MwanzoContactsEmail
Home Makala Mchakato wa Katiba Mpya Ziwa Kisiba na mauzauza yake
BOOKMARK THIS PAGE
Ziwa Kisiba na mauzauza yake  Send to a friend
Monday, 05 December 2011 10:02

Peter Edson
KATIKA mkoa wa Mbeya Wilaya ya Rungwe kata ya Masoko kuna ziwa linalojulikana kwa jina la Kisiba, ziwa hili limepata umaarufu mkubwa miaka mingi iliyopita kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa wakoloni wa kijerumani waliweza kutupa mali nyingi ndani ya ziwa hilo na vitu vingine kuvifukia kwenye mahandaki.

Mali zinazosadikiwa kuachwa na wakoloni hao  ni pamoja na madini ya rubi, dhahabu, almasi, zebaki, fedha za kijerumani kama vile rupia,  silaha za kivita vikiwamo vifaru, risasi nyingi, bunduki, magari ya kivita yaliyomo kwenye mahandaki na pembezoni mwa ziwa hilo.

Wakazi wa eneo hilo wanaeleza  kuwa ziwa hilo lina umri wa miaka milioni hamsini, lina kina cha urefu wa mita 50 hadi 60 na mzunguko wake wa mraba ni maili moja.

Aidha historia ya ziwa hilo imegawanyika katika pande mbili ambapo kitaalamu linaelezwa kuwa ni ziwa Volkano.

Katika hali nyingine ziwa hili linaelezwa kuwa lilitokana na imani za kishirikina na mazingaombwe yaliyofanywa na Chifu wa Kikinga aliyejulikana kwa jina la Lwembe ambaye alifika katika eneo hilo lililokuwa lina makazi ya watu na kuomba maji ya kunywa akiwa na jamaa zake, lakini wakazi wa eneo hilo walimnyima na kumkejeli.

Baada ya muda alimfuata mwanamke mwingine aliyekuwa pembezoni mwa ziwa hilo na akakubali kumpatia maji baada ya kumpa maji alimuamuru ahamishe mali zake na kisha kuuchoma mkuki wake chini na maji yakaanza kujaa katika eneo hilo na kuwaua wanakijiji wote waliokuwapo katika eneo hilo.

Katika eneo hili za ziwa Kisiba kuna mali nyingi inayosadikiwa kuachwa katika eneo hilo na wajerumani.

Taarifa kutoa katika eneo hilo inaeleza wazi kuwa Wajerumani walipoondoka eneo hilo waliacha vitu mbalimbali na vitu vingine walivifukia na vingine kuviacha kwenye mahandaki waliyokuwa wakiyatumia enzi za ukoloni.

Akizungumza na Mwananchi, mwongoza watalii wa siku nyingi katika eneo hilo na mzamiaji majini, Joshua Mwakipesile anasema kwamba wakoloni waliacha mali nyingi ambayo kama Serikali itafanya mpango wa kuitaifisha basi itaweza kuilisha Tanzania kwa muda wa miaka 25.

Anasema awali Wajerumani walikuwa wakilitumia eneo hilo kama kambi yao ya jeshi namba tano, ambalo lilikusanya askari kutoka katika nchi za Zambia, Tanganyika, Malawi, Kongo na nyingine ambapo rasilimali nyingi zilizokuwa zikichumwa na wakoloni hao zilikuwa zikihifadhiwa eneo hilo kabla ya kusafirishwa.

Anasema baada ya vita ya pili ya Dunia iliyodumu kuanzia mwaka 1914 hadi 1918, Wajerumani walilazimika kuondoka nchini kwa nguvu na hivyo kuviacha vitu hivyo kwa kuweka alama na ramani maalumu kwenye miti na hata kwenye mawe zinazoonyesha kwa mahali hapo pamefukiwa vitu.
 
Mwakipesile anasema mpaka hivi sasa wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakiokota risasi pamoja na fedha za kijerumani ambazo hutoka katika ziwa hilo pindi linapopumua, lakini mbali na ishara zote hizo, Serikali imeendelea kukaa kimya bila kufanya jitihada zozote za kufuatilia suala hilo.

Anasema kinachoshangaza hivi sasa ni kwamba utitiri wa wazungu wamekuwa wakivamia eneo hilo kwa madai kuwa wanafanya utafiti, jambo ambalo si kweli kwani lengo lao mahususi ni kufuatilia mali zilizoachwa na Wajerumani.

Anasema mwaka juzi walifika baadhi ya wazungu katika eneo hilo na kutaka kutoa sanduku kubwa lililotupwa katikati ya ziwa hilo, kwa kuwa yeye ni mzamiaji alipatiwa vifaa akiwa na mwenzake ili waingie katika ziwa hilo na kurudisha taarifa.

