MwanzoContactsEmail
Home Makala Jungukuu Kapunga waachwa njiapanda
BOOKMARK THIS PAGE
Kapunga waachwa njiapanda  Send to a friend
Friday, 03 February 2012 13:48

Na Daniel Mbegga
MAMIA ya wakazi wa Kapunga wameachwa njiapanda kwa miezi minne sasa baada ya barabara kwenda Mpunga Mmoja, ambako ndiko yaliko mashamba yao, kufungwa na Meneja Uzalishaji wa Kapunga Rice Project Limited, kampuni ya ubia inayoendesha shamba hilo.

Wakazi hao wa Kapunga, ambao wamekuwa wakitumia barabara zinazopita katikati ya shamba la mwekezaji kwa zaidi ya miaka 20, kwa kipindi kirefu walishindwa kuandaa mashamba yao kwa msimu huu wa kilimo kwani barabara pekee inayozunguka shamba hilo ina urefu wa kilometa 14.

Wakazi wanasema iwapo wanataka kwenda kweye mashamba yao inawapasa kupitia kwenye kijiji cha Site One.

Hata kama utaamka alfajiri, umbali huo ni mrefu kwa sababu utafika shambani ukiwa umechoka, anasema Shem Masharubu Nziku (80), mkazi wa Kapunga ambaye ameishi hapo kwa zaidi ya miaka 25.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kapunga, Ramadhan Nyoni, anasema juhudi zao za kumshawishi Meneja Mradi kufungua njia hizo ziligonga mwamba na kwamba pamoja na kumweleza Mkuu wa Wilaya ya Mbarali na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, viongozi hao walikaa kimya kwa muda mrefu kabla ya kufanya ziara hivi karibuni.

Anasema Mkuu wa Wilaya, Cosmas Kayombo, na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro, walifanya ziara mwezi uliopita na kuzungumza na pande zote mbili ili kurejesha amani, lakini alichofanya mwekezaji mpaka sasa ni kuruhusu pikipiki na waendao kwa miguu tu kupita, lakini akigoma kabisa kuruhusu magari.

Kapunga ina wakazi zaidi ya 2,000, lakini kuna watu zaidi ya 3,000 kutoka Chimala na kwingineko ambao wana mashamba katika eneo la moja la Mpunga na ambao wameathirika na hatua ya kufunga barabara. Uamuzi wa kuzifungua umechelewa na kwa maana nyingine hata mavuno hayatakuwa ya kuridhisha kwa sababu wengi wameshindwa kulima, akaongeza.

Akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake mwezi Agosti 2011, Sergei Bekker, meneja uzalishaji wa KRPL alisema alikuwa anazifunga njia zote zinazopita shambani kwake kwa sababu wakazi wa Kapunga walikuwa wanaiba mpunga wake.

Baadhi ya wanakijiji wanaiba mpunga wangu kila wanapopita kwenye barabara hizi, kwa hiyo tunafunga barabara. Waache wapite huko Site One, alisema.

Bekker alisema wizi ni changamoto kubwa tangu Export Trading Company ilipochukua shamba hilo kwani baadhi ya wafanyakazi wao wamekuwa wakiiba dizeli, betri na vipuri, na kuviuza katika maeneo ya jirani.

Alipoulizwa ni kwa nini ameamua kufunga njia zinazopita shambani kwake mwaka huu, Bekker alisema ni kwa sababu uhusiano baina ya kampuni yake na wanakijiji umetetereka.

Mwekezaji huyo alisema kwamba kijiji cha Kapunga kimo ndani ya eneo lake kwa mujibu wa mipaka na nyaraka za mkataba.

Tulilinunua shamba. Kama kulikuwa na makosa basi wa kulaumiwa ni serikali. Serikali iko wapi sasa? Tangu tulipolinunua shamba hili wametuacha tupiganie wenyewe haki zetu. Kwa upande mwingine wanakijiji, kama wamekuwa wakiishi pale kwa miaka mingi, wana haki.

Lakini ni haki kutulaumu sisi? Serikali ndiyo iliyouza eneo hili. Hivi ni kweli haikujua kwamba hapa kulikuwa na watu wanaoishi kijiji cha Kapunga?” alihoji Bekker.

Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, aliitaka serikali kulishughulikia suala hilo haraka kwani linakwamisha maendeleo ya eneo hilo.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Prof. Jumanne Maghembe, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka waliahidi kuja kuangalia hali halisi ya mgogoro, alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Cosmas Kayombo, alisema anautambua mgogoro huo wa Kapunga, lakini akaongeza kwamba suala hilo linashughulikiwa na uongozi wa mkoa na wizara husika.

Mgogoro ule unashughulikiwa lakini siwezi kusema utatatuliwa lini. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Wizara husika zinashughulikia. Tuwe wavumilivu tu wakati serikali ikilishughulikia, alisema.

Kayombo alisema kwamba tatizo lililopo Kapunga ni la kiufundi, lakini kuna haja ya kurejesha amani na uhusiano mwema kati ya mwekezaji na wananchi wa eneo hilo, jambo ambalo wanalifanya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mstaafu, John Mwakipesile, alisema katika mahojiano maalum Agosti 2011 kwamba hakukuwa na mgogoro wowote Kapunga, na kwamba wananchi ndio waliovamia eneo la Mradi wa NAFCO na kuweka makazi ili baadaye wadai kwamba wamekuwepo pale kwa miaka mingi.

Mwakipesile, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shamba la NAFCO wakati linauzwa, hakuweza kueleza eneo halisi la Shamba la Kapunga lililokuwa la NAFCO, akisema hilo lilikuwa jukumu la PSRC.
Wananchi walivamia eneo la Mradi wa NAFCO miaka mingi na kuanza kujenga nyumba zao. Kuhusu eneo la mradi, nadhani PSRC ndio wanaofahamu, mimi sielewi chochote, alikaririwa akisema wakati huo.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Eng. Christopher Chiza, alikiri kuufahamu mgogoro huo na kwamba ofisi yake inalifanyia kazi.
“Nilitembelea eneo hilo Agosti Mosi 2011. Wananchi walieleza malalamiko yao ambayo ni ya msingi.

Nakuhakikishia kwamba serkali inajitahidi kusuluhisha mgogoro huo, alisema.
Wakati akihitimisha makadirio ya bajeti ya wizara yake mwezi Agosti 2011, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, Prof Anna Tibaijuka alisema serikali yake ingetembelea maeneo yote yenye mgogoro na kuona njia sahihi za kuitatua.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner