MwanzoContactsEmail
Home Makala Jungukuu Amina: Nilifanyishwa ngono nikiwa na miaka 12, sasa saratani ya kizazi inanitesa
BOOKMARK THIS PAGE
Amina: Nilifanyishwa ngono nikiwa na miaka 12, sasa saratani ya kizazi inanitesa  Send to a friend
Friday, 27 January 2012 12:28

Na Florence Majani
KATIKA kitanda alicholala Amina Shabani amefunikwa na blanketi la simanzi, hofu ya mauti, majuto na maumivu makali ... yasiyostahimilika. Anajuta na mengi. Anakumbuka vingi, na kubwa zaidi … anateseka na maradhi ya saratani ya  shingo ya uzazi yaliyomsababishia uvimbe mkubwa katika sehemu zake za siri.

Maji yenye harufu humwagika kwa saa 24, hali inayomfanya Amina atumie  nepi maalum au ‘diapers’ ili kuzuia maji hayo yasilowanishe shuka.

Si hivyo tu, bali uvimbe huo mkubwa umeziunganisha sehemu ya haja kubwa na uke hali inayompa tabu zaidi kupata haja kubwa.

Uvimbe huo, ambao humfanya atembee kwa taabu, unamsababishia asiende haja ndogo  kama  wanawake wengine wafanyavyo, bali kwa mtindo ambao anadai, hauelezeki.

Na kubwa zaidi ni maumivu, ambayo anadai, yanafanana na mdudu anayetafuna sehemu za kiuno chake- huku wakati mwingine akihisi kisu kikali kikipita chini ya tumbo lake.

Amina anakesha akilia kwa maumivu, huku akitamka maneno haya kila mara:
“Mungu ni baba wa yatima na ni mume wa wajane, yeye ndiye ameamua niupate ugonjwa huu, na kama akipenda, basi nitapona.”

Akiwa na umri wa miaka 31 tu, mwanamke huyu  anasema amepitia machungu zaidi kuliko furaha.  Na hii ndiyo historia ya maisha yake;

Alizaliwa mkoani Mbeya, Wilaya ya Katumba. Awali aliishi na mama yake Rose Freddy pekee. Alipofikisha umri wa miaka minne, mama yake aliamua kumpeleka kwa baba yake.

Amina anasema, maisha nyumbani kwa baba yake, mzee Samweli Shabani hayakuwa mazuri sana.
“Pale kwa baba, familia ilikuwa kubwa, sikupelekwa shule wala hakukuwa na mtu wa kuniangalia kwa karibu ingawa nilikuwa bado mdogo,” anasema.

Anasema, alipoona hakuna dalili ya kupelekwa shule, aliamua kutoroka, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 10.
“Nilitoroka nyumbani. Nilipanda gari  kuelekea mjini kutoka hapo Nzovwa anapoishi baba, lakini nilipotea kwa kuwa sikuwa nikifahamu ninakoelekea, nia yangu ilikuwa kumtafuta mama tu,” anasema.

Katika kuzunguka zunguka mjini Mbeya, Amina alikutana na mwanamke mmoja, ambaye ni askari wa Usalama Barabarani(Traffic). Anasema, askari huyo aliamua kumsaidia, lakini kwa masharti ya kuwa, Amina atamsaidia kulea watoto wake wadogo.

“Nilipewa kazi ya kulea watoto wa yule mama, hakunipa ujira ingawa nilikula na kuvaa,” anasimulia.
Kama waswahili wasemavyo, “ng’ombe wa maskini hazai, akizaa basi huzaa dume, nalo likafa,” ndiyo ilivyokuwa kwa Amina.

Baada ya miaka miwili, traffic yule alifariki dunia, na ikambidi Amina kukimbilia kwa Joyce Mwamkinga, maarufu kama Mama Lusi.

Mama Lusi alikuwa ni rafiki wa askari yule na alikuwa akiishi katika kijiji cha Isanga.  Na hapo ndipo kilipo kiini cha machungu ya Amina.

Maisha nyumbani kwa mama Lusi
Amina alifika nyumbani kwa mama Lusi akiwa na umri wa miaka 12 tu. Maisha aliyoyakuta hapo, hayakuwa  kama alivyodhani.

Mama Lusi hakuwa na mume na wala hakuwa akifanya kazi yoyote, lakini alikuwa akitoka usiku na kurejea asubuhi.

 Siku moja, Mama Lusi alianzisha utaratibu mpya ndani ya nyumba hiyo. Utaratibu  ambao twaweza kusema ni wa kikatili, ambao pengine ndicho chanzo  cha mateso anayoyapata Amina leo hii katika kitanda hospitalini Ocean Road.

“Mama Lusi alituambia, ni lazima kila mmoja alale na mwanaume ili tupate pesa ya kuishi,”  Amina anasema huku akilia.

Mama huyo, hakufanya hivyo kwa Amina pekee, bali hata kwa watoto wake wawili wa kike, wa kuwazaa, Tuma na Lusi.

“Tuma alikuwa na miaka 14 Lusi alikuwa na miaka 16, na mimi 12, nilikuwa sisikii chochote kimapenzi, wala sijui kitendo cha ngono ni kitu gani, lakini nilifanyishwa kwa nguvu,” anasema Amina.

Msichana huyu mwenye mtoto mmoja anasema, katika umri huo, alifanya mapenzi na wanaume wenye umri tofauti tofauti.

“ilifikia mahala ikawa ni tabia, kwa hiyo nikazoea kuishi kwa kujiuza kimwili, “ anaeleza  zaidi.

 Mama yangu  baada ya kusikia kuwa nakaa kwa mama Lusi alikuja kutoka Katumba na kunichukua, lakini nilikuwa situlii, nakaa kidogo kwa mama , kisha natoroka narudi kwa Mama Lusi.

 Amina anasema, anasikitika kwa kuwa, Mama Lusi pamoja na watoto wake wote, hivi sasa wamefariki kwa ugonjwa wa UKIMWI.

Chanzo cha maradhi yake
Amina anabainisha kuwa, katika harakati za kufanya biashara ya ukahaba ndipo alipoyapata maradhi hayo.
Amina alikumbwa na ugonjwa wa zinaa ambao kwa kitaalamu unaitwa Human Papillomaviruses (HPVs) au sugu za sehemu za siri.

 Daktari wa Patholojia, wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili Innocent Mosha anasema, Ugonjwa huu huambukizwa kama magonjwa mengine ya zinaa yaani kwa njia ya kufanya ngono, na kwa asilimia kubwa husababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Amina anasema, kwa kumbukumbu zake, alianza kuugua ugonjwa wa zinaa mwaka 2000.  Wakati huo, alikuwa ndiyo ametoka kujifungua.

“Nilianza kuona vitu kama sugu(wart) katika sehemu zangu za siri, kadiri siku zilivyozidi kusonga ndivyo zilivyozidi kuongezeka ukubwa zikiambatana na maumivu,” anasema Amina.

 Juhudi za kwenda hospitali  mjini Mbeya hazikufua dafu na ilipofika mwaka 2000, Oktoba 5, alipewa rufaa ya  kufika Muhimbili.

Hapo  alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe huo zaidi ya mara tatu. Mwezi Desemba mwaka jana alipewa kibali cha kwenda katika taasisi ya saratani ya Ocean Road.

Alipofika Ocean Road ndipo  madaktari walipompasulia Amina kuwa ana saratani ya shingo ya uzazi kitaalamu(cervical cancer). Saratani hiyo ndiyo iliyomsababishia uvimbe mkubwa katika sehemu zake za siri.
 

Upendo wa kaka
Nazungumza na kaka yake Amina, Joseph Nyalile (31) ambaye  ametoka Mbeya ili kumuuguza dada yake kipenzi, ambaye  anadai wamecheza pamoja tangu wangali makinda.

“Dada yangu hana mama na mimi ndiyo ndugu yake” anasema Nyalile.

Nyalilie anasema, amekuwa akilala nje ya hospitali ya Ocean Road kwa mwezi mzima sasa kwa kuwa hana ndugu hapa jijini na ameishiwa fedha kabisa.

“Siku nyingine nakosa  hata fedha ya kula, nikikopa basi ni kwa ajili ya Amina,” anasema.
Lakini jambo linalomsikitisha zaidi Nyalilie, ni muonekano wa daktari  alipokuwa akisoma majibu ya vipimo vya Amina, hivi majuzi.

