Umoja wa Ulaya wazungumzia sakata la viongozi Chadema

Muktasari:

  • EU kupitia balozi anayewakilisha ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland van de Geer imetoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu ujumbe wa wabunge na madiwani hao wa Chadema ambao walikwenda katika ofisi hizo, Alhamisi iliyopita.

Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU), umezungumzia malalamiko yaliyotolewa na wabunge wa Chadema ‘walioandamana’ kwenda katika ofisi za umoja huo jijini Dar es Salaam, ukitaka demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu viheshimiwe ili kupambana na umasikini.

EU kupitia balozi anayewakilisha ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland van de Geer imetoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu ujumbe wa wabunge na madiwani hao wa Chadema ambao walikwenda katika ofisi hizo, Alhamisi iliyopita.

“Umoja wa Ulaya unaendelea na mijadala na Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kidini, vyama vya siasa na taasisi nyinginezo katika hali ya uwazi,” alisema Balozi de Geer kupitia barua pepe aliyoituma Mwananchi.

Alhamisi iliyopita, baadhi ya wabunge na madiwani wa Chadema ‘waliandamana’ kwenda ofisi za umoja huo kuwasilisha kile walichoeleza kuwa ni masuala mbalimbali yanayowakumba viongozi wakuu wa chama hicho, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kupewa dhamana.

Walikwenda ofisi za EU wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiendelea kusikiliza kesi inayowakabili viongozi sita wakuu wa chama hicho akiwamo mwenyekiti, Freeman Mbowe ambao hata hivyo siku hiyo hawakufikishwa Kisutu kutoka Gereza la Segerea, ikielezwa kuwa gari lililopaswa kuwafikisha liliharibika.

Mbali na Mbowe, viongozi wengine wanaokabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kisutu ni katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko.

Katika kesi hiyo licha ya washtakiwa wote kuelezwa kuwa dhamana ipo wazi, Hakimu wa Mahakama ya Halimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri alitaka wafikishwe mahakamani hapo Jumanne ijayo na kila mmoja atatakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni na kuwa na barua kutoka kwa viongozi wa vijiji au mtaa.

Akizungumza baada ya kutoka ubalozi wa EU, meya wa Ubungo, Boniface Jacob alisema miongoni mwa mambo waliyowaeleza wawakilishi hao wa Jumuiya ya Ulaya ni ukandamizaji wa demokrasia na utawala bora, kitendo cha viongozi wao kuendelea kusota gerezani, matukio ya mauaji na utesaji kwa viongozi na wanachama wa Chadema pamoja na nguvu inayotumiwa na Jeshi la Polisi.

Jacob, ambaye pia ni diwani wa Ubungo alisema masuala mengine ni kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya na uhuru wa Mahakama.

Baadhi ya wabunge waliofika kwenye ofisi hizo ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Cecil Mwambe (Ndanda), Peter Lijualikali (Kilombero), Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mikumi) na wabunge wa viti maalumu; Jesca Kishoa, Cecilia Paresso, Anatropia Theonest na Susan Mwakagenda.

Kauli ya EU

Katika barua pepe hiyo, Balozi Geer alisema umoja huo unaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuleta maendeleo, demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu.

“Machi 29, ujumbe wa Chadema walileta malalamiko kuhusu hali inavyoendelea Tanzania kwa Umoja wa Ulaya na kwa kuwajibu, tunarudia kusema tutaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo ikiwa pamoja na kuondoa umasikini, kwa demokrasia, utawala wa sheria na heshima kwa haki za binadamu,” alisema Balozi Geer katika barua pepe hiyo.

Alisema EU imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Tanzania na imekuwa ikiwasiliana na Serikali, mashirika yasiyo na kiserikali na taasisi.

“Hata hivyo, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zimeshaeleza masikitiko yake kuhusu matukio yanayoendelea nchini katika taarifa yake iliyotoa Februari 23, 2018 na imepata majibu kutoka serikalini,” alisema.

Katika tamko hilo la Februari 23, umoja huo ulieleza matukio ya utekaji na mauaji yanayotokea nchini, ukiitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina.

Taarifa yao hiyo ilitolewa na ushirikiano wa mabalozi wa nchi wanachama wa umoja huo wenye uwakilishi Tanzania na kuungwa mkono na mwakilishi na mabalozi wa Norway, Canada na Uswisi.

Ulieleza kushuhudia kwa wasiwasi mwendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayotishia nidhamu ya demokrasia na haki za Watanzania, katika nchi iliyojizolea umaarufu mkubwa duniani kwa utulivu, amani na uhuru.

Walieleza kusikitishwa na kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi Februari 16, mwaka huu Akwilina Akwilini.

EU ilitoa wito wa kuchunguzwa kwa kina kwa vifo vyote vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu.

Umoja huo ulitoa pole kwa familia zao zote, kuonyesha wasiwasi na ongezeko la ripoti za ukatili katika miezi ya hivi karibuni kama vile jaribio lililohatarisha maisha ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu; kupotea kwa watu kama mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Mwananchi mkoani Pwani, Azory Gwanda na mashambulio yaliyopoteza uhai wa viongozi wa kisiasa.

Mashtaka viongozi wa Chadema

Viongozi hao sita wa Chadema wanakabiliwa na jumla ya makosa manane, likiwamo la kuhamasisha uasi, chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani, waligoma kutii amri ya kusambaratika na kuvunja mkusanyiko huo uliosababisha kifo cha Akwilina huku maofisa wa polisi wakipata majeraha.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni anadaiwa kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali na ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai. Mchungaji Msigwa anashtakiwa akidaiwa kushawishi raia kutenda kosa la jinai.