Mwalimu Nyerere na siri ya maendeleo ya Kiswahili nchini

Muktasari:

Tukiangazia macho Kenya, tunaona kuwa Waingereza walipenyeza Kiingereza ambacho ni lugha rasmi ya taifa hilo hadi sasa. Hivyo, Kiswahili hakikuweza kustawi.

Katika Afrika ya Mashariki, tangu enzi za ukoloni mpaka sasa, Kiswahili kinaonekana kutamalaki zaidi Tanzania kuliko nchi nyingine.

Tukiangazia macho Kenya, tunaona kuwa Waingereza walipenyeza Kiingereza ambacho ni lugha rasmi ya taifa hilo hadi sasa. Hivyo, Kiswahili hakikuweza kustawi.

Nchini Uganda, Kiswahili hakikupendwa kwa sababu kilitumiwa na askari wa kikoloni kuwanyanyasa wazalendo; pia lugha za kikabila zilipewa kipaumbele. Burundi, Kiswahili kilionekana kama lugha ya watu wasiostaarabika. Rwanda nako, kwa sababu ya utawala wa kijadi, Kiswahili hakikupewa nafasi ya kutosha.

Tanzania ina historia tofauti. Badala ya kutumia lugha za kigeni kutokana na wageni waliopata kuwapo nchini; yenyewe imejikita katika matumizi ya Kiswahili. Suala hili halikuja kama ruya, bali limetokana na jitihada kubwa za Mwalimu Nyerere.

Akiwa kiongozi wa TANU, alikitumia Kiswahili katika kampeni za kisiasa za kuwaunganisha Watanganyika wote ili kupiga vita ukoloni. Hivyo, siasa na sera za TANU zilienezwa sehemu mbalimbali nchini kwa kutumia Kiswahili.

Wale ambao hawakukifahamu vizuri, ilikuwa nafasi nzuri kwao kujifunza. Ikumbukwe pia, sababu mojawapo ya Tanganyika kupata uhuru mapema ni lugha ya Kiswahili ambayo iliwaunganisha Watanganyika na kujiona kitu kimoja kutokana na jitihada za Mwalimu.

Kuanzishwa kwa asasi zilizoshughulikia ukuaji na ueneaji wa Kiswahili. Mwalimu Nyerere akiwa kiongozi mkuu wa nchi, alitoa idhini ya kuanzishwa kwa asasi hizo ili ziweze kushughulikia maendeleo ya Kiswahili nchini. Asasi hizo ni pamoja Tuki/Tataki (1964), Bakita (1967); UKUTA (1959), na asasi nyinginezo. Mchango wa asasi hizi ni mkubwa katika maendeleo ya Kiswahili nchini.

Septemba,1962, iliamriwa kuwa Kiswahili kitumike bungeni na katika shughuli zote za kiserikali. Mwaka 1964, Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya Taifa la Tanzania. Pia, kilitangazwa kuwa lugha rasmi Tanzania.

Mwaka 1965, Kiswahili kiliteuliwa kitumike kufundishia masomo yote katika shule za msingi nchini ilhali Kiingereza kilibaki kufundishwa kama somo.Mwalimu Nyerere ni mwandishi na mfasiri wa vitabu vya Kiswahili. Vitabu vilivyoandikwa na Mwalimu kwa Kiswahili ni pamoja na Ujamaa kama Msingi wa Usoshalisti, Demokrasia na Mfumo wa Vyama vya Siasa, TANU na Raia, Tujisahihishe. Pia, alifasiri tamthilia ya The Merchant of Venice (William Shakespeare) kama “Mabepari wa Venisi” kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.

Mpango wa Elimu ya Watu Wazima ambao ulianzishwa katika uongozi wake, ulienda sambamba na kuanzishwa kwa maktaba za vijiji ambazo zilisheheni vitabu vilivyoandikwa kwa kutumia Kiswahili vikiwa na maudhui tofauti.

Wakati anaachia madaraka kwa hiari mwaka 1985, Nyerere alitumia msamiati wa ‘kung’atuka’ neno lenye asili ya lugha yake ya Kizanaki. Tangu wakati huo neno hili lilipata mashiko na baadaye kuingizwa kwenye Kamusi ya Kiswahili. Hivyo kuongeza msamiati katika Kiswahili.

Hayo yote yalifanywa na Mwalimu Nyerere kwa mapenzi makubwa aliyokuwa nayo katika Kiswahili. Kwa nafasi yake ya ngazi ya juu ya uongozi, kama angekuwa na kasumba katika Kiswahili, basi historia ya Kiswahili ingekuwa tofauti na ilivyo sasa.

Mafanikio ya Kiswahili Tanzania yametokana na jitihada za makusudi za Mwalimu Nyerere. Kwa hakika, viongozi wa nchi nyingine za Afrika wangefanya kama Mwalimu, Kiswahili kingepiga hatua zaidi. Tufuate nyayo za Mwalimu!