Ukosefu wa huduma za afya unavyowaathiri wakazi wa Kisegese wilayani Rungwe

Muktasari:

  • Wakazi hao wamekuwa waathirika wa kushindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma za afya nje ya kata yao.

Moja ya vitu ambavyo wakazi wa Kata ya Kisegese katika Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya wanaomba visiwatokee ni kuugua wakati wakiwa kwenye eneo hilo.
Wakazi hao wamekuwa waathirika wa kushindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma za afya nje ya kata yao.
Wananchi hao wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kwenda kutafuta huduma hiyo muhimu katika vituo vya afya vilivyopo kwenye kata za wilaya jirani ya Kyela.     Kata ya Kisegese ambayo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ina wakazi 10,000, wamekuwa wakipata taabu muda mrefu kwa kukosa huduma ya afya jirani na makazi yao kutokana na kutokuwa na kituo cha afya wala zahanati.
Safari ya kufuata huduma hizo katika wilaya jirani huwagharimu wagonjwa siku nzima na kiasi kikubwa cha fedha.
Mkazi wa Kijiji cha Kasyabone, Fabian Mwakifuna anasema licha ya kituo cha afya cha Ipinda na Hospitali ya Matema wilayani Kyela kuwa mbali, lakini ni gharama nafuu zaidi kufika huko kuliko maeneo ya wilaya hiyo zinakopatikana huduma hizo.
“Tunaenda kutibiwa Matema na Ipinda wilayani kyela kutokana na urahisi wa kufika huko na tunashindwa kwenda hospitali zilizopo kwenye wilaya yetu kutokana na miinuko mikali ambayo tunashindwa kuimundu,” anasema Mwakifuna.
Mwakifuna anasema kwa kuwa kipato chao ni kidogo wanashindwa kumudu gharama za kukodi usafiri wa kwenda na kurudi katika Hosptali ya Itete kwa maelezo kuwa ni ghali ukiringanisha wanapokodi kwenda Matema au Ipinda.
“Kukodi pikipiki kwenda Matema au Ipinda ni Sh15, 000 wakati kwenda Hosptali ya Itete tunakodi pikipiki Sh20, 000 mpaka Sh25, 000 na hii inatokana na Itete kuwa na minuko mikali iliyopo katika milima ya Ipyasyo na Kibole,” anasema Mwakifuna.

Kutokana na ubovu wa barabara katika eneo hilo, hakuna usafiri wowote wa basi kwenda makao makuu ya halmashauri hiyo ambao unaweza kuwarahisishia wakazi wa kata hiyo kufika mapema hospitalini pindi wanapougua.

Barabara kutoka Lwangwa ambako ndiyo makao makuu ya halmashauri ya Busokelo imejaa mashimo pamoja na mawe makubwa na yenye ncha kali kiasi wenye magari kulalamika kuwa wakitembelea wiki mbili hutahitajika kununua mataili mapya.

Sanjari na ubovu wa barabara kuna miinuko mikali ambayo inahitaji umakini wa hali ya juu unapoendesha chombo cha moto kwa kuwa unaweza kujikuta umetumbukia na mgonjwa kwenye maporomoko ya Mto Lufilyo unaomwaga maji yake katika Ziwa Nyasa.

Gharama hizo siyo tu zinapukutisha vipato vya wakazi hao, pia muda wanaotumia kusafiri na kusubiri huduma katika hospitali hizo za jirani unawapunguzia ufanisi katika shughuli za kujiingizia kipato hasa pale wanapokuwa wanaumwa ugonjwa ambao wangetibiwa na kuendelea na shughuli zao.

Joseph Mwanjabupe, mkazi wa Kijiji cha Kasyabone anasema chanzo cha wananchi wa kata hiyo kushindwa kujikwamua kiuchumi ni pamoja na wengi wao wanapougua hutumia muda mwingi kufuata huduma za matibabu wilaya jirani ya Kyela.

“Huwa mtu anapopata shida anatumia wiki nzima kuhangakia matibabu sasa muda anaotumia kuhangakia matibabu shughuli za uzalishaji zinakwama,”anasema.

“Tumeshindwa kuendeleza vitega uchumi vyetu kwa ajili ya familia zetu kutokana na tatizo tulilonalo hapa kwetu la ukosefu wa huduma za afya kwa kuwa tunalazimika kwenda kupata matibabu Kyela ambako ni mbali na makazi yetu,” anasema.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Timia Michael anasema tatizo la ukosefu wa huduma za afya katika kata yao limechangiwa kwa kiwango kikubwa wananchi kutokuwa na uchumi mzuri.

Timia anasema, mbali na wakazi wengi kuwa na uchumi mbovu, pia wazazi wengi wanashindwa kumudu kuzihudumia familia zao ipasavyo kutokana na uchumi wao kuzorota.

“Tunapougua huwa tunakosa kabisa muda wa kuwapatia malezi mazuri watoto wetu kwani muda ambao ulitakiwa kuwaandalia chakula tunatumia kufuata huduma za afya katika hosptali ya Mtema na Ipinda,” anasema Timia.

Licha ya kukosekana kwa usafiri, mawasiliano bado ni tatizo kwa wakazi hao. Mitandao ya simu bado haijawafikia hivyo wanapopata matatizo humteua mtu kwenda kuita gari Ipinda ambapo ni rahisi kuyakuta magari ya kusafirisha wagonjwa.

“Hapa kwetu usafiri wa magari ni shida kiasi kwamba tukipata tatizo tunamteua mmoja wetu kwenda Ipinda kukodi taxi kwa Sh50,000 au tunakodi pikipiki za hapa kijijini kwetu lakini kwa mgonjwa ambaye hajazidiwa sana,” anasema mkazi wa Kijiji cha Ngereka, Happy Godfrey.

