Mbwembwe za kumnyang’anya Sumaye shamba hazijengi

Fredrick Sumaye

Fredrick Sumaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyehudumia nchi kupitia cheo hicho kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine yeyote.

Waziri Mkuu aliyepo ofisini kwa sasa, Kassim Majaliwa ili afikie rekodi ya Sumaye, anapaswa kuomba mambo mawili; kwanza Rais John Magufuli aongoze nchi kwa mihula miwili, pili katika muda wake wote huo ambakishe ofisini kwenye nafasi hiyo.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu pekee katika miaka 10 ya Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa. Aliingia bungeni katika Serikali ya Awamu ya Kwanza akiwa Mbunge wa Hanang, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimfanya kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika kisha Waziri wa Kilimo na Ushirika.

Ufafanuzi huo unaonyesha kuwa Sumaye ameihudumia nchi hii. Siasa ziwekwe kando kisha tuzungumze ukweli, hakuna mtu ambaye anaweza kufuta utumishi wa Sumaye miaka 22 akiwa mbunge, miaka 10 Waziri na Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika kisha miaka 10 Waziri Mkuu.

Sumaye alichaguliwa kuwa Mbunge wa Hanang mwaka 1983 na alitangaza kustaafu mwaka 2005 (miaka 22), aliteuliwa na Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo mwaka 1985 na kudumu miaka tisa mpaka mwaka 1994, alipoteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Ushirika, nafasi ambayo aliishikilia kwa mwaka mmoja.

Kuanzia mwaka 1995 mpaka 2005, Sumaye alikuwa Waziri Mkuu. Nani anaweza kuwaza Sumaye alijitoa mangapi kwa ajili ya nchi hii alipokuwa anashikilia nafasi hizo za uongozi hususan Uwaziri Mkuu?

Fikiria mtu amekuwa mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za Serikali kwa miaka 10. Mauaji yakitokea mahali ni yeye, mafuriko ni yake, mapigano yanamhusu, ukame na baa la njaa ni vyake, shida na changamoto mbalimbali za wananchi kidole kinanyooshwa kwake. Unaweza kutafakari mtu huyo alikosa usingizi mara ngapi kwa ajili ya kuwahudumia watu wa nchi yake.

Usifikirie uwaziri mkuu katika ile maana ya ukuu au kuula, mfikirie Waziri Mkuu kwa maana ya mtoa huduma. Utendaji wa kila wizara unamhusu. Inabidi afanye kazi na kila wizara kuhakikisha bajeti zake zinapitishwa na Bunge.

Waza sasa kibinadamu jinsi ambavyo Sumaye anaweza kuwa anaumia pale mbwembwe zinapoonyeshwa kumnyang’anya shamba lake kwa maelezo kuwa ameshindwa kuliendeleza.

Suala la kumnyang’anya shamba ni moja na mbwembwe ambazo zimeonyeshwa ni jambo lingine. Tunaweza kukubaliana kuwa ni sahihi kwa mujibu wa sheria kumnyang’anya Sumaye shamba lake la ekari 33 lililopo Mabwepande, lakini mbwembwe zina faida gani?

Kwa nini uamuzi wa kumnyang’anya Sumaye shamba uendane na maonyesho ambayo moja kwa moja yanakuwa yanamdhalilisha? Je, ilishindikana kweli kutumia uungwana mdogo kulichukua shamba kidiplomasia, yaani kumshirikisha mwenyewe Sumaye na akaridhia?

Ukitazama mbwembwe nyingi ambazo zimetumika, tafsiri yake ni kuwa hana nguvu na kwamba wenye nguvu wameamua. Na hapo ndipo kwenye ukakasi. Watu wanasahau mapema mno kuwa mtu huyo alikuwa Waziri Mkuu na aliachia madaraka miaka 11 tu iliyopita.

 

INAENDELEA UK 24

 

INATOKA UK 23

Ieleweke dunia haisimami

Ukiwa kiongozi kwa nafasi yako unapaswa kutambua kuwa dunia haisimami. Inazunguka, upo wakati utajikuta upo nje. Je, nawe utajisikiaje muda huo watu kukutenda kama vile hujawahi kutoa mchango wowote katika nchi?

Mathalan, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza mara nyingi aombewe kwa sababu anakabiliana na uozo mkubwa serikalini. Tunakubaliana naye kuwa hali ni mbaya na watu kweli wanaiba. Sauti yake inaakisi hisia zake kwamba anajitoa kwa ajili ya Tanzania yake anayoipenda.

Siku Dk Magufuli akiwa nje ya ulingo akatokea kiongozi mwingine akaamua kumsumbua pasipo kuthamini kazi kubwa aliyojitolea kuifanya katika nchi hii, je, hali hiyo ikitokea atajisikiaje? Bila shaka ataumia na itamuumiza zaidi kuona kuwa alifanya mengi kwa ajili ya nchi yake lakini hayathaminiki.

