
| Hatua za kuomba nafasi za masomo ughaibuni | Send to a friend |
| Tuesday, 10 August 2010 16:38 |
ALIHANGAIKA kutafuta nafasi za masomo ya elimu ya juu, hatimaye akaja kuipata nafasi hiyo nchini Marekani. Baada ya kufanikiwa, Ernest Makulilo, Mtanzania anayeishi na kusoma nchini… ameamua kuwasaidia wengine jinsi ya kuomba nafasi za masomo ya juu katika nchi za Ulaya na Marekani ikiwa ni mchango wake kama anavyoeleza katika mahojiano haya na mwandishi wetu. Swali: Sababu zipi zilikusukuma kuwasaidia wanaotafuta nafasi za masomo nje ya nchi? Jibu: Kwanza naomba niseme kuwa nilianza kuitoa huduma hii rasmi Julai mwaka 2007, na huu ni mwaka wangu wa tatu. Sababu kubwa ya kuingia katika huduma hii ni kwa kuwa nilihangaika sana kutafuta nafasi za masomo hadi kufanikiwa kuja hapa Marekani. Hivyo nikawa na taarifa nyingi za mtu unawezaje kupata nafasi hizi kwa Marekani na Ulaya. Sikuona kama ni jambo la busara kwa kuwa mimi nimehangaika basi na wengine nao wahangaike, hivyo niliamua kurahisisha njia ya watu wanaopenda kutaka kusoma zaidi kwa kupata udhamini ughaibuni. Kitu kingine kilichonisukuma kujikita katika suala hili ni kuwa na blog (gazeti tando) mahsusi kwa ajili ya kuweka taarifa za misaada ya masomo kwa watu wa nchi maskini. Niligundua kuwa blog nyingi zilizopo Tanzania zina vitu mchanganyiko, nikaonelea ni vema basi nianzishe kitu ambacho mtu akisema anataka nafasi za masomo basi ajue wapi pa kwenda na kupata msaada. Swali: Ukoje mwamko wa Watanzania katika kupata taarifa za vyuo ambazo wewe umekuwa ukizitangaza? Jibu: Mwamko wa Watanzania ni mdogo sana tofauti na mataifa ya Afrika Magharibi, Amerika ya Kusini na Asia. Watanzania wengi bado wana ile dhana na kasumba kuwa ili mtu aende Ulaya au Marekani kusoma ni lazima atoke katika familia tajiri au ya kisiasa. Hivyo wengi hukata tamaa mapema. Kitu kingine kinachosababisha mwitikio mdogo kutoka kwa Watanzania ni wengi wao kukosa ari ya ushindani kama ilivyo kwa Wakenya na watu wa nchi za Afrika Magharibi. Ukiachilia hayo, wengi hudhani upatikanaji wa nafasi hizi ni kitu rahisi mno. Ninapompa mtu taratibu za vitu gani ajiandae navyo ili aweze kuwa mshindani mkubwa na kufanikiwa kupata nafasi, wengi hukata tamaa. Baadhi ya Watanzania tunapenda vitu mteremko sana wakati uhalisia si huo tena. Dunia hii ni ya ushindani, inabidi Watanzania tubadilike, tuendane na ushindani uliopo katika dunia ya kibepari. Tuachane na fikra za kijamaa) Swali: Je wewe ni wakala wa vyuo au unaiendesha vipi huduma hii? Jibu: Mimi si wakala wa chuo au taasisi yoyote ile. Na hakuna mtu, chuo au taasisi yoyote ile inayonilipa kwa huduma hii. Naiendesha huduma hii kwa imani kwamba kuna watu wana ndoto kubwa za maisha yao, lakini ndoto hizo mara nyingi hufa kutokana na ufinyu au ugumu wa upatikanaji wa elimu ya juu Tanzania na katika nchi nyingi zinazoendelea. Hivyo ninachokifanya ni kuhakikisha watu hawa wanatimiza ndoto zao za kielimu na maisha yao kijumla. Aidha nimekuwa nikizipitia tovuti mbalimbali za vyuo na taasisi ambazo zinatoa udhamini wa elimu kwa watu wanaotoka nchi zinazoendelea. Nikishapata taarifa hizi, nazichuja kwa umakini na kuzihakiki kisha nazitangaza kwenye tovuti zangu ambazo ni www.makulilo.blogspot.com na www.scholarshipnetwork.ning.com. Kwa wale wenye maswali zaidi kuhusu taarifa fulani niliyoitangaza huniandikia barua pepe nami huwajibu kwa kutoa ufafanuzi husika. Swali: Nani hasa walengwa wa huduma zako na kwa nini? Jibu: Walengwa wakuu ni watu wenye nia na sifa ya kufanya shahada za Uzamili na Uzamivu, kwa Kiingereza Masters Degree na PhD. Kuna nafasi nyingi za makundi haya mawili kuliko wale wanaotaka kusoma shahada ya kwanza. Kwa digrii ya