano wangu.

“Hili la kukosa kazi halijanitokea mara moja, hali hiyo ilinipelekea kuninyanyapaa kisaikolojia juu ya ajira nchini,” anasema.

Kunyanyapaliwa na wenye nyumba

“Utakuta napokewa vizuri kwenye nyumba ya kupanga lakini sijui watu wanatokea wapi na kumletea mwenye nyumba maneno. Basi baada ya siku mbili tatu, nafukuzwa kwenye nyumba,” anasema.

Siku moja alipokuwa katika baa moja jijini alijikuta akifuatwa na watu alipoingia choo cha wanaume, ambacho kwake ni sahihi kwa sababu anaamini yeye ni mwanamme.

Japokuwa mama yake hakuwa anaikubali hali aliyonayo, baba yake amekuwa akimtia moyo. ‘’Usitetereke na wala usisikilize wanayosema mabaya juu yako. Usiogope, cha muhimu ishi na watu vizuri,” anasema akinukuu maneno ya baba yake.

Mazingira haya yamemfanya awe mwanaharakati wa masuala ya afya ya uzazi, virusi vya ukimwi nafasi inayompa fursa ya kufanya kampeni jamii imuelewe na isimnyanyapae pamoja na wengine wengi wa aina yake.

Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa idadi ya watu wenye jinsi tata duniani ni asilimia 1.7. Kadhalika, Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ripoti yake ya 2015 kuhusu miongozo ya afya ya jinsia, haki za binadamu na sheria limeeleza kuwatambua watu wenye jinsi tata.

“Jinsi tata ni kasoro za kimaumbile kama zilivyo nyingine na hivyo wasibaguliwe, wapewe huduma za afya wala wasitengwe,” inasema ripoti hiyo.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kutetea afya kwa makundi maalumu nchini (CHESA), John Kashia anasema mtazamo hasi juu ya watu wa kundi hili ndiyo unaosababisha wakati mwingine wakose hata huduma za afya.

“Wizara ya afya inatakiwa iwape elimu watu hawa, iwatengenezee mazingira rafiki wafikapo katika vituo vitoavyo huduma za afya,” anasema.

Kashia anasema kadri unyanyapaa unavyozidi ndivyo wanavyogeuka kuwa watu hatari au hata wanapata magonjwa.

Pia, amewahi kuhubiriwa alipokwenda hospitali kupata huduma. Madaktari na washauri wanamuuliza maswali mengi ambayo lengo si kumsaidia bali kutaka kujua au kujifurahisha.

Semenya na Odiele

Utata wa jinsi alionao Nyanda ni kama ule wa mwanariadha Caster Semenya wa Afrika Kusini, mshindi wa medali ya dhahabu katika mbio za mita 800 kwenye Michezo ya Olimpiki 2016 na ubingwa wa dunia 2009.

Semenya mwenye mwonekano wa kiume na baadhi ya sifa za mwanamke, alianza kupata changamoto mwaka 2009 wakati huo akiwa na umri wa miaka 18, baada ya kushinda mbio za wanawake za mita 800. Wanariadha wenzake walilalamika kuwa si mwanamke iweje ashiriki mbio za wanawake?

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), Pierre Weiss alisema; “Semenya ni mwanamke lakini inawezekana siyo kwa asilimia 100.”

Baadaye alizuiwa kushiriki mashindano hadi alipopimwa na kuonekana ana korodani kwa ndani, homoni za kike kwa kiasi fulani, nyumba ya uzazi lakini na uume mdogo.

Pia, Nyanda ni kama alivyo mwanamitindo wa Kibelgiji, Hanne Gaby Odiele ambaye amejitambulisha Januari mwaka huu. Odiele ana baadhi ya sehemu za kiume, kama korodani zilizojificha kwa ndani na sehemu za kike kama matiti, lakini hana nyumba ya uzazi huku mwendo na sauti yake vyote ni vya kiume.