Jeshi la Zimamoto lawataka wamiliki magari ya abiria kuondoa mabomba dirishani

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Mkoa wa Ilala,Elisa Mugisha

Muktasari:

Zimamoto limewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuondoa mabomba kwenye madirisha ili kuwasaidia abiria kutoka nje pindi inapotokea ajali au moto.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji limewataka wenye vyombo vya usafiri kuyaondoa mabomba waliyoweka kwenye madirisha ya magari ya abiria kwani iwapo ajali itatokea  madirisha hayo yanatumika kama mlango wa dharura.

Akizungumza leo Septemba 14, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Mkoa wa Ilala,Elisa Mugisha alipokuwa kwenye kampeni ya ukaguzi ya kujikinga na tahadhari za moto kwenye vyombo vya usafiri.

Amesema tatizo hilo  ni kubwa na wamebaini wenye vyombo vya usafiri hasa kwenye magari ya abiria wamekuwa wakiweka mabomba hayo  kwenye madirisha.

Mugisha amesema mabomba hayo yanapowekwa kwenye madirisha ya magari ya abiria watu wanashindwa kutoka mfano  moto umetokea au gari limedondoka  upande wa mlango  hawataweza  kutoka nje matokeo yake wataendelea kuteketea.

“Kama utaweka mabomba kwenye madirisha je watatokaje wakati mlango umelaliwa na waokoaji watashindwa kuokoa watu hata wakiyakata yatawaumiza watu,”amesema Mugisha.

Pia amesema katika ukaguzi huo wataangalia mfumo wa umeme wa gari,betri lilivyowekwa kama haliwezi kusababisha cheche na kuleta moto na uvujaji wa mafuta kama ni dizeli au petrol inamwagika hivyo ikatokea cheche inaweza kusababisha moto.

Amesema zoezi hilo ni endelevu hivyo anawakumbusha wanaotumia vyombo vya moto kuweka tahadhali za moto kwenye magari yao pamoja na majanga mbalimbali.

Mugisha amewataka wamiliki wa magari wayapeleke ili yakakaguliwe na wametakiwa wawe na kifaa cha zimamoto ambapo wakaguzi watawaelekeza awe na cha aina gani na ukubwa upi.

Amesema wenye vyombo vya moto hasa wenye magari wametakiwa  kupeleka fomu ambayo itawasaidia  wakaguzi wa zimamoto kwenda eneo husika ili kuyakagua bure.