Anasema walipoingia katika ziwa hilo walikuta katika eneo moja vipande vingi vya maboksi vilivyokuwa na risasi na walipoendelea mbele wakakuta alama kwenye miamba zinazoashiria kuwa eneo hilo kuna hatari na baada ya kuendelea mbele walikutana na samaki mkubwa kimo cha mtu mzima mwenye rangi nyeupe na nyeusi.

Anasema hata hivyo waliendelea mbele na kufanikiwa kuliona sanduku hilo lenye ujazo mkubwa lililohifadhiwa katikati ya ziwa kwa kujengewa na saruji ya kujenga madaraja baharini.
Anaongeza kuwa walipolisogelea walishuhudia likianza kubadilika na kuwa nyoka mkubwa aliyekuwa na vichwa kumi na viwili, walipoona kuwa ni hatari waliamua kuondoka katika eneo hilo.

“Ndugu yangu vitu hapa vipo, tena ni vingi sana na vyenye thamani kubwa, kusingekuwa na vitu katika eneo hili, hawa wazungu wasingekuwa wanakuja,” anasema Mwakipesile.

Viongozi wa Serikali ya mtaa katika eneo hilo wamethibitisha kuwapo kwa taarifa mbali mbali zinazohusiana na ziwa hilo.

Kiongozi mmoja aliyezungumza na Mwananchi anasema anasikitishwa sana na hali inayoendelea kujitokeza katika eneo hilo kwani hadi hivi sasa inasadikiwa kuwa wapo baadhi ya watu wanaofanya kila jitihada za kuhakikisha kuwa wanaitoa mali hiyo kwa maslahi yao binafsi.

“Unajua ndugu yangu sijajua Serikali yetu imelogwa ama ni nini kinachoendelea eneo hilo la ziwa Kisiba, dalili zote zinaonyesha dhahiri kuwa katika eneo hilo ipo mali nyingi lakini Serikali yetu haisadiki, msururu wa wazungu wanakuja kila leo lakini Serikali bado imekaa kimya,” anasema kiongozi huyo.

Anasema siku za hivi karibuni kuna  wazungu waliofika katika eneo hilo na kujitambulisha kuwa wanafanya utafiti wa miamba, baada ya siku kadhaa walikuja na mitambo mingi na yenye nguvu na kufanikiwa kuondoka na baadhi ya mali ambayo walikuwa wakiichukua wakati wa usiku.

Anasema wazungu hao waliofika katika eneo hilo wakiwa na maboti, pamoja na vifaa vingine, waliipandisha mashine kwenye boti hadi eneo la katikati ya ziwa mahali ambapo panasadikiwa kuwa na sanduku hilo lilihifadhiwa.

Anasema inapofika majira ya saa sita usiku walikuwa wakiondoka kwenda katikati ya ziwa hilo na kuwasha mashine waliyoiweka na kurudi saa nane usiku wakiwa na furaha kama vile wamefanikiwa kufanya utafiti wao.

“Tunaibiwa katika ardhi yetu wenyewe, sijua wasomi wako wapi, yaani tunaonekana sisi ni wehu na wala hatuna akili, kwani hii ni miaka mingi imepita tokea wakoloni kuondoka lakini hatufanyi chochote,” anasema kiongozi hiyo.

Aidha kiongozi huyo anasema kuwa inasadikiwa kwenye lango kuu la kuingia kwenye handaki sehemu ambayo limehifadhiwa kila aina ya zana za kivita kumetegwa mabomu ambayo kama eneo hilo litavamiwa kihasara basi maelfu ya watu wanaweza kupoteza maisha yao iwapo  mabomu yaliyofukiwa yatalipuka.

Anasema hivi karibuni Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange akiwa na baadhi ya maafisa wake na magari matatu walifika katika eneo hilo na kuchunguza, hata hivyo haikujulikana kuwa ni kitu gani walikuwa wakikiangalia kwani walifanya mambo yao na kisha kuondoka bila kuacha taarifa zozote.

Anasema mbali na hilo wapo watu waliojitambulisha kuwa wanatoka Malawi walishawahi kufika katika eneo hilo na kufanikiwa kutoa vitu mbalimbali zikiwamo baiskeli, bunduki aina ya bastola na pesa za kijerumani hata hivyo bado viongozi wakuu serikali hawajashtuka kuwa mahali pale kuna rasilimali.

“Unajua hii mali waliyoiacha hapa si kwamba ilikuwa yao ni yetu sisi Watanzania, kwani waliichuma katika ardhi yetu, lakini kutokana na ubinafsi wao ndiyo maana walizifukia katika eneo hilo ili baadaye watoto wao waweze kufika na kuzichukua.