“Daktari aliposoma tu majibu ya vipimo, alitingisha kichwa, nilipomuuliza kwa nini, hakunijibu,” anasema Nyalile.
Amina anawaomba Watanzania wamuombee, mateso anayoyapata ni mazito na  haijui hatma ya maisha yake.
 Kwa kumsaidia Amina piga simu namba 0763205938/ 0768476777


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #1 2012-02-29 08:09
Hakika inasikitisha sana habari ya Amina. Na msemo wa majuto mjukuu unatimia hapa. Lakini, majuto haya hayakutokea kwa Amina kupenda. Kwanza umri wake ulikuwa mdogo sana alipoanza mambo ya mapenzi. Umri huo pia ulikuwa mdogo alipoamua kutoroka. Uwezo wake wa kufikiri na kufanya maamuzi magumu ulikuwa mdogo sana!
Uamuzi wa mama yake kumpeleka kwa baba yake, ndio mwanzo wa matatizo kwa Amina. Lakini KIINI cha tatizo, kipo kwa baba na mama yake, ambao hawakuishi pamoja kumlea Amina, kwa sababu ambazo hazijatajwa kwenye kisa hiki.
Hapa tujifunze kwamba,
* 1.Kuzaa watoto nje ya ndoa inaweza kuleta athari kubwa sana kwa mtoto siku za mbeleni.
* 2.Kuvunjika kwa ndoa kunaweza kleta athari kubwa sana kwa mtoto.
* 3.Tofauti kati ya wazazi, zinapaswa kushughulikiwa mapema, ili kurekebisha mambo kwa kumfikiria mtoto.
* 4.Kuwafanyisha ngono watoto, ni jambo baya mno, mno. Bora ukafagia barabara, ukachoma mahindi, au hata ukachimba mtaro, mtoto apate mahitaji muhimu, kutia ndani ELIMU, ili hatimaye awe salama.
* 5.Maadili yakivunjwa, madhara hayaepukiki. Tukimtii Mwenyezi Mungu kama anavyotuagiza juu ya ngono, tutakuwa salama.
* 6.Viongozi wa kidini waendelee kuhudumia watu kiroho kwa bidii, ustawi wa jamii waweke mikakati ya kupeleka elimu mpaka vijijini, juu ya malezi.
* 7.Viongozi kuanzia ngazi ya mjumbe wa nyumba kumi, Serikali za mtaa, n.k. wapite nyumba kwa nyumba kujua hali halisi za familia na kuzifuatilia. Ili panapohitajika msaada wa kiafya, kisheria na kiusalama waweze kuchukua hatua mapema.
* 8.Mtu/watu wakiona watoto walioko katika mazingira fulani magumu, hatarishi au yasiyoeleweka, watoe ushirikiano, kwa kumjulisha mjumbe au ofisi ya Ustawi wa Jamii, na ikiwezekana hata polisi. Ila wahakikishiwe USALAMA WAO na USIRI.
Japo inaweza kuwa vigumu [NENO BAYA]liza kabisa tatizo, lakini si bure, jitihada zitasaidia. Na iwekwe mikakati maalumu ya kudhibiti ongezeko la watoto wa mitaani. Mungu atabariki jitihada. Litengwe fungu maalumu na Serikali au wafadhili kwa ajili hiyo. Fungu ambalo litasimamiwa na idara kadhaa ili kuhakikisha halitumiwi kwa malengo tofauti.MUNGU TUBARIKI, TUHURUMIE, TUSAMEHE, TUONGOZE NA KUTUFUNDISHA. MSAIDIE PIA AMINA AISHI KWA MATUMAINI, NA HATA KAMA MAUTI YATAMFIKA, AKUTUMAINIE WEWE< ATUBU MAKOSA ALIYOSABABISHIW A, NA AWE TAYARI KWA AJILI YA UFALME WAKO. Sisi sote pia tujiandae kiroho, maana hata kama hatutapata kama yaliyompata Amina, lakini tunaweza kufa kwa sababu yoyote, kwa kuwa tumerithi dhambi ya Adamu, mshahara wa dhambi ni kifo. Lakini tumaini la uzima wa milele, liko kwa wote wanaojinyenyeke za mbele za Mungu.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner