Wednesday, November 20, 2013

Wanaoutaka urais wa Tanzania 2015 wajitangaze

 

Dar es Salaam. Kadri Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 unavyokaribia ndivyo fununu za makada wa vyama vya siasa wanaotaka kuwania urais zinavyozidi kuongezeka.

Japo wenyewe hawathibitishi lakini tayari pilikapilika zao zinadhihirisha kujiandaa na mbio hizo. Kwa mfano wanaotajwa ndani ya CCM ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, Waziri Mkuu msaatafu, Fredrick Sumaye na wengineo.

Ndani ya Chadema wanaotajwa ni Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Naibu wake Zitto Kabwe, japo mwenyewe amesema hivi karibuni hatalizungumzia tena suala hilo.

Kwa CUF, inaeleweka wazi licha ya kusubiriwa kwa vikao rasmi vya chama kuidhinisha kwamba mgombea pekee huwa ni Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.

Kwa vyama hivi vitatu vinavyoonekana kuwa na ushawishi mkubwa kwa wapiga kura, mvutano mkali unaonekana kuwa ndani ya CCM. Huko tayari vibweka vimeshaanza kujionyesha miongoni mwa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.  Lakini ukiwauliza hao wanaofanyiana vibweka hivyo kama wana nia yoyote ya urais baada ya Rais Jakaya Kikwete, wanaruka kimanga.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu msataafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye akizungumza na waandishi wa habari alikuja na lundo la malalamiko dhidi ya kada mwenzake Edward Lowassa akidai kuwa anamfanyia mbinu chafu.

Sumaye alikwenda mbali akidai kuwa wapo washindani wenzake wanaozuia hata mialiko yake kwa kumhofia. Lakini alipoulizwa kama ana mpango wa kugombea urais alisita kuthibitisha.

Siyo yeye tu, hata Membe amewahi kuulizwa, akasema eti hadi aoteshwe. Lowassa naye hajawahi kuweka wazi ingawa anasema “tuliohuzunika pamoja tutashinda pamoja.”

Mara nyingi Lowassa amekuwa akionekana makanisani na mara nyingine misikitini akiongoza harambee za mamilioni ya pesa huku mwenyewe akidai kuwa fedha hizo huchangwa na rafiki zake. Hao marafiki ni kina nani? Wana lengo gani? Tafakari.

Sidhani kama hii ni njia sahihi kwa nchi yetu kwa wagombea hawa kuachwa tu wajipange kimya kimya bila kuhojiwa mapema.

Kama kweli mtu ana nia ya kuwa kiongozi wetu, lazima hata chama alichomo kimfahamu na wapiga kura wamwelewe mapema.

Hakuna sababu ya vyama walivyomo kuwazuia kujitangaza kwa sababu, mikakati ya kupata urais haianzii kwenye Halmashauri Kuu au Kamati Kuu ya chama.

Wapiga kura wana haki ya kuthibitishiwa kama nani ana nia ya kugombea na amelenga kuwafanyia nini. Kwanza itawasaidia hata wao, kujirekebisha hapa na pale watakapokosolewa.

Hii tabia ya pilika za chini kwa chini, fedha zinachangwa tangu Januari hadi Desemba, anayezitoa hajulikani, wala malengo yake, ni hatari mno. Tutakuja kuuziwa mbuzi kwenye gunia.

-->