Damu Salama kanda ya Ziwa yajikita kutoa elimu

Muktasari:

Ndaki amesema hayo kutokana na hospitali kukabiliwa na upungufu wa akiba ya damu kunakotokana na hofu ya kupimwa na kugundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) miongoni mwa wananchi.

Mwanza. Ofisa Ubora wa Damu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Ziwa, Emmanuel Ndaki amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwaondoa hofu wananchi waweze kuchangia damu.

Ndaki amesema hayo kutokana na hospitali kukabiliwa na upungufu wa akiba ya damu kunakotokana na hofu ya kupimwa na kugundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) miongoni mwa wananchi.

Amesema ugonjwa huo umekuwa ni miongoni mwa vikwazo vya watu wengi kukwepa kujitokeza kuchangia damu.

“Ni hiari ya mtu kupima VVU  na kupokea majibu. Tunachohitaji ni watu kujitolea kuchangia damu. Tukishapima hatutoi majibu kwa wahusika bila ridhaa yao,” amesema Ndaki.

 Ametaja kukosa uaminifu kwenye ndoa na uhusiano ni miongoni mwa sababu zinazowafanya kuwa na hofu wanapoombwa kuchangia damu wakidhani wameathirika.