Wednesday, November 22, 2017

Wazee, bodaboda waapa kutokomeza mimba za utotoni Tarime

 

By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Changamoto ya mimba na ndoa za utotoni katika Wilaya ya Tarime ni sawa na maeneo mengine nchini, lakini huenda ikawa historia baada ya wazee wa kimila na madereva wa bodaboda kusema sasa inatosha na wapo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali za kupinga vitendo hivyo.

Wilaya ya Tarime ipo ndani ya Mkoa wa Mara ambao ni kati ya mikoa mitano inayoongoza kuwa na tatizo la mimba za utotoni linalokatisha ndoto za watoto wa kike kufikia malengo yao.

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo Jinsia, Watoto na Wazee zinaonyesha Mkoa wa Katavi unaongoza kwa mimba za utotoni kwa asilimia 45 ukifuatiwa Tabora (43), Dodoma (39), Mara (37) na Shinyanga (34).

Kiongozi wa wazee wa kimila wa kabila  la Kikulya kutoka koo 13 za wilaya hiyo, Elias Maganya hivi karibuni  ameeleza msimamo walioufikia kuhusu mimba za utotoni ikiwa ni sehemu kusaidia kampeni ya Serikali, wadau na watetezi wa haki za watoto kuhakikisha tatizo  hilo linakwisha  kwa kuwajengea uelewa wananchi umuhimu wa mtoto wa kike.

Msimamo huo wa wazee wa kimila ulikuja baada ya  Mkuu wa Wilaya  ya Tarime, Glorious Luoga kuwaomba viongozi hao kushirikiana nao katika kutetea haki za mtoto wa kike ikiwamo kupambana na kupinga ndoa za utotoni, mimba na ukeketaji kunakodaiwa kuchangiwa na mila na desturi za wakazi wa wilaya hiyo.

Luoga alitoa ombi hilo wakati wa kongamano la kujadili utoaji wa haki za msingi kwa mtoto wa kike ikiwamo ulinzi wake lililoandaliwa na masharika mbalimbali ya kutetea haki za watoto likiwamo la Plan International na lilihudhuriwa na wazee wa kimila na wanafunzi kutoka shule mbalimbali pamoja na watendaji wa Serikali kutoka Wizara ya Afya na Halmashauri ya Tarime.

 

Serikali inasemaje?

 

Maganya anasema wanaunga mkono juhudi za mtoto katika kufikia malengo yake na hawana shida kushirikiana na Serikali na wadau na watetezi wa watoto.

“Napenda kumhakikishia mkuu wa wilaya na Watanzania kwa ujumla suala la mimba na ndoa za utotoni litakuwa historia katika wilaya hii wazee wa kimila tumeshaamua kuunga mkono juhudu za wadau,” anasema na kuongeza:

“Kama tuliweza kusitisha mapigano ya kikoo huko nyuma hili halitashindika na uzuri wenyewe tunajuana  kupitia koo zetu.”

“Msituone hivi, sisi wenyewe tunatambua  umuhimu wa  mtoto wa kike tunaishukuru sana  Serikali  kwa  kutukutanisha na masharika ya kutetea haki za watoto ambayo yametujengea uwezo wa kutambua thamani na haki za watoto hawa.”

Maganya anasema katika kuhakikisha wanafanikiwa mchakato huo wataanza kufanya mkutano na wazazi kuwaelimisha namna ya haki za mtoto wa kike, pia watawapa mikakati ya kuwadhibiti watoto na kutowaruhusu kwenda sehemu zenye uvunjifu wa maadili.

Kiongozi huyo, anasisitiza kuwa ikitokea kijana au mtu ameoa au kumpa mimba mwanafunzi ataitwa katika mabaraza ya kimila kisha kujadiliwa na kulipa faini ya ng’ombe watakaohitajika kulingana na makubaliano ya baraza.

 “Tumedhamiria  kumaliza tatizo hili na hatutakuwa na mlolongo mrefu kwa atakayebainika kutenda vitendo hivi dhidi ya mtoto wa kike, akibainika hatutasubiri vyombo vya dola  tutaanza naye kisha tutamkabidhi vyombo hivyo kwa hatua za  kimahakama na tutahakikisha anafungwa,” anasema Maganya.

 

Madereva bodaboda

Wakati wazee wakieleza hayo, Umoja wa Madereva wa Bodaboda wa Wilaya ya Tarime Mjini (Uwamitamo), umesema wakati umekwisha kwa wanachama wao kunyooshewa vidole dhidi ya uhalifu kwa watoto wa kike na atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu  ikiwamo  kufukuzwa na kutozwa faini ya papo papo.

Madereva wa bodaboda  wa Tarime wanadaiwa kufanya uhalifu kwa watoto wa kike  kwa kuwapa ujauzito kutumia mbinu ya kuwapa lifti wakati wa kwenda na kurudi shule pia wanawarubuni hata wale wasiobahatika kwenda shule.

Lakini katika kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau katika kupiga vita dhidi ya ndoa na mimba za utotoni umoja huo kupitia vijiwe vya maegesho wamejiwekea mikakati thabiti ya kuhakikisha haki ya mtoto wa kike inalindwa.

Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu wa kituo cha  pikipiki cha Juminta, Steve Nashon, wilayani Tarime  anasema katika kuhakikisha wanawadhitibiti  madereva wenye vitendo vya utovu wa nidhamu kwa mtoto wa kike kituo chao kimeweka  faini ya Sh5,000 papo hapo kwa dereva atakayebainika kumshikashika mtoto wa kike.

