MwanzoContactsEmail
Home Makala Jungukuu Umeme; ndoto ya wananchi Kagera iliyomtesa Waziri Ngeleja
BOOKMARK THIS PAGE
Umeme; ndoto ya wananchi Kagera iliyomtesa Waziri Ngeleja  Send to a friend
Friday, 27 January 2012 12:31

Na Phinias Bashaya
NISHATI ya umeme inachukuliwa na wengi kuwa nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo hasa maeneo ya vijijini. Kwa jumla, wananchi hawawezi kufungua milango ya maendeleo ikiwamo miradi midogo ya kujiongezea kipato kama hawana nishati hiyo.

Miongoni mwa adha kubwa kwa wananchi hao ni kutembea mwendo mrefu kutafuta huduma kama za kukoboa na kusaga nafaka huku mafundi wa fani mbalimbali wakishindwa kutumia ujuzi wao kikamilifu kujiletea maendeleo kutokana na vifaa vyao kutegemea umeme.

Baadhi ya wananchi vijijini Mkoani Kagera mzigo mkubwa  kwao ni kumiliki vitu kama simu za kiganjani kutokana na huduma za umeme kuwa mbali au kutokuwapo kwa nishati hiyo wakati huo wakilazimika kwenda na mabadiliko katika teknolojia ya mawasiliano.

Katika ziara yake mkoani humo wiki chache zilizopita, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja katika wilaya za Bukoba, Karagwe na Ngara mkoani humo ilithibitika dhahiri kilio cha wananchi juu ya mahitaji ya umeme.

Hata katika baadhi ya vijiji Ngeleja alipokea malalamiko ya kucheleweshwa kwa ahadi za kupatiwa nishati hiyo zinazorudiwa kila mara na wanasiasa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Awali, kabla ya kuanza kwa ziara katika wilaya ya Bukoba, Ngeleja alilazimika kufanya majadiliano na viongozi wa mkoa huo kuangalia jinsi ya kumaliza aibu kwa Watanzania kwenye mpaka wa Mutukula.

Tangu Uhuru hawajawahi kupata umeme ilihali umeme upo mita chache upande wa pili wa mpaka wa Uganda ambapo hulazimika kuvuka kufuata huduma ambazo zingepatikana kwao kama umeme ungekuwepo.

Hatima ya majadiliano hayo ilikuwa ni kutangaza neema kwa wakazi wa Mutukula wilayani Missenyi kuwa wizara itatoa zaidi ya bilioni moja zinazohitajika ili kupeleka umeme katika eneo hilo kabla ya kumalizika mwaka huu.
Kukosekana kwa umeme katika mpaka wa Mutukula kwa upande wa Tanzania kumechangia shughuli nyingi za biashara kuhamia upande wa pili wa mpaka,jambo ambalo pia linaikosesha serikali mapato.

Kilio cha umeme Karagwe
Kwa wakazi wa Wilaya ya Karagwe mahitaji ya umeme ni makubwa hasa kutokana na kasi ya kukua kwa shughuli za biashara katika maeneo mbalimbali ndani ya vijiji.

Kijiji cha Rwambaizi , Kata ya Kanoni wilayani humo ni miongoni mwa vijiji vingi ambavyo wakazi wake wamesubiri utekelezaji wa ahadi ya kupelekewa huduma ya umeme kwa muda mrefu kama walivyohaidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka mmoja uliopita.

Akiwa katika ofisi za CCM mjini Kayanga wilayani humo, Waziri Ngeleja alipewa taarifa ya chama kuwa ucheleweshwaji wa ahadi hiyo unaleta hofu ya kisiasa na kujenga hoja kwa wapinzani juu ya ahadi hewa za umeme.

Ziara ya Ngereja ilifufua matumaini ya wakazi wa Kata za Kanoni, Kituntu ikiwamo Kijiji cha Rwambaizi ambapo alimwagiza Meneja wa Tanesco wilayani humo, Oliva Mushumbusi kuomba milioni 250 zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo uliosimama tangu mwaka 2004.

Kama ilivyo takribani vijiji vyote vya wilaya ya Karagwe, pia kilio cha mahitaji ya umeme kilisikika kwa wananchi wa Ngara ambao mazingira yao yanaonyesha upatikanaji wa umeme unaweza kufungua njia nyingi za kujikwamu a kiuchumi.

Kuthibitisha kuwa suala la umeme ni kete muhimu kwa wanasiasa, Mbunge wa Jimbo hilo, Deogratias Ntukamazina aliwakumbusha wapigakura wa kijiji cha Rulenge kuwa kama alivyoahidi umeme na sasa alikuwa ameambatana na waziri mwenye dhamana hiyo.

Pamoja na kuwahakikishia umeme wananchi ,pia Ngeleja alisema miaka michache ijayo wilaya hiyo itakuwa na umeme wa ziada mara utakapoanza mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Rusumo.

Hata hivyo, anasema ziada ya umeme haitakuwa na maana kwa wananchi wa wilaya hiyo endapo haitatumika kuongeza uzalishaji na kuibua miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Anasema kwa kutumia Wakala wa Usambazaji wa Umeme  Vijijini(REA), maeneo mengi yatafikiwa na umeme na kuwa mwezi Machi  mwaka huu Serikali itatangaza awamu nyingine ya miradi itakayofadhiliwa kupitia wakala wa nishati vijijini.

Ngeleja na historia ya umeme
Waziri Ngeleja anasema mipango iliyopo na iliyoanza kutekelezwa itawezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha na hata kuwa na ziada ya kuuza nje ya nchi ifikapo mwaka 2015.

“Mipango imeanza kutekelezwa na tunalisema hili kwa wanaotaka na wasiotutakia mema,ifikapo mwaka 2015 tutakuwa na ziada ya umeme wa kuuza nje ya nchi,”alibainisha Ngeleja.

Anasema kwa kipindi hiki tunalazimika kuishi kwa matumaini hadi wakati huo ambapo wananchi watashuhudia matunda kamili yanayotokana na mipango thabiti ya serikali kuondokana kabisa na kero ya umeme.

Kwamba ni dhamira ya serikali kuondokana na utegemezi wa uzalishaji wa umeme kwa njia ya maji na badala yake kuwekeza zaidi katika umeme wa gesi,upepo na makaa ya mawe.

Anabainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kuiunganisha mikoa ya Kagera,Kigoma na mingine katika gridi ya umeme ya taifa ambapo wilaya ya Biharamulo kama zilivyo wilaya nyingine utawaku ni wakati wa kuondokana na uzalishaji wa umeme kwa kutegemea mitambo iendeshwayo kwa mafuta ya dizeli.

Akizungumzia mipango ya uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya Rusumo wilayani Ngara, Waziri Ngeleja anasema kuwa hatua za awali za mradi huo tayari zimeanza kwa kushirikiana na nchi za Rwanda na Burundi.

Anasema kukamilika kwa mradi huo ifikapo mwaka 2016 utaiwezesha Tanzania kupata megawati 30 kati ya tisini zitakazokuwa zinazalishwa katika maporomoko hayo ambapo kila nchi itapata mgao sawa.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner