Kila mwananchi anayo nafasi kushiriki ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini

Washiriki wa Jukwaa la Fikra wakiwa katika ukumbi wa Kisenga wa jengo la LAPF jijini Dar es Salaam walipohudhuria kongamano hilo hivi karibuni. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Tanzania inajenga uchumi wa viwanda utakaompa kila mwananchi fursa ya kuushiriki. Inashauriwa, kila mmoja afanye anachoweza mahali alipo. Anayeweza kuzalisha malighafi afanye hivyo, msambazaji au mtoa huduma nyinginezo pia aendelee na majukumu yake kuhudumia viwanda na wafanyakazi waliopo na watakaokuwapo.

Safari ya kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda ilianza miaka mingi iliyopita japo japo sasa kuna vitendo na mkazo nzaidi hasa wa Serikali.

Waziri wa Viwanda, Bishara na Uwekezaji, Charles Mwijage anasema safari hiyo ilianza tangu mwaka 1961 wakati Tanzania inapata uhuru kwa kurithi viwanda 125 kikiwamo cha Coca-Cola na cha sigara.

Anasema historia hiyo iliendelea hadi mwaka 1964 kilipojengwa kiwanda cha Tipper na General Tyres ambavyo mwaka 1967, baada ya Azimio la Arusha, Serikali ilivitaifisha na kuviweka chini yake.

“Yalikuwa ni maamuzi thabiti. Na mimi kama mfuasi wa Mwalimu (Julius Nyerere) nathubutu kusema yalikuwa ni maamuzi ambayo yangeleta maendeleo,” anasema Mwijage.

Anasema baada ya kuvichukua hali ilikuwa ndivyo sivyo, zipo sababu ambazo zilizofanya viwanda hivyo vishindwe kufanya vizuri ikiwemo mipango iliyotegemea zaidi kutengeneza bidhaa tunazozihitaji nchini.

Pamoja na hayo, nchi ilipata mtikisiko wa kiuchumi ikiwemo bei za mafuta, vita vya Kagera na utegemezi wa fikra katika kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu viwanda.

Serikali kutaka kushikilia uendeshaji wa viwanda na lilikuwa tatizo la mafanikio na Mwijage anasema ndio maana mmabadiliko ya sera yalifanywa. Anasema mpango endelevu wa viwanda (1996-2020) unahimiza kutoka kwenye fikra hizo na kuitanguliza sekta binafsi.

Anasema mwaka 1997, kipindi cha uongozi wa awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ilitungwa dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2020-2025 iliyolenga kujenga uchumi utakaoboresha maisha ya wananchi.

“Uchumi tunaoulenga sisi ni wa mwananchi kuwa na kipato kisichopungua Dola 3,000 za Kimarekani kwa mwaka,” anasema waziri huyo.

Kufanikisha hayo yote mwaka 2025 au kabla ya hapo, anasema ni lazima nchi iwe na utulivu, amani na utawala bora utakaowawezesha wananchi kutafuta maarifa na teknolojia ya uzalishaji mali, kujifunza kwa wepesi ili kuimarisha kipato chao na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Amani na utulivu anasema unajengwa kwenye mazingira yenye usawa hasa wa kipato hivyo ni lazima wananchi wote wajumuishwe kwenye mkakati huo.

Wanachotakiwa kufanya wananchi ili kushiriki katika kujenga uchumi jumuishi ni kila mtu kufanya kazi kwa upande aliopo kusaidia kuzalisha malighafi, kutoa huduma tofauti kwa kiwanda, wafanyakazi au jamii inayokizunguka.

“Kama unalima matunda na mwingine anayasafirisha mpaka kwa anayesindika au kukamua juisi kila mmoja anakuwa amehusishwa kujenga uchumi wa viwanda kwa nafasi yake,” anasema Mwijage.

Kuhakikisha ushiriki huo unawagusa wengi zaidi, anasema upo mpango wa miaka mitano ulioanza kutekelezwa mwaka 2011 unaolenga kuondoa vikwazo vya uanzishaji na ufanyaji biashara nchini.

“Dhima ya mpango huu ni ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu yanayopimwa kwa elimu, kipato na afya,” anasema Mwijage.

Katika ujenzi wa viwanda, kipaumbele ni vile vitakavyotumia zaidi malighafi zinazozalishwa na nchini ikiwezekana na wananchi wengi zaidi, vinavyozalisha bidhaa zinazotumika kwa wingi na vinavyolenga rasilimali maalumu kama gesi.

Hii anasema itatusaidia kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje na kuuza nje bidhaa za Tanzania akitolea mfano saruji, nondo na mabati.

Anaamini uchumi shindani utaitoa nchi kiuchumi kwa kutimiza malengo yaliyowekwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 huku akibainisha kuwa msisitizo mkubwa ni kujenga viwanda vidogo.

“Unapofikiria kuhusu kiwanda waza kile chenye uwezo wa kuajiri kuanzia watu wawili, wanne, au watano kisha uongeze kitakapoanza kukua kutoka kidogo kwenda cha kati na kuwa kikubwa,” anasema Mwijage.

Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia viwanda (Unido), Dk Stephen Kargbo anasema Serikali inatakiwa kuandaa sera thabiti kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Anasema sera nzuri zinaweza kuwavutia wawekezaji wengi kuwekeza fedha zao au kuingia ubia na mashirika yaliyopo ili kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi.

“Sio Serikali wala sekta binafsi, kila upande hauwezi kutembea peke yake bali kwa kushikamana” anasema.

Kutokana na aina ya uongozi uliopo nchini ambao unasimamia uwajibikaji na kutekeleza mipango kwa vitendo, anasema ana imani sera ya viwanda itafanikiwa hasa ukiwapo ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Tunajua, viwanda bila umeme ni kitu kisichowezekana hivyo tumekuwa tunafanya kazi kwa ukaribu na taasisi za Serikali kuhakikisha tunakuza nishati jadidifu kwa sababu ndicho kitu muhimu kwa miaka ijayo,” anasema.

Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Dk Edwin Mhende anasema sera, sheria na mikakati imara itaisaidia nchi kufikia azma yake ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.

Anasema suala hilo litatengeneza uwiano sahihi ili kila mtu ajue wajibu wake kwenye sera na sheria zote kuanzia mwaka 1996 kusaidia nchi kukimbizana na maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Mazingira ya ndani na nje yatamsaidia muwekezaji kuwa na uhuru katika kufanya biashara yake. Msongamano wa gharama uliokuwa unawekwa na TFDA na TBS wanapochukua sampuli moja kwa ajili ya kupima nayo ilikuwa inakatisha tamaa,” anasema Mhende

Mwijage na Mhende wanasema Serikali hivi sasa inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inawavutia wawekezaji kuzitumia fursa zilizopo nchini kwa kuwatengenezea mazingira rafiki na sera zinazoweza kuwashawishi.