Anasema watahakikisha faini hiyo inatekelezwa kwa ufanisi  ili iwe fundisho kwa madereva wenye tabia ya kuwashikashika watoto wa kike ambao baadhi yao ni rahisi kurubuniwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kipato kidogo  cha fedha.

“Kijiweni wananiogopa ndiyo maana wakaamua kunipa cheo hiki na sina haya na tutahakisha jambo hili linafanikiwa ingawa nitajenga chuki na madereva wengine kutokana na msimamo wangu kwa mtoto wa kike na tunatoa onyo kwa madereva bodaboda kubadilika,” anasema Nashon.

Wakati Nashon akieleza hayo, mjumbe mkuu wa Umitamo, Kulwa Joseph anasema  kwa kipindi kirefu wamekuwa madereva wa bodaboda wa wilaya hiyo wakionyoshewa vidole  dhidi ya vitendo vya kihalifu  kwa mtoto wa kike kwa kuwarubuni na kusababisha ndoto zao kutokamilika.

“Tunanyooshewa vidole na jamii ya Wanatarime kwa sababu sisi ndiyo tupo karibu nao kutokana na shughuli zetu zinatufanya kufika sehemu yoyote na huwa tunawapakiza wakituomba msaada wa usafiri. Lakini madereva wasiowaaminifu wanatumia mwaya huo wa msaada kufanya uhalifu dhidi ya watoto hawa ambao kwa kiasi kikubwa watakuwa na mchango mkubwa kwa siku za baadaye,” anasema Joseph.

Joseph anasema mwanachama akibainika anapewa onyo kwanza kisha wanatafuta ushahidi kuhusu uhalali wa kosa alilotenda na ukipatikana anaondolewa eneo hilo ili iwe fundisho kwa wanachama wengine.

Amesisistiza kuwa umoja huo umejipanga kisawasawa katika kuhakikisha wanatetea haki za watoto hao na kwamba hawatakubali kuwa sehemu ya watuhumiwa wa kukatisha ndoto za watoto hao.

“Tayari kuna wanachama watatu walishakumbana na adhabu hii. Sasa tunawatangazia kiama wale wenye mchezo huu kuacha mara moja kama wanataka kuendelea kuishi Tarime mjini,” anasema Joseph.

 

Serikali inasemaje?

Katika kuhakikisha  haki ya mtoto wa kike inaendelea kulindwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jinsia na Watoto na Wazee,  Ummy Mwalimu anatoa miezi sita kwa  shule za msingi na sekondari kuanzisha madawati  ya ulinzi na usalama ili kuzuia mimba za utotoni.

Ametoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika kitaifa uwanja wa TCC wilayani Tarime yaliyokuwa na kaulimbiu ya ‘Tokomeza Mimba za Utotoni Tufikie Uchumi wa Viwanda’.

Mwalimu anasema bado ana imani ndani ya miezi hiyo mchakato huo utakamilika kwa kiasi ili kuwaokoa watoto wa kike waliopo kwenye hatari mbalimbali  kuondokana na mimba za utotoni na hatimaye kuendelea na masomo na ili kutimiza ndoto zao.

“Mimba za utotoni bado ni tatizo katika mikoa mbalimbali. Madawati haya yatasaidia kufanikisha kuzuia kwa kuwa yatapokea matatizo yanayowakabili hasa kutoka kwa wazazi na mazingira yanayowazunguka kisha kufanyiwa kazi,” alisema Mwalimu.

Serikali imeadhimisha siku hiyo kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali zaidi ya 10 yanayotetea haki za watoto ikiwamo Umoja wa Ulaya kupitia taasisi za Plan International, Save the Children na Unicef.

 

Kauli ya wanafunzi  

Rehema Amos mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Nyamisangura anasema baadhi ya watoto wa kike wameingia  kwenye matatizo kutokana na wazazi wao kutowasikiliza hasa mahitaji yao jambo linalosababisha kudanganyika.

Mwakilishi wa shirika la Unicef nchini, Maniza Zaman ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha siku hiyo kwa kutumia kaulimbiu ya ‘Tokomeza mimba za utotoni tufikie uchumi wa viwanda’. 

“Napenda kusisitiza umuhimu wa mtoto wa kike katika kuifanya Tanzania iwe nchi imara na yenye maendeleo ya kiuchumi. Umri wa kubarehe ni kipindi muhimu cha kuelekea katika utu uzima. Watoto wa kike wakiandaliwa na kuweza kuvuka kipindi hiki kwa usalama, wana fursa ya kuja kuwa wananchi watakaochangia maendeleo ya jamii na taifa,” anasema Zamani.

Zamani anasema binti mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wana watoto na kwamba Tanzania ni moja kati ya nchi yenye kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni.

Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Taasisi ya Plan International, Martha Lazaro anasema shirika hilo linatambua ndoa za utotoni, mimba na ajira hatarishi ni vikwazo kwa mtoto katika kutimizi ndoto zake ndiyo maana limeamua kuungana na Serikali katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki yake.

“Mikakati yetu ni kuhakikisha mtoto wa kike anatambulika, ikiwamo kushiriki kikamilifu katika kufanya uamuzi sahihi kwake.Mtoto wa kike asipopata nafasi ya kufanya uamuzi hawezi kutimiza ndoto zake.

“Pia, Plan imejiwekea mkakati wa kumjengea uwezo mtoto wa kike ya kuweza kujitambua, kujiamini na kujua ni wapi anaweza kupata haki za msingi,” anasema Lazaro.

-->