Hisia hizo hizo za kibinadamu anazo pia Sumaye. Kipindi hiki ambacho amegeuzwa kituko kwa shamba la Mabwepande, ndani ya moyo wake anawaza huduma ambazo alizitoa kwa nchi hii, lakini leo anachukuliwa utadhani hana chochote alichochangia kwa taifa lake. Shamba tu la ekari 33.

Swali moja tu, je, Sumaye angekuwa bado yupo CCM angefanyiwa alichofanyiwa? Kuhama vyama vya siasa ndiyo mwanzo wa kukomoana? Nani anajihakikishia kuwa maisha yake baadaye yatakuwa salama bila kuguswa?

Dunia haisimami; Rais Magufuli ambaye alifanya uamuzi wa kisheria kumnyang’anya Sumaye shamba, alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kisha Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Awamu ya Tatu ambayo Sumaye alikuwa Waziri Mkuu.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alikuwa Naibu Waziri wa Kazi na Vijana kisha Mnadhimu wa Bunge kwa maana ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, katika Serikali ya Rais Mkapa ambayo Sumaye ndiye alikuwa Waziri Mkuu.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ambaye ndiye alitoa tamko husika, kwa umri wake alikuwa darasani wakati Sumaye akihudumia nchi hii kama Waziri Mkuu.

Ufafanuzi kuhusu Rais Magufuli, Lukuvi na Hapi dhidi ya Sumaye ni kuonyesha kuwa dunia haisimami. Inasonga mbele tena kwa kasi kubwa.

Nafasi uliyonayo leo unaweza usiwe nayo kesho au ukawa juu zaidi. Hakuna mwenye kuijua kesho zaidi ya Mungu.

Hata Sumaye mwenyewe nyakati zake akiwa Waziri Mkuu, pengine hakuwaza kama utafika wakati atakuwa chama pinzani, kisha watu ambao walikuwa chini yake, yaani Rais Magufuli na Lukuvi wanaweza kugeuka mwiba kwake.

Bila shaka Sumaye hakuwaza kama kijana aliyekuwa darasani yeye akiwa Waziri Mkuu, tena akipambana kurahisisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wa Tanzania, anaweza kuwa mtoa tamko la yeye kunyang’anywa shamba bila staha japo kidogo.

 

Wastaafu wapewe heshima

Rais Mkapa akiwa kwenye mkutano mmoja wa kimataifa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, uliofanyika Mlimani City, Dar es Salaam, aliwahi kuzungumza maneno yaliyoacha maswali mengi kwamba kuna mambo alikuwa hawezi kuyasema kwa sababu bado anapenda kuishi.

Swali likawa Mkapa alikuwa anasakamwa na nani mpaka anatoa maneno hayo? Mtu huyo ambaye alizungumza hayo ndiye kwa miaka 10 kati ya mwaka 1995 mpaka 2005, alikuwa raia mwenye nguvu na anayelindwa kuliko yeyote Tanzania.

Miaka hiyo 10, alikuwa ndiye raia mtoa uamuzi wenye nguvu kuliko yeyote. Sauti yake ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa nchi. Saini yake ilikuwa ikiheshimiwa kuliko ya mwingine yeyote. Hata hivyo, miaka michache tu baada ya kuondoka madarakani alitamka kuwa yapo lakini anaogopa kuyasema kwa maana anapenda kuishi.

Kauli ya Rais Mkapa ni kuonyesha kuwa dunia haisimami, inazunguka kwa kasi kubwa. Unapopata nafasi ya uongozi halafu ukashindwa kung’amua mzunguko wa dunia, utajikuta unafanya vitu ambavyo baadaye unaweza kuvilipia gharama itakayokuumiza.

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alipokuwa anakabidhi mamlaka ya uenyekiti wa CCM kwa Dk Magufuli, Julai mwaka huu, aliwakumbusha watu kutendeana mema kwa sababu dunia inazunguka.

Kikwete alijitolea mfano kuwa alipata kuwa msaidizi wa mzee Pius Msekwa, wakati huo Msekwa akiwa Katibu Mtendaji wa CCM, cheo ambacho kwa sasa kinafahamika kama Katibu Mkuu. Baadaye Kikwete alikuja kuwa Rais na Mwenyekiti wa CCM halafu Msekwa akawa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.

Wastaafu wasinangwe kama vile hawatambuliki. Ilitokea hivyo hata kwa Waziri Mkuu wa kwanza katika Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa kuhusu tamko la kunyang’anywa shamba Monduli, Arusha. Tamko hilo lilitolewa na Lukuvi bungeni wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu.

Hata kama uamuzi unafanyika kisheria ipo namna ya kulinda heshima ya watu ambao wana yao mengi mazuri waliyafanya kwa ajili ya nchi hii. Tofauti za kisiasa zisisababishe wastaafu wanangwe bila heshima.

Kama nchi, viongozi lazima wawe na utaratibu wa kuheshimiana na kustahiana. Sumaye na Lowassa wakinangwa leo, ipo siku JK na Magufuli kwa wakati wao wanaweza kushushuliwa bila staha. Huo siyo utu, siyo Utanzania ambao tunatakiwa kuujenga na kuuenzi.

 

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya mtandao www.luqmanmaloto.com