MTERA, KONDOA KASKAZINI NA KONDOA KUSINI : UKAWA IJIFUNGE MKANDA

Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde

Muktasari:

Jimbo la Mtera linapatikana katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Wilaya ya Chamwino ilianza mwaka 2006 baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Halmashauri ya Dodoma Vijijini ambayo ilizaa Halmashauri ya Bahi na Chamwino.

Jumatano iliyopita tuliangazia majimbo ya Dodoma Mjini, Bahi na Chilonwa. Leo tunaendelea kuchambua majimbo ya Mkoa wa Dodoma tukijikita kwenye majimbo ya Mtera, Kondoa Kaskazini na Kondoa Kusini.

Kwa sababu wiki iliyopita tuligusia masuala mengi ya jumla kuhusu Mkoa wa Dodoma, leo tutagusia machache tu kabla hatujajikita majimboni.

 

JIMBO LA MTERA

Jimbo la Mtera linapatikana katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Wilaya ya Chamwino ilianza mwaka 2006 baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Halmashauri ya Dodoma Vijijini ambayo ilizaa Halmashauri ya Bahi na Chamwino.

Kwa mwaka 2014 wilaya ilikadiriwa kuwa na jumla ya watu 349,714. Kwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Wilaya ilikuwa na idadi ya watu 171,661 na wastani wa idadi ya watu kwa kaya ni 4.5.

Shughuli kuu za uchumi katika Wilaya ya Chamwino ni kilimo na ufugaji.  Mazao ya chakula yanayolimwa ni; mtama, uwele, mpunga, mahindi, mhogo, viazi vitamu, kunde, nyonyo, mboga mboga, choroko na mazao ya biashara ni ufuta, zabibu, karanga na hulimwa katika eneo linalofaa. Makadirio ya pato la mkazi kwa mwaka ni Sh540,000 kwa mwaka.

Tangu kuanza kwa vyama vingi nchini Tanzania na hasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Jimbo la Mtera liliendelea kuongozwa na Chama Cha Mapinduzi hadi leo. Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania, John Samwel Malecela, ndiye aliyefungua pazia la ushindi wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 1995 kwa kupata kura 27,368 dhidi ya kura 1,052 za mgombea wa CUF. Malecela alishinda pia uchaguzi wa mwaka 2000.

Katika Uchaguzi wa Mwaka 2005, John Samwel Malecela wa CCM alipata ushindi wa asilimia 92.7 uliotokana na kura 42,994 huku wagombea wa CUF, TLP, UDP, DP na Chadema wakipata jumla ya kura 3,392 (asilimia 7.3) katika uchaguzi rahisi sana kwa CCM. Hata kwa upande wa kura za Rais, Jimbo la Mtera bado lilitekwa na nguvu ya CCM na mgombea urais wake alipata kura 44,586 (91.4) huku akiwaacha mbali wagombea wa urais wa upinzani ambao walipata kura 14,174 (asilimia 8.6).

Kura za maoni za ndani ya CCM zilizofanyika mwaka 2010 zilizima ndoto za kisiasa za Mzee Malecela. Safari hii aliangushwa na kijana mdogo wa umri wa kumzaa. Watu wengi hudhani kuwa, mwanasiasa nguli kama Mzee Malecela, mwenye uzoefu wa kuwa Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, msomi wa ngazi ya shahada ya uzamivu – kwamba angehitaji kupambana na nguli mwenzake na mwenye sifa kama zake ili aangushwe, la hasha! Mambo yalikuwa tofauti sana.

Kijana Lusinde Joseph Livingstone akiwa na umri wa miaka 38 tu alifanikiwa kumng’oa kiongozi mkubwa na mzoefu katika siasa za Tanzania. Lusinde ana historia mchanganyiko ya kisiasa, Mwaka 1992 – 1995 alikuwa mwanachama wa CUF na aliwahi kushikilia wadhifa wa Katibu wa Jimbo la Kawe, baadaye alihamia Chadema na kushikilia wadhifa  muhimu pia na baadaye Lusinde alihamia CCM na kupewa wadhifa wa Katibu Msaidizi kati ya mwaka 2006 – 2007 na baadaye akawa Katibu wa CCM wa Wilaya mwaka 2006 - 2010. Lusinde ana elimu ya darasa la saba tu na ana cheti cha Uongozi kutoka Chuo cha CCM cha Ihemi.

Baada ya CCM kumteua kuwa mgombea ubunge, alipata ushindi mkubwa wa kura 23,612 (asilimia 80.02) dhidi ya kura 4,955 (asilimia 16.79) za wagombea wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR na UDP. Jimbo la Mtera ni kielelezo cha kutosha kuwa vyama vya upinzani vina kazi ya ziada ya kufanya katika Mkoa wa Dodoma. Baada ya Mzee Malecela kushindwa kura ya maoni kulitokea mpasuko mkubwa wa CCM jimboni humo, lakini mpasuko huo haukuvinufaisha vyama vya upinzani.  Kwa upande wa wagombea urais, jimbo la Mtera lilitoa matokeo yaleyale yaliyotarajiwa, CCM ilijibebea ushindi mkubwa wa asilimia 82.31 (kura 24,248) huku vyama vya CUF, Chadema na NCCR vikipata kura 3,759 (12.76) na vyama vya APPT, UPDP na TLP vikipata jumla ya asilimia 1.52.

Kati ya mwaka 2010 – 2014 vyama vya Upinzani havijafanya kazi kubwa ya kisiasa katika jimbo la Mtera na hata Mbunge wake Livingstone Lusinde hajasifika kwa kufanya jambo lolote kubwa katika jimbo hilo. Wananchi wa Mtera na maeneo ya Dodoma ni kati ya wananchi wenye vipato vya chini sana hapa Tanzania na hakujawa na mikakati bayana ya kukuza vipato vyao kupitia sekta za kilimo na ufugaji.

Kwa hivyo, mchuano mkubwa wa ubunge katika jimbo hili utakuwa ndani ya CCM na tayari makada kadhaa wa CCM wameonyesha nia ya kugombea kwenye kura za maoni za CCM. Mmoja ni William Malecela “Le Mutuz” (mtoto wa mzee John Malecela) ambaye sehemu kubwa ya maisha yake ameifanya ughaibuni na baada ya kurejea nchini amepata nafasi ya kushiriki siasa za CCM moja kwa moja. Kwa sababu Lusinde ni  mbunge mwenye vituko, kejeli na kila aina ya siasa za kuchangamsha na kushangaza, kuudhi na kubughudhi sana, kuna uwezekano mkubwa kuwa CCM ikamrejesha tena kugombea Oktoba mwaka huu ikiwa William Malecela hatajipanga zaidi.

WILAYA YA KONDOA

Wilaya ya Kondoa ni moja kati ya wilaya za Mkoa wa Dodoma. Katika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa Wilaya ya Kondoa ilikuwa 269,704. Wilaya hii ina majimbo mawili ya uchaguzi, Jimbo la Kondoa Kaskazini na Kondoa Kusini.

Wilaya ya Kondoa ilianza kama kituo cha biashara katika karne ya 19 na ni mji ambao ulipokea madhehebu ya dini mapema kabisa. Msikiti wa kwanza ulijengwa Kondoa mwaka 1885 na kanisa la kwanza lilijengwa mwaka 1910. Wakati wa ukoloni wa Kijerumani mji ulijulikana kwa jina Kondoa-Irangi ukawa kituo cha jeshi la kikoloni la Kijerumani. Mwaka 1912 ilikuwa makao makuu ya mkoa mpya wa Kondoa-Irangi. Makabila makuu ya wilaya hii ni Warangi, Wasandawe, Waburunge na Wasi. Kirangi ndiyo hasa lugha ya Warangi, ambayo wao huiita “Kilaangi”.

