Wednesday, March 20, 2013

Hivi Jeshi la Polisi linamtumikia nani?

 

By Elias Msuya

Siku niliposikia kuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Wilfred Lwakatare amekamatwa na polisi kwa madai ya kupanga mikakati ya uhalifu kupitia video iliyosambazwa na mitandao ya jamii nilibaki na maswali mengi.

Lwakatare alikamatwa siku moja tu baada ya video hiyo kusambaa kwenye mitandao ya jamii, huku zikiwa zimepita siku kadhaa baada ya tukio la kushambuliwa kwa Mhariri Mtendaji wa Habari Corparation, Absalom Kibanda.

Si kwamba napinga kazi za Jeshi la Polisi na wala siwafundishi kazi, lakini najiuliza, haraka hii ya kumkamata Lwakatare imetoka wapi (kama kweli amehusika)? Mbona video zinazohamasisha uhalifu zimejazana mitandaoni na wahalifu hawakamatwi?

Hivi karibuni kulikuwa na video inamwonyesha kiongozi mmoja wa dini akihamasisha mauaji kwenye mitandao ya intaneti. Lakini hatukusikia jeshi hilo likimfanya lolote.

Tulishuhudia mwaka jana aliyekuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari Dk Steven Ulimboka akishambuliwa na kutupwa msitu wa Pande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Hakuna jitihada za maana zilizofanywa na jeshi hilo kuwasaka na kuwakamata watesaji aliowataja, badala yake alikamatwa tu kijana mmoja aliyejipeleka kwenye Kanisa la Ufufuo na uzima Kawe jijini Dar es Salaam ndiyo akakamatwa na kesi yake inaendelea mahakamani.
Hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ni kulifungia gazeti la Mwanahalisi lililokuwa likitoa taarifa za mashambulio hayo na kuonyesha mwanga kwa waliotajwa na Ulimboka.

Mwaka jana tena tukashuhudia tena tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi ambaye alipigwa bomu la machozi baada ya kushambuliwa na polisi wa kutuliza ghasia (FFU) kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Baada ya Wizara ya Mambo ya ndani kuunda Tume iliyochunguza, matokeo yake yakafichwa kwa madai kuwa kesi iko mahakamani.

Hata hivyo Tume ya Haki za Binadamu na Baraza la Habari nchini (MCT) wakatoa taarifa zao zilizoonyesha makosa kwa Jeshi la Polisi na baadhi ya watendaji wa Serikali.

Kama kweli Jeshi la Polisi lingekuwa na huruma na raia wake lingemwacha kazini Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda aliyeongoza operesheni iliyoishia kwa mauaji hayo?

Mwaka huu tumeshuhudia shambulio tena kwa Absalom Kibanda. Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi huo, ndiyo tumesikia Lwakatare akihusishwa na video inayomwonyesha akipanga mikakati ya mashambulio.

Hivi Jeshi la Polisi likihusishwa na mikakati ya kudhoofisha vyama vya upinzani na kuisaidia CCM litapinga?

Kwa mfano, wakati Lwakatare anakamatwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela anapiga marufuku maandamano ya kudai maji yaliyoandaliwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kwa sababu zisizo na mashiko.

Mara ngapi jeshi hilo limepiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya upinzani huku likiruhusu mikutano ya CCM kwa sababu hizo hizo zilizokatazwa?
Jeshi hili linalopaswa kulinda raia na mali zao, sasa limegeuka kushindana na vyama vya upinzani tu.

Kwa hali hii Jeshi la Polisi linamtumikia nani, wananchi dhidi ya wahalifu au CCM dhidi ya wapinzani?

0754 897 287

-->