Hata hivyo, wakazi wanaeleza kuwa siku wanazozitumia kufuata huduma zinawakwamisha kujiinua kiuchumi kutokana na nguvu kazi yote kuhamishia kutafuta huduma za matibabu.

Mkazi wa kijiji hicho, Jonas Nikodemu anasema yeye anajishughulisha na ukamuaji mafuta ya mawese ambayo kwa siku humwingizia kati ya Sh10, 000 na Sh15, 000.

Nikodemu anasema inapotokea mtoto au mke ameugua hulazimika kuacha shughuli zake za kila siku za kumwingizia kipato na kuanza kuhangaikia matibabu ya familia yake.

“Ninapopatwa na matatizo ya magonjwa kwenye familia yangu najikuta shughuli zangu zinakwama kwani muda ninaotumia kutafuta huduma za matibabu ndiyo ambayo nilitakiwa kukamua mafuta ya miwese ili nitengeneze mafuta ya kuuza.

“Hii shughuli ndiyo inaendesha familia yangu na kusomesha watoto wangu ambao mmoja anasoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kisegese.”

Diwani wa Kata ya Kisegese, Edson Mbila anasema Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya alifika katika kata hiyo Julai mwaka huu na kuwaagiza wenyeviti wa vijiji kuhakikisha kila kijiji kinafyatua matofali 10,000 kabla ya Oktoba mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.

Ujenzi wa kituo cha afya

Mbila anasema ili kuondokana na adha hiyo, kata kwa kushirikiana na halmashauri imendaa mpango mkakati wa kujenga kituo cha afya na zahanati katika Kijiji cha Ngereka na tayari maeneo yametengwa na wananchi wa kijiji hicho.

“Tumetenga eneo lenye ukubwa wa hekta tano kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pamoja na nyumba za waganga, lakini pia wananchi wa kijiji cha Ngereka wametenga eneo lenye ukubwa wa hekta mbili kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.

“Hatua hii imefikia baada ya kupeleka kilio kwenye vikao vya halmashauri na kata yangu imetengewa Sh20 milioni kwa ajili ya kituo cha afya,” anasema.

Mbila anaongeza kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo hilo wananchi wamehamasika kwa kiwango kikubwa kuchangia michango ambapo kila mwananchi anachangia kiasi cha Sh5, 000 na ambao hawana kiasi hicho wameahidi kutumia nguvu kazi zao ili mradi tu waepukane na adha hiyo ya muda mrefu.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Busokelo, Gilbert Tarimo anasema katika mwaka wa fedha ujao wanatarajia kipaumbele kikubwa kitakuwa ni afya kutokana asilimia kubwa ya wananchi wa halmashauri hiyo kuwa mbali na huduma za afya kwa muda mrefu.

“Mwaka wa fedha ujao tunatarajia 2018/19 kipaumbele kikubwa katika bajeti yetu itakuwa ni ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ambapo wananchi watashiriki kujenga mpaka mgongo wa panya harafu sisi tutamalizia sehemu itakayobaki,” anaeleza Tarimo.

“Maeneo ambayo wananchi tumepanga kujenga vituo vya afya na zahanati ni pamoja na kata za Lufilyo, Mpombo, Kambasegera, Ntaba, Lupata na Lukasi kwani maeneo hayo huduma za afya bado mbaya ndiyo maana halmashauri inataka kujikita kupekeka huduma haraka,” anaongeza.

Kata ambazo zimelengwa kujengewa vituo vya afya na zahanati kwa mujibu wa Tarimo ni zile zinazoongoza kupeleka wagonjwa katika hospitali teule ya Itete ambapo kwa siku hupokea wagonjwa 10 hadi 20.

“Huwa tunapokea wagonjwa 10-20 kutoka kwenye kata nilizokutajia na ukizingatia muundo wa halmashauri yetu ilivyo kuwa na miinuko mikali, miundombinu ya barabara tukagundua kwamba wananchi wanasumbuka sana mpaka kufika hospitalini hapa ndiyo maana tukaona kuna haja ya kuwajengea vituo vya afya kama sera ya mwaka 2007 inavyoelekeza,” anasema.

Kauli ya mkurugenzi wa halmashauri

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Eston Ngilangwa anasema Serikali inatambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi wake.

Kutokana na kutambua kuwa maendeleo ya nchi yataletwa na wananchi wenye afya bora, kwa sasa uhamasishaji wa ujenzi wa zahanati na vituo vya afya kwenye vijiji na kata katika halmashauri hiyo umeshika kasi na wameagiza kila kijiji kifyatue matofali.

“Halmashuri yangu ina kata 13 lakini kata tano zimeanza kuonyesha matumaini ya kwanza kujenga vituo vya afya kwani tayari wameanza shughuli za kufyatua matofali na wengine wanaitisha harambee kwa ajili ujenzi huo,” anasema.

Wadau wanasema ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya, Serikali haina budi kuwekeza ipasavyo katika kujenga zahanati na vituo vya afya kila kijiji na kata kama Sera ya Afya ya mwaka 2007 inavyoelekeza.

Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Elimisha, Festo Sikagonamo anasema kwa matatizo wanayokumbana nayo wakazi wa Kata ya Kisegese Serikali inapaswa kutekeleza kwa vitendo ahadi ambazo imekuwa ikitoa mara kwa mara kwa wakazi hao.

“Asasi yangu ilifika katika kata hiyo mwaka 2014 na kuangalia hali halisi ya wakazi hao. Kiuhalisia hali ni tete Serikali inabidi iwaangalie kwa jicho la karibu wakazi hao kwani tutapoteza nguvu kazi ya kizazi kijacho kwa kuwa wanaoathirika kwa asilimia kubwa ni watoto,” anasema.