Wapendekeza wabakaji wahasiwe, wanyongwe

Muktasari:

Vitendo vya kunajisi na kubaka vimekithiri nchini mithili ya moto uliowashwa kwenye msitu wa majani makavu tena ulionyunyiziwa mafuta ya petroli huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto chini ya umri wa miaka 15.

Hata hivyo, ni vigumu kutambua ni watoto wangapi ambao wako mitaani kwa umri huu ambao ni waathirika wa vitendo hivi, lakini kwa upande wa walioko shuleni, wastani wa watoto 50 katika kila shule ya msingi jijini Arusha mathalan wamenajisiwa. 

Ilitarajiwa kuwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa wanaume wanaokutwa na hatia ya makosa ya kunajisi watoto, ubakaji au ulawiti ingeweza kuwa suluhu ya kutokomeza vitendo hivyo katika jamii lakini hali imekuwa kinyume na hivyo.

Vitendo vya kunajisi na kubaka vimekithiri nchini mithili ya moto uliowashwa kwenye msitu wa majani makavu tena ulionyunyiziwa mafuta ya petroli huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto chini ya umri wa miaka 15.

Hata hivyo, ni vigumu kutambua ni watoto wangapi ambao wako mitaani kwa umri huu ambao ni waathirika wa vitendo hivi, lakini kwa upande wa walioko shuleni, wastani wa watoto 50 katika kila shule ya msingi jijini Arusha mathalan wamenajisiwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu, wastani huo ni kwa wale wanafunzi tu ambao walikuwa tayari kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

“Tumetembelea hizi shule za msingi kutoa elimu ya utoaji taarifa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kunajisi watoto ambapo baadhi yao walikiri kufanyiwa vitendo hivyo tena na ndugu zao wa karibu kama baba, kaka mjomba, binamu na wengineo,” alisema na kuongeza:

“Lengo la sisi kuja huku mashuleni ni baada ya kuona taarifa tunazopokea tukikaa maofisini zimechelewa na zimeshamuathiri mtoto kwa kiwango kikubwa kutokana na kutojua umuhimu wa kutoa taarifa au nani wa kumpa taarifa.”

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya kuzungumza na baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali ulibaini kuwa wahusika wakubwa wanaowanajisi watoto chini ya umri wa miaka 15 ni ndugu zao wa karibu.

John (siyo jina halisi) mwenye miaka 11 anayesoma darasa la tatu anasema: “Baba yangu wa kambo (ambaye ni mume wa mama yake mzazi) huwa ananibaka asubuhi kabla sijaenda shule na hutimiza dhamira yake hiyo mara mama anapokwenda sokoni kuuza mboga mboga.”

Mwandishi: Hebu niambie inakuwaje?

John: Mimi huwa naingia darasani saa tano kwa hiyo naondoka nyumbani saa nne, lakini mama yangu huamka alfajiri ya saa 12 kuwahi sokoni na kuniacha na baba ambaye yeye huenda katika kazi zake za ujenzi wa nyumba saa tatu au saa nne asubuhi.

Mwandishi: Enhe, mama akiondoka nini kinatokea?

John: (Anavuta pumzi kidogo huku machozi yakilenga lenga kwenye mboni za macho) baba ananiambia nimsogelee kisha ananivua nguo na kuniingilia kwa nguvu huku akiniziba mdomo hadi anaridhika.

Mwandishi: Alianza lini kukufanyia hivyo?

John: Tangu nikiwa darasa la pili mwaka jana baada ya kugombana na mama na kumfukuza nyumbani.

Mwandishi: Kwanini hukutoa taarifa?

John: (Huku machozi yakimdondoka hadi kulowesha shati lake la shule) Siku ya kwanza nililia sana kwa maumivu niliyokuwa nasikia hadi nilishindwa kwenda shule kwani nilishindwa kutembea, lakini baba aliniambia nikithubutu kumuambia mtu atanichinja anifukie kwenye shimo la taka lililopo nje ya nyumba yetu (analia kwa kwikwi kali), hivyo niliogopa kumuambia mtu.

Hata hivyo, baada ya siku chache nilipona na nikaenda shule, nikachapwa kwanini sikwenda shule wiki nzima, lakini nilivumilia kuchapwa, baada ya wiki chache mama alirudi nyumbani na kutokana na kuchoshwa na hali ile nilitaka kumuambia mama ukweli lakini kila nikitaka kumuambia nakosa nafasi kwani anatoka nyumbani alfajiri na kurudi usiku.

Mwandishi: Ikawaje?

John: Siku hizi haniingilii tena tangu nimeingia darasa la tatu kwani natoka nyumbani asubuhi na mama na kurudi jioni naingia masomo ya jioni na hata kama sijapewa hela nakaa chini ya mti hapo nje ya shule hadi jioni ndiyo narudi nyumbani.

Hiyo ni simulizi ya mtoto anayefanyiwa ukatili na baba yake huku Furaha (siyo jina lake halisi), msichana mwenye umri wa miaka 12 anakiri kutendewa hivyo na kaka yake mkubwa aliyepishana naye miaka minne.

Mwandishi: Nieleze yaliyokusibu

Furaha: (huku akitafuna sweta lake), mimi baada ya mama kufariki na baba kuoa mke mwingine akawa anatunyanyasa, hivyo mimi na kaka yangu tuliamua kuhamia kwa bibi yetu mzaa baba huku Sombetini.

Mwandishi: Ilikuwaje mkafanya ngono

Furaha: Kule kwa bibi yangu tulikuwa tunalala na kaka yangu kitanda kimoja tangu akiwa kidato cha kwanza na mimi niko darasa la nne, hivyo siku moja usiku alianza kunipapasa na kunitaka nifanye naye huku akiniambia atakuwa ananitembelea shule kuniletea pesa za barafu.

