Wilbard; mwanafunzi mwenye ulemavu anayeishi mazingira hatarishi

Thursday December 7 2017

Wilbard Marwa akirudi nyumbani kutoka katika

Wilbard Marwa akirudi nyumbani kutoka katika Shule ya Msingi Erienyi wilayani Rorya, Mkoa wa Mara. Picha na Anthony Mayunga 

By Anthony Mayunga, Mwananchi

       Kilometa 55 kutoka Musoma Mjini nafika Shule ya Msingi Erienyi katika Kijiji cha Erienyi, Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara, nawakuta baadhi ya wanafunzi wakiwa madarasani na wengine wakiwa nje.

Chini ya mti kuna walimu wakiendelea na kazi ya kusahihisha madaftari ya wanafunzi, unaweza kusema wanapunga upepo, ukweli ni kwamba wana uhaba wa ofisi katika shule hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1958 kabla ya uhuru.

Ndani ya darasa la tatu watoto wamejaa, naambiwa na mwalimu kuwa watoto 153 wanatumia chumba kimoja, miongoni mwao yumo Wilbard Marwa (15), ambaye ni mlemavu wa miguu mwenye ndoto ya kusoma na kuwa kiongozi hasa ngazi ya kata, lakini kwa hali ya ulemavu wake na wingi wa watoto mpaka sasa hajajua kusoma.

Mahudhurio yake shuleni hutegemea kubebwa kwa baiskeli na binamu yake, inapoharibika au asipokwenda shule naye anabaki nyumbani. Anapokosa usafiri wa kurudi kwao walimu hulazimika kutafuta namna ya kumrudisha nyumbani kilometa zaidi ya mbili kutoka shuleni.

“Natamani kuwa mtendaji wa kata, kama nitafanikiwa kusoma na kufaulu, ili nami siku moja niweze kuhudumia wananchi … kama nitabaki shule hii sitaweza kufaulu kutokana na mazingira ninayoishi, usafiri na shule si rafiki,” anasema kwa upole.

Marwa anasema alicheleweshwa kuandikishwa shule kutokana na ulemavu wake na hali duni ya mama yake, vinginevyo angetafutiwa shule ya watoto wenye matatizo kama yake.

“Maisha ya nyumbani ni magumu sana, hakuna mtu wa kunisaidia ili nisome kwa kuwa mama yangu kazi yake ni kuuza pombe, darasani mko wengi hivi, dawati moja mnakaa watano hadi sita, kiti ninachokalia siwezi kukanyaga chini unakuwa umening’inia, utasomaje?” anahoji.

Anachangia choo na wenzake

Anasema kuwa miundo mbinu ya shule si rafiki hivyo anachangia choo na wenzake.

“Mimi natembelea magoti na mikono, naingia chooni humo hivyo, wanajisaidia ovyo ovyo…nyumbani nako najisaidia vichakani, ili nifikie ndoto yangu lazima nipate msaada,” anasema.

Anasema wakati wa mvua anapata shida zaidi kutembea kwenye tope na kama angepata baiskeli ya magurudumu matatu kwake ungekuwa msaada mkubwa katika maisha yake.

Anakiri ulemavu wake umechangia migogoro ndani ya ndoa ambayo imemfanya baba yake kumtelekeza bila huduma.

Binamu anena

Justine Mapambano (13) mwanafunzi wa darasa la tatu ambaye pia ni binamu wa Wilbard anasema: “Kusoma kwake kunanitegemea mimi, kama kuna tatizo ambalo linanifanya nisiende shule ama kutokuwa na baiskeli naye hukaa tu nyumbani.”

Anasema historia ya maisha yao inafanana kwa kuwa mama yao aliwakimbia na kuwaacha yeye na mdogo wake wanaishi na baba yao na Marwa baba yake alimtelekeza anaishi na mama yake.

Hata hivyo, anakiri kuwa uwezo wa Wilbard darasani ni mdogo kiasi kwamba anakuwa katika nafasi za mwisho.

Mazingira ya nyumbani na shuleni yanachangia matokeo mabaya, kama kuna watu wanasaidia wenye matatizo kama yake wamsaidie asome anapenda shule,” anadai.

Walimu wakiri mazingira ni mabaya

Mwalimu wa darasa, Rehema Mwerinde anasema Marwa anatakiwa kuwa kwenye shule maalum kwasababu darasa lao kuna watoto zaidi ya 150, wanakaa watano hadi sita dawati moja na wengine chini, kwahiyo inakuwa vigumu mwalimu kufuatia maendeleo ya mwanafunzi mmoja mmoja darasani.

Mkuu wa shule msaidizi, Lucas Naamani anasema pamoja na ukongwe wa shule lakini mazingira ni magumu hata kwa watoto wasiokuwa na ulemavu, kwa Marwa hali ni mbaya zaidi.

Mwenyekiti aomba msaada

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Erienyi, Chacha Wakibara anakiri kuwa kutokana na mitizamo ya jamii si rahisi kumsaidia mwanafunzi huyo badala yake anawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kumsaidia.

“Maisha ya mama yake ni magumu anauza pombe za kienyeji, huyu mtoto anapaswa kusaidiwa na jamii, lakini hakuna aliye tayari ndiyo maana tunaomba wadau mbalimbali watusaidie,” anasema.

