Maswali kumi kwa Mbunge wangu: Abdul-Aziz Abood

Mbunge wa Morogoro mjini, Abdul-Aziz Abood

Muktasari:

Bado naendelea na mradi huo wa kuchimba visima katika maeneo mengine, sambamba na kuboresha miundombinu ya usambazaji maji ili kumaliza tatizo la ukosefu wa maji.

Hamida Shariff

1.Juma Ng’ondavi, mkazi wa kihonda

Lini tatizo la ukosefu wa maji katika maeneo mengi ya jimboni kwako litaisha?

Jibu: Tatizo la ukosefu wa maji litakwisha muda si mrefu kwa kuwa naendelea kufuatilia kwa karibu miradi ya maji iliyopo jimboni kwangu ukiwepo mradi wa MCC ambayo itaboresha vyanzo vya maji, lakini pia kwa juhudi zangu binafsi nimechimba visima virefu 24 katika maeneo mbalimbali yenye kero ya maji.

Bado naendelea na mradi huo wa kuchimba visima katika maeneo mengine, sambamba na kuboresha miundombinu ya usambazaji maji ili kumaliza tatizo la ukosefu wa maji.

2.Mussa Okita, Mkazi wa Mazimbu

Umesaidiaje wanafunzi wanaotoka kwenye familia maskini ambao wanashindwa kumudu kulipa ada, kupata sare na mahitaji mengine ya shule?

Jibu: Kwa kutambua umuhimu wa elimu, hadi sasa nimewasaidia wanafunzi zaidi ya 4,220 waliopo kwenye shule za msingi, sekondari na hata vyuo na bado naendelea kuwasaidia wengine watakaobainika kuwa wanatoka katika mazingira magumu. Ni kufuata utaratibu tu kuhakikisha nani hasa hana uwezo wa kulipa ada wakati amefanya vizuri.

3. Filemon Mapunda, mkazi wa Kilakala

Unavisaidiaje vikundi vya ujasiriamali hasa vya kina mama na wafanyabiashara wadogo ili kuhakikisha wanakuza mitaji yao?

Jibu: Kwanza nimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha vijana, kina mama, watu wenye ulemavu na makundi mengine kujiunga kwa pamoja ili waweze kusaidiwa. Hata hivyo, hadi sasa nimeshavisaidia vikundi zaidi ya 631 vya wajasiriamali kwa kuviongezea mitaji au kuvisaidia vifaa mbalimbali kulingana na mahitaji yao; vipo vikundi nimevipa vyerehani, pikipiki na wanaendelea na uzalishaji mali.

4. Mohamed Mkwinda, mkazi wa Mjimpya

Je, unaishughulikiaje migogoro ya viwanja ambayo imekuwa ikitokea kila kukicha katika maeneo ya Kihonda, Mkundi, Lukobe, Tungi na maeneo mengine?

Jibu: Ni kweli kumekuwa na migogoro mingi ya viwanja katika jimbo langu lakini nimekuwa nikiishughulikia migogoro hii kwa karibu. Nimekuwa nikienda kwenye maeneo yenye migogoro nikiwa na wahusika wenyewe pamoja na maofisa wa ardhi wa manispaa ili kuona ukubwa wa tatizo na baadaye kwa kushirikiana na maofisa wa ardhi nimekuwa nikimaliza migogoro hiyo na ile inayoshindikana nimekuwa nikiiwasilisha kwa waziri husika kupitia bungeni na wananiahidi kuishughulikia.

5. Frank Graison, mkazi wa Kiwanja cha Ndege

Lini kero ya ubambikizaji wa ankra za maji itakwisha?

Jibu: Hili ni tatizo ambalo hata kwangu ni kero. Tatizo liko kwa watendaji wa idara za maji. Hiki ni kilio cha wananchi wa jimbo langu, wamekuwa wakizidishiwa ankara za maji tofauti na matumizi halisi. Nilifika kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Morogoro (Moruwasa) na kufuatilia suala hili na kwa sasa kero hii imepungua. Hata hivyo, kupitia mikutano yangu nimekuwa nikiwaambia wananchi wenye tatizo na ankara zao za maji kufika ofisini kwangu ili kushughulikia.

6. Pendo Mjema, Mkazi wa Barabara ya Kitope

Una mpango gani wa kuboresha vituo vya afya ili viweze kutoa huduma ya mama na mtoto?

Jibu: Tayari nimeshapeleka vitanda vya kujifungulia, vifaa vya kujifungulia, magodoro pamoja na vifaatiba katika kituo cha afya Kingolwira, Mafiga, Magadu, Kibwe, Chamwino, Mjimpya pamoja na kuanzisha ujenzi wa zahanati mbalimbali lengo likiwa ni kuboresha huduma ya mama na mtoto na bado naendelea kusaidia vituo vingine ili viwe na uwezo wa kutoa huduma ya kuzalisha.

7. Hassan Masenda, mkazi wa Boma

Lini barabara ya Mafiga hadi Kichangani itatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya mji?

Jibu: Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 barabara hiyo iko katika mpango wa kutengenezwa kwa kiwango cha lami, ninachotaka kusema hapa ni kutoa muda tu, utekelezaji utafanyika.

8. Boniface Kingson, Mkazi wa Barabara ya Kitope

Lini ujenzi wa soko la kisasa la Mkoa wa Morogoro utaanza mbona hakuna hata dalili?

Jibu: Ujenzi wa soko la kisasa utaanza ndani ya kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2014/2015 tayari kibali kimeshapelekwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi ili kuweza kupata mkopo kutoka kwenye benki au taasisi za fedha na mchakato huo utakapokamilika, haraka ujenzi utaanza.

9. Johari Mohamed, mkazi wa Tubuyu

Mbona barabara zilizopo pembezoni mwa mji kama Mafisa, Tungi na Kiegea zimesahauliwa. Una mpango gani wa kuziboresha barabara za mitaani?

Jibu: Zipo barabara za mitaani ambazo mimi mwenyewe kama mbunge niliwahi kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia greda ili lizichonge. Pia nimenunua makaravati kwa ajili ya kuweka kwenye mifereji ya kupitisha maji ya mvua.

Pia na nimekuwa nikishirikiana na wenyeviti wa mitaa husika na kuziainisha barabara ambazo ni kero. Hata hivyo, nimekuwa nikifuatilia kwa mhandisi wa manispaa kuangalia namna ya kuzifanya barabara hizi kuwa za kudumu na ninaendelea kupambana.

10.Lucas Mahumpa,Mkazi wa Forest

Lini kero ya foleni ya ulipaji wa ankara za umeme Tanesco itaisha?

Jibu: Tayari nimeshaifuatualia Tanesco baada ya kuonana na meneja wa mkoa nilimshauri uanzishwe utaratibu wa kisasa wa ulipaji wa ankara za umeme kwa njia ya benki na mitandao ya simu. Amelikubali hilo na kwa sasa utaratibu huo unaendelea kuandaliwa. Tatizo la foleni Tanesco litakwisha muda si mrefu endapo utekelezaji wa hayo niliyopendekeza ufafanyika.