Kaka yangu huwa akitoka shule anaenda kuuza maji ya kujengea au kutumia majumbani na kupewa fedha, akawa ananipa Sh200 au Sh300, hivyo nikawa navumilia bila kujua nafanya vibaya, lakini siku moja bibi alitukuta na kutuchapa, tangu siku hiyo nikawa nalala na bibi.

Hao ni baadhi ya watoto wanaokiri kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono, wakiwemo 11 wa shule wa msingi Sombetini wa darasa la tatu waliokamatwa wakifanya mapenzi na mbwa baada ya kufundishwa tabia hiyo na jirani wa mmoja wao hali iliyofikia kufanyiana vitendo hivyo wenyewe kwa wenyewe.

Kamanda Tesha anasema sababu kubwa ya vitendo hivi kukithiiri katika jamii inatokana na baadhi ya watoto kuteswa, kunyanyaswa au kuachwa bila malezi, hivyo hushawishika na kunajisiwa na kulawitiwa.

“Pia wazazi kujikita zaidi katika shughuli za kutafuta uchumi wa kifamilia bila kutenga muda wa malezi kwa watoto wao na huwa hawana nafasi hata ya kuzungumza nao ili kama kuna changamoto wazikabili kwa pamoja.

“Pia wapo wazazi au walezi wanakuwa wakali kwa watoto wao, hivyo kushindwa kupata taarifa za ndani siri za watoto,” anasema Kamanda Tesha na kuongeza:

“Mtoto mwingine anakuambia aliogopa kumuambia mama au baba yake alipofanyiwa kitendo hicho kwa mara ya kwanza kwa kuhofia kupigwa au kusimangwa.”

Anasema baadhi wamekuwa wakitoa taarifa na wahusika kufikishwa polisi au mahakamani, lakini wazazi au walezi hushindwa kutoa ushirikiano. Wako wengine ambao huamua kumalizana na mtuhumiwa kwa kulipwa fidia.

Kuhusu mradi wa kuzungukia shule zote za msingi kutoa elimu, Tesha anasema kuwa katika shule nyingi wamekumbana na changamoto na simulizi za kutisha na kusikitisha hasa kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule zilizoko pembezoni mwa mito.

“Hawa wanafunzi wanaosoma kwenye hizi shule za pembezoni mwa mto wamekuwa wakibakwa na kulawitiwa na wahuni wanaovuta madawa huko, hivyo sisi kama polisi tunaanzisha pia msako wa mateja hao, lakini halmashauri pia zifanye mpango wa kuzijengea hizi shule ukuta ili kuwanusuru hawa watoto,” anasema.

Anasema shule ambazo wanagunzi wanalalamika kufanyiwa vitendo hivyo ni pamoja na Meru, Kaloleni, Makumbusho, Ngarenaro na Mwangaza, lakini wanaogopa kutoa taarifa hizo kwa walimu au wazazi kwa kutishiwa kuuawa.

“Baada ya kuzunguka hizi shule kweli tumegundua taarifa tunazopata ofisini tulikuwa tunaona ni nyingi ambapo kuanzia Januari hadi Oktoba, 2016 tulipata kesi 138 za ubakaji na ulawiti katika mkoa wa Arusha pekee, lakini kumbe ni chache kulinganisha na matukio halisi hivyo kuanzia sasa tutakuwa tunatenga siku za kuwa mtaani pia,” anasema Tesha.

Tatizo ni kubwa kwenye maeneo yanayoongoza kwa uhalifu

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia anasema tatizo la ubakaji na ulawiti limekuwa tishio hasa katika maeneo ambayo yanaongoza kwa uhalifu.

“Kwanza niseme nasikitishwa sana na taarifa hizi ambazo zimekuwa zikinifikia ofisini mara kwa mara, ikiwemo za hawa wanafunzi kufanya ngono na mbwa, lakini maofisa jamii wangu hawajui wala waratibu wa elimu hawana taarifa hizo, hilo ni jambo baya sana.

‘Kutokana na tukio hilo tumewaandikia barua za kuwataka wawe wanatembelea hizi shule mara kwa mara kutokomeza hili kwani vitendo hivi vikiendelea tutakuja kuwa na taifa lisilobebeka kabisa au la vijana wenye mtindio wa ubongo au visasi kutokana na matendo waliyotendewa utotoni.

“Hili suala la shule kujengewa ukuta, wataalamu wa halmashauri watakwenda kufanya tathimini katika hizo shule ambazo baadhi zitajengewa ukuta na zingine zitawekwa uzio wa kawaida wa miti au mbao,” anasema Kihamia.

Mwenyekiti wa Klabu ya Haki za Watoto, Jackson Mutalemwa anasema endapo Serikali isipobadili sheria au kuchukua hatua za makusudi dhidi ya vitendo hivi vya ukatili, ijiandae kuwa na Taifa lililojaa visa na visasi siku za usoni.

“Hivi vitendo wanavyofanyiwa watoto vinauma jamani na kwa sababu hawana pa kusemea basi huhifadhi moyoni ili baadaye kuja kulipiza kisasi au hata kutendea wengine yale waliyotendewa utotoni,” anasema.

Mutalemwa anasema walitarajia adhabu ya kifungo cha miaka 30 ingekuwa suluhu, lakini tatizo badala ya kupungua linaongezeka.

Mutalemwa anasema wanaiomba Serikali kubadilisha sheria na kuweka adhabu kali kwa wabakaji na walawiti kunyongwa hadi kufa au kuhasiwa ili wasiweze kufanya hivyo tena maishani.