kwanza, inakuwa ngumu kupata udhamini kwa kuwa sababu nchi zote ambazo lugha mama si Kiingereza, hutumia lugha zao kama Kijerumani, Kifaransa na nyinginezo kufundishia katika daraja hili. Hali hii huwa kikwazo kwa waombaji wengi kwa kuwa wanalazimika kujifunza lugha hizi na baada ya kufaulu mitihani ya lugha ndio upate nafasi. Nchi zinazotumia lugha zao za ndani ni kama Sweden, Denmark na Ujerumani. Lakini kwa shahada ya pili na tatu, nchi hizi zimekuwa zikitumia pia Kiingereza Swali: Kwa hiyo unawaeleza nini Watanzania kuhusu hali hii? Jibu: Ninachowaambia wasome shahada ya kwanza Tanzaniaa au katika nchi nyingine za Afrika kisha shahada ya pili na tatu waende Ulaya, Marekani au nchi za mabara mengine. Swali: Kuna watu wengi wanaotumia njia hii ya mitandao kutafuta na kuomba nafasi za masomo bila mafanikio, nini sababu? Jibu: Kuna sababu nyingi zinazomfanya mtu akiomba asipate. Hili nitalifafanua kwa kirefu.Kwanza watu wafahamu kuwa kupata nafasi za masomo ughaibuni si jambo la bahati bali vigezo na kufuata taratibu husika. Kwa kukosa vigezo au kwa kushindwa kufuata masharti, wengi wamekuwa wakikimbilia kusema kuwa hawana bahati au kuna upendeleo. Kwa mfano ili mtu aweze kupata udahili na kisha udhamini, vitu vifuatavyo ni muhimu:Mosi, matokeo bora ya vyuo, vyuo vingi vinataka wastani wa daraja la pili la juu yaani Upper Sercond kwa Kiingereza.Pili, mwombaji aandike malengo yake kwa umakini na ufasaha kupitia kitu kiitwacho Statement of Purpose/Interest. Ukiandika kwa kulipua hata kama una matokeo mazuri, sahau kupata udhamini. Tatu, kuna kitu kinaitwa Writing Sample, hii ni kazi ambayo umeshawahi kuandika kama insha au utafiti wowote ule wakati unasoma. Lengo lake wanataka kujua uwezo wako wa kuandika mambo ya msingi. Nne,ni barua ya kukupendekeza kutoka kwa walimu wako au mahala unapofanyia kazi.Hawa nao wanapswa waiandike vizuri, waonyeshe uwezo wako wa taaluma na kazi. Pia kuna zoezi la kupima uwezo wa lugha kwa muombaji. Uingereza wana mitihani ya TOEFL na IELTS, wakati Marekani wana mitihani kama GRE na GMAT. Waombaji wahakikishe vyeti vyao vimethibitishwa uhalali na wakili au mahakama kama si nakala halisi. Baada ya hatua hii na ukishakuwa na vigezo, omba vyuo ila kumbuka vyuo unavyoomba viwe vimeshatangaza udhamini wa masomo kwa wanafunzi kutoka nje ya nchi husika. Lakini pia mwombaji asitosheke kuomba chuo kimoja. Anatakiwa kuomba vyuo zaidi ya ishirini ili kuwa na uhakika wa kupata udhamini mkubwa na ulio mzuri. Swali: Unanufaika vipi kama mtu binafsi kwa kuendesha huduma hii? Jibu: Mafanikio makubwa ninayopata ni kuwa na furaha ya kweli kutoka moyoni. Ninafurahi sana watu wanapozipitia tovuti zangu, kuzifanyia kazi na kisha kufanikiwa. Furaha hii ni zaidi ya pesa kwangu, maana mimi kujua mbinu hizi si kwa ujanja au werevu nilionao kwa wengine. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu kanipa maarifa haya, sina budi kuyafikisha kwa wengine wanaotafuta elimu au maisha.Moyo huu ndio ulionisukuma pia kuanzisha mfuko wa kijamii utakaoitwa Makulilo Foundation kwa lengo la kuongeza wigo wa taarifa na mbinu zaidi za upatikanaji wa nafasi za masomo. |



ALIHANGAIKA kutafuta nafasi za masomo ya elimu ya juu, hatimaye akaja kuipata nafasi hiyo nchini Marekani. Baada ya kufanikiwa, Ernest Makulilo, Mtanzania anayeishi na kusoma nchini… ameamua kuwasaidia wengine jinsi ya kuomba nafasi za masomo ya juu katika nchi za Ulaya na Marekani ikiwa ni mchango wake kama anavyoeleza katika mahojiano haya na mwandishi wetu. 











Comments
Pamoja sana
Jerome
Na pia hongera kwa kuamua kusadia watu bila malipo, maana huku bongo kuna mawakala kibao lazima uwalipe ili upate hizi info.
Mdau, UDSM