Wajane katika mpango kazi wa kuukimbia unyanyasaji

Mkurugenzi wa Tawia,Rose Sarwat akizungumza katika mkutano wa wajane wa nchi za maziwa makuu.

Muktasari:

Wajane hao walikutanishwa na Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (Tawia), ambapo pamoja na mambo mengine waliweza kuonyesha bidhaa ambazo wanazitengeneza na kuziuza kwa ajili ya kukabiliana na maisha.

Hivi karibuni, wajane kutoka nchi za ukanda wa Maziwa Makuu walikutana jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna ya kuzitatua.

Wajane hao walikutanishwa na Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (Tawia), ambapo pamoja na mambo mengine waliweza kuonyesha bidhaa ambazo wanazitengeneza na kuziuza kwa ajili ya kukabiliana na maisha.

Nchi zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na DR Congo, Malawi, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.

Mkurugenzi wa Tawia, Rose Sarwat, anasema kwamba katika kila shuhuda aliyesikilizwa kutoka nchi hizo kuna matukio ya kufanana huku mambo makuu yakiwa ni mila na desturi, sheria mbovu za serikali na kuamua kuja na mpango kazi wa pamoja kuhusu nini cha kufanya.

Anasema kwamba katika mkakati huo wangependa kuona nchi hizo zinapitia upya sera na sheria ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiwakandamiza wajane ikiwemo ile ya mirathi.

Katika kulifanikisha hilo, Rose anasema kwamba wamejipanga kushirikiana kwa karibu na viongozi wa kisiasa, serikali na wale wa dini ambao wana nafasi kubwa katika kuibadilisha jamii dhidi ya mtazamo walionao wajane.

“Katika moja ya tamko tulilotoka nalo katika mkutano huo uliochukua siku tatu ni kuhamasisha pia uandikaji wosia kwa kinababa ili kuwaepusha wajane kuja kupata tabu hapo baadaye.

“Hii ni ampeni ambayo tunatarajia kuianza Aprili mwaka huu.

“Wakati wakifikiria kujipanga maisha ya kustaafu wajue pia kuna kifo tena hii haina taarifa bora kustaafu unajua tarehe, siku na mwaka, ifike mahali watu wasiogope kuandika wosia kwa hofu ya kujichulia kufa kwani kifo kipo tu hakikwepeki,”anasema Rose.

Hata hivyo anasema kwamba ili kukabiliana na unyanyasaji wa wajane, jamii hususuani ndugu wa mume wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu, kwani wengi wao wamekuwa wakimdhulumu mama mfiwa na kujikuta anaanza moja katika maisha na kwa wale wanaoshindwa kuhimili hufikia hatua hata ya kujiua.

Jingine anasema kwamba ipo haja ya uwekwaji wa sera au sheria kimaandishi itakayomlinda mjane mara tu anapompoteza mume wake kwani kutokuwepo hilo kumewapa nafasi watu kuwanyanyasa.

Kwa upande wa viongozi wa dini, Rose anasema kwamba ni vema wakawa wanasisitiza umuhimu wa kuwajali wajane katika ibada za maziko za waume zao ili jamii na ndugu wote wawasikie na kuongeza kuwa ni vema kuwa na utamaduni wa kuzitembelea mara kwa mara familia hizo.

Kwa majirani wa wajane, Mkurugenzi huyu anasema kwamba ni vema wakaacha tabia ya kufumbia macho pindi wanapoona mama ananyanyaswa kwa kuwa wao ndio watu wanaoishi nao karibu na hivyo wanatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika jambo likalowatia woga wenye nia mbaya dhidi ya wamama hao wajane.

Viongozi wa dini wanena

Baadhi ya viongozi wa dini ambao walialikwa katika mkutano huo akiwemo Sheikh kutoka Msikiti wa Khadir Kigogo Post jijini Dar es Salaam, Said Omar, anasema kwamba kufiwa na mume sio mwisho wa maisha na kuitaka jamii kuwaheshimu wajane.

Omar anasema kwamba wakati watu wakiwadhulumu wajane, Uislam unamtambua mjane kuwa na haki zote za kurithi mali za mumewe kulingana na idadi ya watoto alionao.

Wakati kwa wale aambao wana tabia ya kurithi wake za ndugu zao, anasema kwamba taratibu zote zinapaswa kufuatwa ikiwemo kulipa mahari na mwanamke mwenyewe kuridhia jambo hilo na si mambo ya kulazimishana kama wanavyofanya baadhi yao.

Naye mwakilishi kutoka Kanisa Katoliki Kariakoo jijini Dar es Salaam, Heavenlight Swai, anasema kwamba imefika mahali wajane wamezeeka kutokana na na matatizo wanayokumbana nayo huku umri wao ukiwa bado mdogo.

Heavenlight anasema kwamba ifike mahali jamii iwape nafasi wanawake hawa nao ili waweze kufurahia maisha ukizingatia kwamba baadhi yao wanakuwa wameachwa na magonjwa na hivyo kuwaongezea maumivu mara dufu.

Shamsa Mwangunga awapa somo

Aliyewahi kuwa Waziri katika serikali ya awamu ya tatu na ya nne, Shamsa Mwangunga, ambaye naye alihudhuria mkutano huo, anasema kwamba ni marufuku wajane kukata tamaa katika maisha kisa wameondokewa na wenza wao kwa kuwa maisha lazima yaendelee.

Mwangunga ambaye amewahi kuwa waziri wa maliasili na utalii, anafafanua kwamba ni mwaka sasa naye ameonja machungu ya kuwa mjane baada ya kuondokewa na mume wake, hivyo anajua na wanawake wengine wanavyotaabika hususani wale ambao walikuwa mama wa nyumbani, lakini pamoja na yote hayo hawapaswi kutoa nafasi ya kukata tamaa katika maisha yao.

Waziri huyu mstaafu alifika hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya namna wanawake hao watakavyoweza kujishughulisha na biashara kama njia mojawapo ya kupambana na hali ya maisha.

Mmoja wa wajane kutoka nchini DRC Congo, Mwamvita Masumbuko, anasema kwamba mila za kurithi wajane zimekuwa zikiwaathiri wanawake wengi na kutoa wito kwa taasisi mbalimbali na serikali kwa ujumla kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

Mjane kutoka nchini Kenya, Dianah Kamande, amewasihi wajane kuendelea kuungana na kwa viongozi ambao ni wawikilishi wa wananchi kupigania haki za wajane wawapo katika vikao vyao.

Naye Programu Ofisa, kutoka Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Jacline Waya, amesema kwamba wadau wa masuala ya wanawake tayari wameshawasilisha muswada wa sheria ya mirathi wizarani, na tayari wameahidiwa utafikishwa muda wowote kuanzia sasa Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Waya amesema kwamba muswada huo pamoja na mambo mengine, unazungumzia kuzingatia jinsi na wakati wa ugawaji mali kwa familia pindi inapotokea mume amefariki kwani kwa sasa makabila mengi yamekuwa yakiwatenga watoto wa kike na mama zao kwa ujumla.