JIMBO LA KONDOA KASKAZINI

Jimbo hili tangu mwaka 1995 lilikuwa chini ya CCM. Khalid Samure Suru msomi wa stashahada ya Ualimu ya Chuo cha Ualimu Marangu alishinda uchaguzi wa mwaka 1995 akipata upinzani hafifu. Pia, Mwaka 2000 Khalid Samure Suru alishinda na kuongoza kwa kipindi cha pili hadi mwaka 2005.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, CCM ilimleta mwanamama Zabein Mhaji Mhita. Mhita aliyezaliwa Septemba 9, 1950 (Miaka 65 sasa) na mhitimu wa shahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa na uzoefu wa kufanya kazi kama mkurugenzi wa elimu wa wizara ya Elimu, aliipatia CCM ushindi wa kura 42,899 (asilimia 60.8) dhidi ya mgombea wa CUF, Othman Omar Dunga aliyepata kura 26,592 (asilimia 37.7) huku wagombea wa DP na TLP wakipata jumla ya kura 1,020 (asilimia 1.4). Kwa upande wa urais, Jakaya Kitwete wa CCM alipata kura 47,521 (asilimia 64.6), akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF 24,521 (asilimia 33.5) huku wagombea urais wengine wanane wakipata jumla ya kura 1371 (asilimia 1.9).

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, mgombea wa CUF ambaye alikuwa amekwishajijenga vya kutosha na alitarajiwa kulichukua jimbo hilo kirahisi uchaguzi ambao ungefuatia, Omar Dunga, alihamia CCM na kuua chachu aliyokuwa ameianzisha. Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 ulishuhudia upinzani mkali kutoka kwa Mgombea wa CUF, Deni Yahya Rashid aliyeishia kupata kura 17,413 (asilimia 31.13) huku Mgombea wa CCM yuleyule  Zabein Muhaji Mhita akipata kura 33,413 (asilimia 59.74) na kushinda ubunge kwa kipindi cha pili (2010 – 2015) safari hii akiwa na uzoefu wa miaka saba kama Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (2000 – 2005) na Maliasili na Utalii (2006 – 2008). Wagombea wa Chadema na UDP kwa ujumla walipata kura 3,482 (asilimia 6.23).

Nguvu, uwezo na ubora wa chama cha CUF katika jimbo la Kondoa Kaskazini ni jambo lililo dhahiri. Mara zote CCM inashinda si kwa zaidi ya asilimia 61. Kukosekana kwa mgombea mahiri, mwenye msimamo na anayeweza kuaminiwa na wananchi imekuwa ni tatizo ambalo limeikabili CUF katika jimbo hili. Wagombea wake mara nyingi hurubuniwa mara tu baada ya uchaguzi mmoja na kukosa fursa ya kulichukua jimbo hili katika uchaguzi unaofuata. Wananchi wa Kondoa Kaskazini wako tayari kwa mabadiliko, amekosekana mtu wa kuongoza mabadiliko hayo kutoka upinzani.

Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni muhimu mno kwa CUF kuweka mgombea sahihi na anayekubalika na mwenye uwezo wa kushinda jimbo hili, lakini, nguvu za CCM si za kubeza, zinatosha pia kuiwezesha CCM kulibeba ikiwa Ukawa, hususani CUF haitajipanga kumpata mgombea madhubuti. Japokuwa, taarifa nilizonazo zinaonesha kuwa, mbunge wa Viti Maalumu wa CUF Moze Abeid Said anayetokea Wilaya ya Kondoa, anajipanga kuomba ridhaa katika jimbo hili na kwamba amekwishafanya kazi za kisiasa na kimaendeleo katika maeneo mbalimbali ya Kondoa tangu mwaka 2011, muda haufichi kitu, tutajua mbivu na mbichi siku si nyingi.

JIMBO LA KONDOA KUSINI

Kondoa Kusini kama lilivyo Jimbo la Kondoa Kaskazini, limedhihirisha ukuaji na uimara wa upinzani. Wananchi wameendelea kuonyesha kuwa tayari kwa mabadiliko huku upinzani hasa CUF ikikosa watu thabiti wa kulichukua jimbo hili na hivyo kuifanya CCM iendelee kujikita.