“Tunachokishangaa ni kuona kampuni nyingi zikifika katika eneo hili na kudai kuwa wanafanya utafiti, hatuamini kuwa watu hao wanaofika katika eneo hili hufika kwa ajili ya maslahi ya Watanzania bali kwa ajili ya maslahi yao binafsi.”

Anasema baadhi ya watu waliweza kugundua eneo ambalo linasadikiwa kuwa na dhahabu kiasi cha tani tatu, baada ya kuanza kuchimba eneo hilo walifika kwenye eneo lililosakafiwa na saruji kali hivyo kulazimika kutumia baruti, walipotoka ndani ya shimo hilo na kurudi walishuhudia nyoka mkubwa akiwa ndani ya shimo hilo.

Anasema walikimbia na kisha kwenda kwa waganga, lengo likiwa ni kutajirika, baada ya kurudi na kufanya ndumba zao nyoka alitoweka lakini upepo mkali ulianza kuvuma eneo hilo na baadaye lilitokea fuvu la mtu lililokuwa likizungumza lugha isiyoeleweka, kufuatia hali hiyo watu hao walikimbia.

“Hadi sasa shimo hilo lipo, jambo hilo linaonyesha dhahiri kuwa wakoloni hao hawakuiacha mali hii hivi hivi bali waliiacha kwa kutumia mazindiko makubwa ndiyo maana watu wanashindwa kuitoa,” anadai kiongozi huyo.

Naye Joel Mwakatumbula anasema baadhi ya watu wamekuwa wakifika katika eneo hilo kwa ajili ya kujaribu kuchukua rasilimali hizo kwa njia isiyo halali kiasi cha kwamba wamejikuta wakiishia katika matatizo, jambo ambalo kama litaendelea basi linaweza kusababisha athari kubwa kwa jamii ya wakazi wanaolizunguka eneo hilo.

Anasema ni muda mrefu sana tangu kuwapo kwa hisia na tetesi kuhusu mali zilizotupwa katika ziwa hilo, hivyo ametoa wito kwa Serikali kufika eneo hilo na kuzitoa mali hizo ili wakazi wa eneo hilo wawe huru.
Aidha wananchi waliozungumza na gazeti hili akiwamo Timothy Mwaikera anasema kuwa wamechoka kusikia tetesi zisizokuwa na mwisho, hivyo wanaiomba Serikali kuingilia kati suala hilo na kutoa rasmi taarifa ili ukweli uweze kujulikana.

“Nadhani ni busara kwa serikali kufikiria jambo hili kwa mtizamo wa mbali, mali hizi zilizoachwa na Wajerumani zimeendelea kuleta gumzo kubwa miongoni mwa wananchi, lakini ufumbuzi wa jambo hili haukufanywa katika kipindi cha ukoloni wa Kiingereza hadi Tanzania ilipopata uhuru na hatimaye sasa Tanzania imetimiza miaka 50 ya uhuru,” anasema Mwaikera.

Anasema huu ni wakati mwafaka wa Tanzania kuanza kuzifuatilia mali zote zilizoachwa na Wajerumani si Kisiba tu na maeneo mengine ili ziweze kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa Watanzania wote na wala si kwa mtu binafsi kama ilivyo hivi sasa kwani wapo baadhi ya watu wachache wanataka kujinufaisha kwa  kuzivuna rasilimali hizo zinazosadikiwa kuwa zilichumwa katika ardhi ya Tanzania.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #5 2011-12-07 22:31
Acheni u[NENO BAYA] nyinyi. Kama kuna mali kwa nini msizichukue nyie muwe matajiri?

Mimi nadhani nyinyi ndio mmelogwa, mmekaa miaka yote hiyo na mnajua mali ipo msiichukue?
Quote
 
 
0 #4 2011-12-05 20:43
Nadhani turudi kwenye msemo.lisemwalo limo huwa tuna shindwa kutokana tuna kataa kujaribu ingawa japo tusiangalie mali tu,hebu serikali ichukulie kipaumbele jambo hili kwani inavyosemekana wakoloni walifukia vyombo vya kivita isije ikatokea maafa zaidi ya Gongo la mboto

Thanks
Quote
 
 
0 #3 2011-12-05 20:20
serikali itoe tamko kuhusu jambo ili,kuliacha hivi bila ya kauli yoyote ni kuwafanya wananchi waishi na imani za kishirikina,wat u awafanyi kazi wanaimani za kishirikina wana imani kuna nyoka wa vichwa 12,fuvu linaongea n.k
Quote
 
 
0 #2 2011-12-05 16:14
Sawa jameni hata kama hakuna mali ya kugawana, basi hata Hifadhi na Historia kama kivutio inatosha kutunzwa.
Quote
 
 
+1 #1 2011-12-05 15:31
Mwamunyange fuatilia mali hizo ingawa sasa ni out of date angalieni tunaweza kupata chochote
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner