NYANZA: Mtoto wa miaka 14 abakwa na vijana watano kwa zamu

Muktasari:

  • Adaiwa kuzirai na ni miongoni mwa waliochaguliwa kujiunga  na kidato cha kwanza mwakani

Mara. Vijana watano wanadaiwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 14 kwa zamu hadi kuzirai. Mtoto huyo alikuwa akitokea Kata ya Nyamatere kusherehekea matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Musoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Phillip Kalangi alisema tukio hilo lilitokea Desemba 20, mwaka huu saa 2.00 usiku katika Mtaa wa Wakala mjini hapa.

Kamanda Kalangi alisema mtoto aliyetendewa unyama huo ni miongoni mwa watoto wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, baada ya kuhitimu katika Shule ya Msingi Buhare.

Kamanda huyo akielezea chanzo cha tukio hilo, alisema mtoto huyo alikuwa njiani akienda nyumbani kwao katika Mtaa wa Makoko Zanzibar akitokea katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Nyamatare kwenye sherehe za ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema njiani alikutana na kundi la vijana watano ambao wote alikuwa akiwatambua kwa sura, ghafla vijana hao walimkamata kwa nguvu na kumpeleka katika nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika na kuanza kumbaka kwa zamu hadi mtoto huyo alipopoteza fahamu na kisha vijana hao kutoroka.

Alisema mtoto huyo alizinduka saa nane usiku akiwa hajiwezi, kwa msaada wa Mungu aliweza kujivuta hadi katika nyumba zilizo jirani na nyumba hiyo na kuomba msaada, majirani hao walimfikisha katika kituo cha polisi usiku huo na kupewa fomu namba tatu, walimpeleka kupata matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mara.

Kamanda alisema hali yake kwa sasa inaendelea vizuri na tayari polisi wanamshikilia mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa, mkazi wa Mtaa wa Nyamatare mjini hapa na atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.