MwanzoContactsEmail
Home Makala Jungukuu Vijana na Katiba Ijayo
BOOKMARK THIS PAGE
Vijana na Katiba Ijayo  Send to a friend
Friday, 03 February 2012 13:33

Kokuteta Mutembei
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba ushiriki wa vijana katika siasa bara la Afrika bado ni mdogo, na wakati mwingine ushiriki umeonekana kupungua, wachache hujiandikisha kupiga kura na katika hao, wachache hujitokeza.  

Wanashiriki katika kusikiliza kampeni za kisiasa lakini hawashiriki kuchagua viongozi.  Wakati mwingine wanashiriki katika maandamano, majukwaa ya kisiasa na fursa mbalimbali za kutoa maoni yao lakini ushiriki katika kufanya maamuzi ya kimsingi katika vyombo mbalimbali ili kuleta mabadiliko huwa ni kidogo.  

Katika kipindi hiki cha kujiandaa kuandika katiba ya nchi, vijana hawana budi kushiriki kikamilifu. Lakini ili washiriki, viongozi wana wajibu wa kutengeneza mazingira ya ushiriki wa vijana na zaidi ni kuhakikisha kwamba maoni yao yanathaminiwa na kupewa kipaombele stahiki.
 
Kwa bahati mbaya wengi wa viongozi walio katika nafasi ya kuwashirikisha vijana katika maamuzi mbalimbali hudharau mchango wa vijana na kuona kwamba vijana hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya demokrasia.  Mitazamo ya aina hii haina budi kubadilika na imefika wakati viongozi wakawajibika kwa kundi hiil la wananchi.  
 
Ni kwa kiasi gani vijana wanaandaliwa kushiriki kikamilifu katika kuchangia maoni katika Katiba? Hili ni swali la muhimu kujiuliza na kutafakari kwa maana maandalizi haya hayana budi kufanyika kabla ya wakati ili kuwaandaa vema kuchangia Katiba ya nchi yao.   

Kwa mfano, maandalizi haya yajidhihirishe katika kuimarisha mifumo ya ushiriki na utoaji maoni, ili vijana waliopo mashuleni, katika ajira na wale ambao wako mashambani au mitaani nao wapate fursa sawa katika kuchangia maoni katika katiba.

Serikali ina jukumu la kufanya kazi kwa karibu na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuhakikisha kwamba vijana wanapata taarifa ya kutosha kuhusu masuala mbalimbali ya kikatiba.  

Viongozi ambao wako katika madaraka na wenye nafasi nzuri ya kuwasiliana na vijana, kwa mfano wabunge, madiwani na viongozi katika ngazi za serikali za mitaa washirikishwe katika utekelezaji wa jukumu hili ili mawazo ya vijana kutoka pande mbalimbali za nchi yapate kupata fursa wa kutosha.

Kwa mfano, katika ngazi za mitaa na vijiji, watendaji ni muhimu kuitisha vikao na vijana, aidha kwa kupitia kamati, taasisi, vikundi vya kijamii au jamii yenyewe ili vijana wapewe habari za kutosha kuhusu ushiriki wao katika kuandaa katiba ya nchi. Ili zoezi hili lifanyike vizuri, Serikali izingatie uwezo wa viongozi kuweza kushirikisha vijana kikamilifu.
 
Mpaka sasa bado hatujajiandaa vizuri kwa ajili ya ushiriki wa vijana katika kutengeneza katiba ya nchi yao. Ipo haja ya kuimarisha mazingira, kujenga uhakika wa ushiriki wa vijana na kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato huu.

Harakati za kuwashirikisha vijana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu muktadha wao wa sasa na baadaye hazina budi kuanza mapema na masuala ya msingi yanayoibuka katika mijadala hii ni vema yakawekwa bayana ili yajadiliwe zaidi hadi kufikia makubaliano.   
 
Katika kushirikisha vijana ni muhimu kuzingatia haja za kielimu (taarifa) za vijana katika makundi mbalimbali, makundi haya yanaweza yakawa na mahitaji ya muhimu kuhusu taarifa wanazohitaji kuhusu katiba ya sasa na mwelekeo wa katiba ijayo.

 Taarifa hizi ni muhimu ziandaliwe, zisambazwe na zijadiliwe na vijana.  Namna moja ya kuhakikisha kwamba vijaa hawapotezi dira ya taifa na wanaendelea kuwa na matumaini, utashi na hamu ya maendeleo ya nchi, ni kuhakiksiha wanashirikiswa ipasavyo katika mchakato huu wa katiba.

 Sio tu wajibu wa viongozi kujenga mazingira stahiki ya ushiriki lakini wanasukumwa kufanya hivyo kutokana na idadi kubwa ya vijana Tanzania, hivyo kulazimika kutambua mchango wao

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner