
| Matamasha ya sanaa yalenge kutangaza utamaduni wa Mtanzania | Send to a friend |
| Friday, 03 February 2012 13:15 |
|
MAWASILIANO ya mwanadamu kwa namna tofauti yanategemea lugha, ambapo humsaidia katika kufikisha ujumbe ama kueleza hisia zake. Sote tunatambua kuwa lugha haifanikishi eneo la elimu pekee katika suala la kujiletea maendeleo, pia katika tasnia ya sanaa lugha imeweza kuwainua wasanii mbalimbali kwa kupitia uigizaji na kuimba na kuwafanya wafanikiwe kuwasilisha sanaa zao na maudhui waliyoyakusudia ili kuweza kuifikia jamii. Katika miaka ya hivi karibuni tangu kuimarishwa kwa Baraza la Sanaa la Taifa(Basata) ambao pia ni wadau katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili, kumekuwapo na matamasha mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kuratibiwa na Basata, huku matamasha hayo yakihusisha wasanii wa ndani na nje ya Tanzania. Sanaa ya uigizaji na muziki zimekuwa zikiwavuta watu, wengi ambao wengi wao ni rika la vijana wakiwamo wanafunzi. Matamasha hayo yapo yanayofanyika maeneo ya wazi na muda mwafaka, ambapo mwanafunzi anaweza kuhudhuria na kuburudika katika kile ambacho wahudhurishaji wameandaa. Hata hivyo sehemu kubwa ya maonyesho ama matamasha hayo yamekuwa yakihusisha lugha ya Kiswahili, hata katika matamasha yanayohusisha wasanii au washiriki wa nje kutokana na umuhimu wa mawasiliano katika kuwasiliana na kuweza kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa mashabiki bado lugha ya Kiswahili imekuwa ikipewa kipaumbele. Miongoni mwa matamasha ambayo yamekuwa kivutio ni yale ya Fiesta, Str8, Sauti za Busara pamoja na Swahili Fashion. Matamasha hayo yote kwa jumla yana nafasi ya kukuza na kueneza utamaduni wa Mtanzania kupitia lugha ya Kiswahili. Hii ni kutokana ukweli kwamba, maonyesho kama hayo licha ya kuonyeshwa moja kwa moja kutoka viwanjani, pia huwa yanarekodiwa huku wengine wakipeleka nakala za maonyesho hayo nje ya nchi kwenda kuonyesha ndugu jamaa, pamoja na kuweka katika mitandao mbalimbali ya kijamii. Nasema ni fursa nzuri kwa kikitangaza Kiswahili kwa kuwa maonyesho hayo yamekuwa yakipata wadhamini mbalimbali kutoka wadau wa maendeleo nchini hasa katika sanaa ya muziki na uigizaji ambapo ni fursa nzuri ya wageni wanaokuja kushiriki nao wakapata kujifunza utamaduni wetu wa lugha na kuelewa namna jamii yetu ilivyoweza kuyafikia maendeleo hayo kupitia lugha ya Kiswahili. Hivi karibuni tumesikia matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari kuwapo kwa tamasha la tisa linalofahamika kama Sauti za Busara litakalofanyika Zanzibar, eneo la Ngome Kongwe na kushirikisha vikundi mbalimbali vya sanaa pamoja na wasanii wakongwe wa hapa nchini. Tunaelezwa kwamba tamasha hilo linatoa fursa kwa wanamuziki wa ndani kujifunza kutoka kwa wanamuziki wa mataifa mbalimbali ya bara la Afrika wanaokuja kutumbuiza na linatambulisha muziki wa Afrika Mashariki kwa wageni. Tamasha hilo linaloshirikisha vikundi zaidi ya 31 vya ndani na nje ya nchi, wanamuziki wa ukanda huu Afrika watajumuika, huku wakiwa na shauku ya kila kikundi kuweza kuonyesha sanaa yake jinsi ilivyokuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, tangu kufanyika kwa tamasha kama hilo mwaka uliopita. Mafanikio ya kuendesha matamasha kama hayo yanaweza kuwa na tija iwapo, waandaaji kwa kushirikia na taasisi husika za ndani licha ya kutoa burudani na kujifunza mambo mbalimbali, wakaangalia pia namna ya kutangaza utamaduni wao wa lugha. Miongoni mwa vikundi hivyo vipo vyenye majina kama Swahili Culture Centre, ambapo vyote hivyo vina malengo yake na shauku ya kupata fursa ya kuonyesha ustadi na ufundi wao katika sanaa waliyobobea. Aidha hivi karibuni mwandaaji na mbunifu wa mavazi Mustafa Hasanali alifanya maonyesho ya mavazi nchini, ambapo imetokea kuwa la kipekee katika kuonyesha mitindo mbalimbali ya mavazi, huku washiriki wa tamasha hilo wapo wale wa ndani na wanaotoka nje ya mipaka ya tanzania hata mataifa kama vile Denmark, Marekani, Uingereza ambapo nao hutumia fursa hiyo ya kujitangaza katika soko la ushindani na jina la mashindano hayo yakifahamika kwa jina la Swahili Fashion. Mathalam waandaaji hao pia wanayo fursa nzuri ya kujibainisha katika kusaidia kuueneza utamaduni kupitia mavazi hata kuutambulisha ulimwenguni utamaduni wa lugha ya Kiswahili kwa namna ambavyo hivi sasa lugha hiyo imepiga hatua. Ipo haja kwa taasisi husika katika kusimamia matamasha kama hayo, kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani kutumia fursa hiyo inapojitokeza katika kuwahimiza waandaaji, kueleza namna gani wanaweza kusaidia katika kutangaza utamaduni wa Mtanzania kwa kupitia matamasha kama Sauti za Busara na Swahili Fashion, ambayo yamekuwa kivutio kwa watu wa mataifa mbalimbali. Ni hivi karibuni tumeona Kiswahili kupata fursa katika kituo cha televisheni cha M-net kwa kurusha filamu mbalimbali za Kiswahili na wamiliki wake kuwapa changamoto waandaaji na wasanii wa filamu hizo, kuongeza ufanisi katika viwango vya uandaaji wa sanaa zao ili kuwa katika viwango vya kimataifa. Wasanii kama kioo cha jamii tunatarajia wangekuwa mstari wa mbele hata katika matumizi ya lugha Kiswahili iliyo fasaha katika uandaaji na uwasilishaji wa sanaa zao kwa kuanzia huko Zanzibar ambako wasanii watakutana katika kuonyesha umahiri jukwaani katika sanaa zao. Kasumba hii iliyozoeleka ya kuchanganya lugha ya Kiswahili pia wasanii wanayo nafasi katika kuelimisha suala hilo. Wasanii wetu watambue kuwa watoto na vijana wapo nyuma yao kuyapokea maneno wanayoyaanzisha yasiyo na maana inayoeleweka kisha kuendelea kuyatumia katika maeneo mbalimbali, huku wanapotoka kwa kutozingatia matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili. Mwandishi ni Mhakiki wa Lugha wa gazeti hili. |














