‘Mila potofu zisikwamishe tiba ya vichanga’

Naibu Mkurugenzi wa Halotel Trieu Thanh Binh na wafanyakazi wenzake wakikabidhi msaada kwa wauguzi wanaohudumia watoto wenye magonjwa ya vichwa vilivyojaa mani na mgongo wazi waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) hivi karibuni. PICHA | MAKTABA

Muktasari:

Watoto wengi hukosa tiba kutokana na wazazi ama walezi kukosa uelewa wa kile kinachosababisha magonjwa haya ya mgongo wazi na vichwa vikubwa. Hali hiyo inaonyesha umuhimu wa mashirika kama Halotel kufanya jitihada za kuwasaidia watoto wenye magonjwa haya.


Dar es Salaam. Jamii ya Kitanzania inaaswa kutoruhusu mila potofu zizuie utoaji tiba kwa watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali ya kiafya, hasa tatizo la kichwa kujaa maji ama mtoto kuzaliwa “mgongo wazi.”

Katika mazungumzo na wanahabari hivi karibuni, Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Taasisi ya Tiba ya  Mifupa Muhimbili (MOI), Laurent Mchome alieleza kuwa watoto wengi hukosa tiba kutokana na wazazi ama walezi kukosa uelewa wa kile kinachosababisha magonjwa haya.

“Changamoto kubwa ni kwamba jamii ya Watanzania haina elimu ya kutosha kuhusu magonjwa haya” alisema Dr. Mchome katika risala yake mara baada ya kutembelewa na wafanyakazi wa kampuni ya simu ya Halotel waliopeleka misaada kwa watoto walioathirika na hali hii pamoja na wazazi wao waliolazwa MOI.

Jamii, anasisitiza Dr. Mchome, haifahamu kuwa “magonjwa haya hutibiwa na watoto hupona kabisa.”

Tafiti zinaonyesha kwamba mara nyingi vichwa kujaa maji na tatizo la mgongo wazi huathiri hasa watoto wachanga wakati wanapozaliwa, na watoto walio na chini ya umri wa miaka mitano.

Jitihada mbalimbali za serikali na taasisi za kijamii kupunguza ama kutokomeza kabisa changamoto hizi nchini Tanzania hujikuta zikikwama kutokana na mila na mitazamo potofu inayosababisha, kwa mfano, baadhi ya jamii kuwaficha watoto wenye shida hizi.

Elimu kwa umma na utoaji wa huduma ndani ya jamii husika ni kati ya jitihada zinazofanyika kubadili mitazamo hiyo. “Tumekuwa tukiweka kambi ya kutibu watoto kila mkoa na kila kanda nchini,” alisema Dr. Mchome.

Kila mwaka, MOI hutibu wagonjwa zaidi ya 350 nchi nzima kupitia kampeni hiyo ya watoto wenye vichwa vilivyojaa maji na mgongo wazi, alieleza Dr. Mchome katika risala yake.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada, Naibu Mkurugenzi wa Halotel, Trieu Thanh Binh alieleza kuwa kampuni yake imejumuika na watoto hao kama sehemu ya jitihada zake za kuinua sekta ya afya nchini Tanzania.

“Msaada huu ni mwendelezo wa kampeni yetu ya kuisaidia jamii yenye uhitaji ili (watoto hawa) waweze kuimarika kiafya wanapoendelea kupata matibabu” alisema Bwana Binh. “Hii ni pamoja na kuonyesha upendo kwao na kuitambua thamani yao katika jamii ya Watanzania.”

Katika mazungumzo yake, Mkurugenzi huyo wa Halotel ametoa pia wito kwa mashirika mengine kuunga mkono jitihada za kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya mgongo wazi na vichwa vilivyojaa maji.

PR disclaimer: Taarifa hii imeandaliwa kwa kushirikiana na Kitengo cha Mawasiliano cha Halotel.