Mauaji Mtwara

Wakazi wa mji mdogo wa Dumila Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro  wakiwakimbia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)  katika barabara ya Dodoma-Morogoro juzi. Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

SABA WAUAWA KATIKA VURUGU MASASI,NYUMBA YA ANNA ABDALLA,MARIAM KASEMBE ZACHOMWA MOTO,MMOJA AUAWA ULANGA

WATU wanane wameuawa na wengine kumi na moja kujeruhiwa kutokana na vurugu zilizizotokea jana mkoani Mtwara na Itete wilayani Ulanga, mkoani Mororgoro.

Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Masasi, Mkomaindo, Amima Simbo alithibitisha vifo vya watu saba waliofikishwa hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo, maiti zilizopokelewa hospitalini hapo zilionekana zikiwa na matundu yanayodhaniwa kuwa ni ya risasi, baadhi yao kichwani, begani, viunoni na tumboni.
Aidha majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo pia walikuwa na majeraha mbalimbali ikiwamo ya risari.

Habari zaidi zinaeleza kuwa vurugu hizo zilizuka baada ya kundi la waandamaji, wengi wakiwa vijana waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda waliokuwa wakipinga mwenzao kukamatwa na kutaka kuvamia Kituo cha Polisi ili kumwokoa.

Vurugu hizo ziliendelea kuutikisa Mkoa wa Mtwara kwa siku ya pili mfululizo na kuutikisa Mkoa wa Mtwara, baada ya vurugu nyingine kuibuka wilayani Masasi jana.

Habari zinasema mbali na vifo na majeruhi, nyumba za wabunge wawili wa wilaya hiyo zimechomwa moto, ambapo pia magari, trekta, Ofisi za CCM Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.

Wabunge ambao nyumba zao zimemwa moto ni Mariam Kasembe wa Masasi Mjini na Anna Abdallah Mbunge wa Viti Maalumu wilayani humo.

Juzi vurugu hizo zilitokea katika Mikoa ya Morogoro kati ya wakulima na wafugaji na kusababisha kifo cha mtu mmoja wakati mkoani Mtwara wananchi  wa eneo la Chikongola waliizingira nyumba ya diwani wa Kata ya Mikindani, Mohamedi Chehako kwa madai ya kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.

Katika vurugu hizo polisi walilazimika kutumia silaha yakiwamo mabomu ya machozi ili kupoza hali ya hewa, ambapo nyumba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia ilichomwa moto.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kuhusu vurugu hizo, Mbunge wa Masasi Mjini, Mariam Kasembe alisema kuwa nyumba yake iliyoko Masasi mjini imechomwa moto na kuteketea kabisa, huku mali zikiibwa na kwamba familia yake sasa haina makazi.

Aliongeza kwamba mbali na uharibifu, vurugu hizo zimesababisha pia mama yake mzazi kukimbia na mpaka sasa hajulikani alipo.

“Wamechoma trekta na gari lililokuwepo nyumbani kwangu, watoto wangu na mume wangu walipoona hali hiyo wakakimbia,” alisema Kasembe akieleza kuwa hawezi kuthibitisha chanzo cha vurugu hizo, lakini anahisi kuwa zinatokana na mgogoro wa gesi.

Alifafanua kwamba watu hao walifanya uharibifu huo baada ya kupanga njama huku wengine wakiwa wamekizingira Kituo cha Polisi, ili kuwazuia wasiende kuisaidia familia yake.

“Ofisi ya Bunge ilitaka kunisafirisha ili nikaangalie hali ilivyo, lakini wapigakura wangu na ndugu wameniambia nisiende ili kulinda usalama wangu,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdalla alisema nyumba yake iliyopo eneo la Masasi mjini imechomwa moto katika vurugu zilizotokea jana.

“Ni kweli nyumba yangu nimesikia imechomwa moto, lakini sijui kinachoendelea,” alisema.
Mkazi wa Kijiji cha Chikunja, alipozaliwa Kasembe, Anna Martin aliliambia gazeti hili kuwa kundi jingine la vijana lipo katika harakati za kutaka kuichoma nyumba ya mbunge huyo, hali iliyosababisha wanafamilia wa mbunge huyo kutoka nje.

Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Idi Mkwachu, ambaye ni Mkandarasi wa Wilaya hiyo alisema kuwa vurugu hizo zilianza saa mbili asubuhi jana, ambapo kundi la watu lililokuwa likizunguka mitaani lilikuwa  likiimba nyimbo za kuitaka Serikali ilipatie ufumbuzi suala la gesi.

Mkwachu alisema kuwa suala la gesi limezua uadui mkubwa kati ya wananchi na Serikali huku akidai kuwa kuna siri imebainika kuwa wabunge wanaoshinikiza gesi itoke Mtwara, wamepewa mamilioni ya fedha na Serikali.

“Kwa mfano gridi ya taifa ingeanzia Mtwara ingekuwa ni karibu zaidi kuliko gridi hiyo kujengwa katika eneo jingine. Mbona  kujenga bomba ni gharama kuliko gridi hiyo?,” alisema Mkwachu.

Alisema kwamba Serikali inavyochukua muda mrefu kutoa suluhu ya mgogoro huo, inajipalia makaa kwa sababu mikoa ya Mtwara na Lindi imebobea katika umaskini kwa miaka mingi.
Mkwachu alisema kuwa hadi kufikia jana saa kumi jioni, baadhi ya majengo yalikuwa yakiendelea kuteketea kwa moto, huku askari kutoka Nanyumbu na Nachingwea wakiletwa ili kusaidia kutuliza ghasia hizo.

