Asilimia 30 ya wanawake wanapenda kupigwa

Muktasari:

Baadhi ya makosa ambayo wanawake hao waliulizwa na wao kujibu kuwa wanaona ni halali kuadhibiwa na waume zao ni ikiwa wameondoka nyumbani bila kuaga au wamewaacha watoto peke yao.

Dar es Salaam. Ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kuondoa Umaskini (Repoa) umeonyesha kuwa asilimia 70 ya wanawake wanafanyiwa ukatili wa kijinsia na asilimia 30 kati yao wanapenda kuadhibiwa na waume zao.

Baadhi ya makosa ambayo wanawake hao waliulizwa na wao kujibu kuwa wanaona ni halali kuadhibiwa na waume zao ni ikiwa wameondoka nyumbani bila kuaga au wamewaacha watoto peke yao.

Akisoma ripoti ya utafiti huo, Mtafiti Mwandamizi wa Repoa, Dk Frola Myamba alisema utafiti huo umebainisha kuwa kuna unyanyasaji mwingi katika makundi ya vijana.

“Kundi la vijana limeonekana kutekeleza unyanyasaji mwingi, waliowanyanyasa walikuwa wenza wao, katika hiyo asilimia 70, asilimia 30 ya wanawake waliona ni halali kupigwa. Tuliwauliza hilo swali wakasema ndiyo,” alisema.

Dk Myamba alisema miongoni mwa maswali waliyoulizwa wanawake hao wakati wa ukusanyaji wa takwimu yalikuwa; Je, ni halali wewe kupigwa na mume wako endapo umeondoka bila kuaga nyumbani au kufanya kosa fulani? Alisema baadhi walijibu “ndiyo” ni sahihi kupigwa.

Utafiti huo uliopewa jina la ‘Matokeo ya kuwekeza fedha ili kuwainua wanawake Tanzania 2016” ulitumia sampuli ya kaya 1,335 kutoka wilaya nane za Uyui, Kisarawe, Itilima, Kahama, Misungwi, Kilosa, Handeni na Mbongwe sanjari na Unguja kisiwani Zanzibar.

Utafiti huo ulifanyika kati ya Julai mwaka jana na Mei mwaka huu ukilenga kuangalia hali halisi ya uwezeshaji wa mwanamke kupitia mradi wa Tasaf na ulifanyika kabla ya kupata fedha za mradi huo katika awamu ya tatu mwaka 2013.

Pia, Repoa ilifanya utafiti mwingine kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kuangalia mradi huo (Tasaf) unawasaidiaje vijana wa umri wa kati ya miaka 14 hadi 28. Kundi hilo ndilo lilibainika kutekeleza unyanyasaji mkubwa wa kijinsia.

Katika utafiti huo ilibainika kuwa kijana mmoja kati ya wanne ndiye anayepata mahitaji muhimu ya chakula huku wengine watatu walionekana kuchanganywa na msongo wa mawazo unaotokana na maisha.

Dk Myamba alisema asilimia 63 ya watu katika kaya 800 zilizohojiwa, walionekana kuanza ngono katika umri wa chini ya miaka 18 tena bila kondomu.

Alisema Februari mwakani Repoa itakwenda tena kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo ili kujua mabadiliko yaliyojitokeza kwa mwanamke baada ya kupokea fedha za Tasaf.

Mkurugenzi wa Taasisi zisizo za kiserikali wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Marcell Katemba akizungumza kwa niaba ya Waziri Ummy Mwalimu, alikiri hali ya utofauti wa kipato na unyanyasaji kwa mwanamke kuwa bado ni changamoto kubwa kwenye jamii.

Alihimiza taasisi nyingine kuibua tafiti nyingi zitakazosaidia kuandaa sera itakayoweza kusaidia jamii.

“Serikali inahitaji kuona wananchi wake wanakuwa na maisha bora, wanakuwa na afya kwa hiyo matokeo ya tafiti hizi yataingia serikalini ili kusaidia uandaaji wa mipango yake,” alisema.

Kaimu mtaalamu wa utafiti kutoka Tasaf, Tumpe Lukongo alisema katika awamu hiyo ya tatu taasisi hiyo imepanga kufikia kaya 1,100,000 huku akifafanua kuwa mwanamke ndiyo hukabidhiwa fedha hizo kama kichwa cha familia kwa ajili ya kupanga bajeti mbalimbali.