Shuleni ni taabu na nyumbani ni shida ndivyo unaweza kusema, kwa kuwa Marwa akitoka shuleni hufikia katika klabu cha pombe mbalimbali ikiwemo gongo, biashara anayoendesha mama yake.

Mama mzazi alonga

Mwananchi lilipofika nyumbani kwa Monica Mtete (35) mama mzazi wa Wilbard lilikutana na baadhi ya wateja wake wakiwa wamelewa na mtoto akikatiza katikati yao huku mama yake akimwangalia tu.

Hata hivyo, katika hali ya kukata tamaa, anasema huyo ni mtoto wake wa kwanza kati ya saba aliozaa, lakini waliohai ni watatu.

“Walizaliwa kwa shida sana, nimekaa Hospitali ya Musoma kwa siku tatu hanyonyi, nimehangaika sana,”anasema.

Anasema hata baada ya kufikisha umri wa kukaa haikuwa rahisi mpaka akawa anachimba shimo na kumkalisha ndani yake. Alichelewa kuandikishwa kuanza masomo kwa miaka mitatu.

“Mwaka 2008 niliachana na mume wangu baada ya kuonekana kama huyu mtoto ni balaa, mzigo kwake…akanikata na panga nikaamua kurudi kwetu, akadai nikachukue mtoto wangu ni mzigo kwake,” anasema kwa masikitiko.

Anasema mume wake alilazimika kurudisha mahari kwao ng’ombe watatu na hajawahi kutoa matumizi kwa mtoto wala kufuatilia maendeleo yake kwa kipindi chote, anasema hana uwezo zaidi ya kumwachia Mungu.

“Hapa hatuna choo kizuri analazimika kwenda kujisaidia kwenye nyasi, maana akiingia choo tunachotumia anaweza kutumbukia…analazimika kukaa hapa kilabuni ili nikipika ale ndipo akalale, nitafanyaje mimi hata Tasaf niliandikishwa lakini sijawahi kupata fedha kwa ajili ya mtoto huyu,” analalama.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Serikali ya kijiji anakiri kuwa aliandikishwa Tasaf awamu ya tatu, ingawa hakuwa tayari kusema kama ni mmoja wanufaika.

Wilbard Marwa (kushoto) akiwa na binamu yake

Wilbard Marwa (kushoto) akiwa na binamu yake Justine Mapambano, ambaye humsaidia kumpeleka shuleni na kumrudisha kwa baiskeli. Wote ni wanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Erienyi iliyoko wilayani Rorya, Mkoa wa Mara. Picha na Anthony Mayunga

Baiskeli

Mkurugenzi wa kituo cha Lake Victoria Disability Centre Musoma, Dennis Maina anasema gharama ya baiskeli ya magurudumu matatu kwa ajili ya mtoto ni Sh450,000 nje ya usafiri.

Jipe moyo

Mshauri nasaha wa Kituo cha Jipe Moyo, Yuster Richard anasema kupitia vikundi vya mpango wa kusaidia watoto wanaojihusisha na ngono utotoni na mazingira magumu wilayani Rorya ndio walioibua taarifa za mtoto huyo.

“Mara ya kwanza tulimkuta na hali mbaya sana, nguo zimechanika, tukampa nguo, viatu vya mkononi ili kumkinga na maradhi mbalimbali, nyumbani kwao analala chini, kwa kweli wadau wanatakiwa kumsaidia ili aweze kufikia ndoto zake,” anasema.

Hitaji la Sheria

Sheria namba 9 ya Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2010 ambayo inatoa wajibu kwa Serikali, wabunge, Mahakama, wizara mbalimbali na wakala wa Serikali, idara za Serikali, mashirika ya umma, Serikali za mitaa, asasi za kiraia na jamii inahimiza utendaji haki.

Miongoni mwa haki zilizobainishwa ni elimu na mafunzo, haki ya kupata huduma zote zinazotolewa na taasisi za umma bila ubaguzi na inatoa wajibu kwa taasisi za elimu kuwa na majengo yanayokidhi matakwa ya kufundishia kundi hilo.

Irienyi ni shule kongwe mkoani Mara, ina wanafunzi 1040, lakini ina vyumba vinane vya madarasa hali inayosababisha watoto kukaa zaidi ya 150 chumba kimoja, mwalimu mmoja anafundisha watoto 150 ambao ni sawa na madarasa manne.

Ina walimu 16 mahitaji yakiwa ni 23, ina nyumba vitano vya walimu kati ya 23, nyumba moja yenye vyumba vitatu wanaishi walimu watatu licha ya kuwa na familia.

“Juu ziko wazi, tulipoomba wazazi wazibe juu, wakasema tunatakiwa kununua redio kubwa za muziki, ili ukifungulia huwezi kusikia chumba cha pili hatuna faragha,” anasema mmoja wa walimu.

Mwaka jana wanafunzi waliohitimu darasa la saba walikuwa 153, kati yao waliofaulu ni 40 wote kwa daraja la tatu.

Kwa watakaoguswa na kutaka kumsaidia Wilbard Marwa wawasiliane na mama yake mzazi kwa namba 0785762392.     

Advertisement