Jimbo la Kondoa Kusini limeongozwa na mbunge mmoja kwa vipindi vitatu mfululizo, huyu ni Paschal Constantine Degera wa CCM. Ameliongoza jimbo hili tangu mwaka 1995 – 2000, 2000 – 2005 na 2005 – 2010 na bado alijaribu kuliongoza mwaka 2010 lakini akaangushwa kwenye kura za maoni za ndani ya CCM zilizoshuhudia Juma Nkamia (mbunge wa sasa) akipata kura nyingi. Juma Nkamia ni mwandishi wa habari mzoefu hapa Tanzania akiwa na Stashahada ya Uandishi wa habari aliyoipata mwaka 1999. Alizaliwa Januari Mosi, 1972 (miaka 43 sasa) na ni Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo tangu Januari 2014 hadi sasa.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 (kipindi cha mwisho cha uongozi wa Degera) aliipa CCM ushindi wa kura 42,155 (asilimia 70.6) dhidi ya kura 14,154 (asilimia 23.7) za Hassan Ally Misanya wa CUF. Wagombea wa Chadema na TLP kwa jumla walipata kura 3,364 (asilimia 5.6). Kwa upande wa wagombea urais, Jakaya Kikwete wa CCM alipata kura 49,492 (asilimia 79.7) huku Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akifuatia kwa kura 10,476 (asilimia 16.9) na kisha wagombea urais wengine wakapata kura 2,151 (asilimia 3.4).

Wakati CCM ilipomuweka Juma Nkamia mwaka 2010, CUF ilimuweka Missanya Hassan Ally kwa mara ya pili, wakiwa wagombea wawili tu katika kinyang’anyiro cha ubunge. Nkamia alishinda kwa asilimia 79.49 akiwa na kura 38,876 huku Missanya Hassan Ally wa CUF akiwa na kura 8,010 zilizompa asilimia 16.38 ya ushindi. Wagombea urais bado walimwachia nafasi Jakaya Kikwete wa CCM aliyepata kura 37,172 (asilimia 76.55).

Hali hii inamaanisha kuwa, itaipasa CUF kutiazama ikiwa bado Missanya Hassan Ally anafaa kupambana na Juma Nkamia ambaye naamini atapitishwa tena na CCM kuwa mgombea, Oktoba mwaka huu. Kwa sababu ushindi wa Missanya ulikuwa wa asilimia 23 mwaka 2005 na umekuwa wa asilimia 16 mwaka 2010, ni lazima Nkamia atafutiwe mgombea mwingine thabiti na aliyejipanga ikiwa Ukawa itahitaji kuleta ushindani mkubwa jimboni humo mwaka huu.

MATATIZO YA KONDOA KWA JUMLA

Wabunge wa sasa, waliopita na wajao wa majimbo ya Kondoa Kaskazini na Kusini, wanakabiliwa na changamoto zilezile za utendaji. Kondoa ni miongoni mwa wilaya ngumu kuanzia kwenye mazingira yake, hali ya hewa, mfumo mzima wa maisha ya jamii, elimu duni, matatizo ya maji, afya, usafiri n.k. Nilipotembelea Kondoa katika moja ya vijiji mwaka 2012 nilishuhudia binadamu na wanyama (ng’ombe) wakichuana kujipatia maji katika chemchemi moja. Kondoa inahitaji kuwa na wabunge imara, watakaosimama kidete kuhimiza halmashauri pamoja na Serikali Kuu ishiriki moja kwa moja kutatua kero kubwa za wananchi hao. Kwa sababu CUF imejikita sana katika majimbo yote mawili na imeonyesha ushindani mkubwa wa kisiasa tangu mwaka 1995, ni wakati mwafaka wa kujipanga zaidi ili kuwapa wananchi machaguo bora kuliko kuweka wagombea dhaifu ambao wataifanya CCM ishinde itakavyo na hivyo demokrasia kutia vigingi.

(Mchambuzi wa ukurasa huu, ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi wa kisiasa ndani ya Tanzania. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759, “mailto:[email protected][email protected] – Uchambuzi na Maoni haya kwa vyovyote vile ni maoni binafsi ya mwandishi).