Maaskofu watoa tamko
Wakati hayo yakiendelea, Baraza  la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste (PCT) Mkoani Mtwara, limetoa tamko likiitaka  Serikali isitishe mpango wake wa kusafirisha  gesi  kutoka Kijiji cha Msimbati mkoani humo, kwenda Kinyerezi Dar es Salaam.

Tamko hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Charles Chilumba walipozungumza na waandishi wa habari katika klabu ya waandishi wa habari Mtwara (MTPC), iliyopo mjini humo.

Chilumba alisema kuwa Serikali inatakiwa kuwa sikivu na kusikia kilio cha wananchi wa Mikoa ya Kusini  ya Lindi na Mtwara, ambako vyanzo vya uchumi wa gesi vipo ili kutekeleza madai yao.
Alisema kuwa, viwanda vya mbolea, plastic na saruji ambavyo viliahidiwa kujengwa, vijengwe sasa na zisiwe propaganda za kisiasa kutoka kwa viongozi wa Serikali, ili  kuondoa dhana iliyokuwapo miaka ya nyuma kuwa kusini ni  ukanda wa vita, hivyo hakuna sababu ya kuendelezwa.

“Serikali isisikilize wabunge wadanganyifu, ambao hawana makubaliano na wananchi katika majimbo wanayotoka, ambao huchochea mgogoro huu kwa lengo lao na masilahi yao binafsi,”alisema Chilumba.

”Inabidi wawaombe radhi bila masharti kwani semi zao  zinaleta chuki, uhasama, utengano katika nchi na kusababisha nchi isitawalike. Serikali ya CCM itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 Ibara ya 63 kifungu H na K,”alisema.

Viongozi wa dini hao wameomba Mungu awape hekima viongozi wa  Serikali kwa kuwa wamepewa dhamana na Mungu kuliongoza taifa kwa umahiri, wakionya kuwa ukaidi wa wenye fitina utawaangamiza.

Alipotafutwa msemaji wa Jeshi laPolisi nchini, Advera Senso alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo na kuomba atafutwa Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Maria Nzuki.

“Sawa lakini, naomba umtafute Kamanda wa Polisi wa Mtwara yeye ndiye ataweza kukujibu unachokiuliza,” alisema Senso.

Hata hivyo gazeti hili lilimtafuta Nzuki bila mafanikio kwani simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alipotafutwa alisema kuwa yeye siyo msemaji.
“Mimi siyo msemaji wa masuala hayo, mtafute Waziri (Emmanuel Nchimbi) yupo atazungumzia hilo,” alisema Silima.

Waziri Nchimbi naye kama ilivyokuwa kwa Kamanda Njiku, simu yake ya mkononi jana ilikuwa haipatikani.

Morogoro
Mkoani Morogoro mtu mmoja anayeaminika kuwa ni mfugaji katika Wilaya ya Itete, mkoani Morogoro ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kundi kubwa la wafugaji kuvamia viongozi wa halmashauri waliokamata mifugo yao kwa madai ya kulisha maeneo yaliyozuiwa.

Tukio hilo limetokea jana asubuhi baada ya viongozi wa eneo la Itete wilayani Ulanga, kupata taarifa kuwa kuna makundi ya mifugo yaliyokuwa yakilishwa ndani ya hifadhi ya ardhi oevu, ambayo Serikali imepiga marufuku kulisha mifugo.

Kwa mujibu wa ofisa mmoja aliyekuwapo kwenye operesheni ya kukamata mifugo hiyo na ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kundi hilo kubwa la wafugaji wakiwa na silaha za jadi waliwavamia na kuanza kuwashambulia kwa lengo la kuchukua mifugo yao iliyokuwa imekamatwa.

Alisema kwamba viongozi hao wa halmashauri walipewa taarifa ya kuwepo kwa mifugo hiyo katika eneo hilo na walipofika waliikuta mifugo hiyo na kuamua kuichukua kisha kuipeleka kwenye makambi yaliyotengwa kuhifadhi mifugo wilayani hapo.

“Baada ya kuchukua mifugo ile, wafugaji walipata taarifa kuwa tumeikamata mifugo yao, ndipo walipojikusanya na kutuvamia tukiwa njiani na kuanza kutushambulia,” alisema ofisa huyo.

Aliongeza kuwa katika kundi hilo la viongozi wa wilaya, walikuwa na askari wawili tu, huku mmoja ndiye aliyekuwa na bunduki, ambapo licha ya kupiga risasi hewani kuwatawanya, wafugaji hao walizidi kuwashambulia.

“Askari yule alipoona maisha yake yako hatarini ndipo alipoanza kuwafyatulia risasi wananchi hao na kumpata mmoja na kufariki huku wengine wote kukimbia,” alieleza

Wakati huo huo, zaidi ya wafugaji 400 wa Kijiji cha Mabwegele Kata ya Kitete, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa walikusanyika katika kijiji hicho wakipinga kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ya kutenguliwa uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kukipandisha hadhi na kuwa kijiji kamili, jambo ambalo lilizua vurugu kubwa katika mji mdogo wa Dumila jana.

Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa Kijiji cha Mabwegere wilayani Kilosa, Sharifu Kasenga alisema kuwa wafugaji hao wamekusanyika katika kijiji hicho baada ya kusikia taarifa za uharibifu wa mali za wafugaji katika mji wa Dumila wakati wa vurugu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alilieleza gazeti hili kuwa hali ya amani imerejea katika mji mdogo wa Dumila pamoja na kitongoji cha Mabwegere.

Imeandikwa na Florence Majani, Dar Mwanja Ibadi, Masasi, Juma Mtanda, Venance George, Morogoro