|
Hadija Jumanne UTAPIAMLO ni tatizo sugu hapa nchini, inaaminiwa kuwa TANZANIA ni nchi ya tatu iliyoathirika vibaya na utapiamlo Barani Afrika na ni nchi ya kumi duniani kwa kuathirika na tatizo hilo, na hiyo ni changamoto kubwa kwa taifa. Si hivyo tu, bali utapiamlo umepoteza fursa za kiuchumi hasa katika uwekezaji katika sekta ya elimu kwani umezaa matokeo duni kutokana na kuchangia asilimia 56 ya vifo vya utotoni hapa nchini na ukosefu wa akili kwa asilimia 13.
Kama hiyo haitoshi kila mwaka huenda Tanzania ikapoteza Sh 700 bilioni kutokana na Utapiamlo na kwamba tatizo hilo limesababisha asilimia 2.6 ya pato la taifa hupotea kutokana na tatizo hilo la Utapiamlo. Utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Uwazi-Twaweza kwa kushirikiana na Asasi za Policy Forum na Sikika umebeba jina la Je, Tanzania inaweza kupuuzia vifo vya watoto 43,000 na upotevu wa sh bilioni 700 kila mwaka’?
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Sikika, Irene Kiria, anasema mtoto mwenye utapiamlo akiugua ugonjwa wa kuharisha, malaria au homa ya mapafu, uwezekano wa kupoteza maisha ni mkubwa.
Wanakufa kwa sababu lishe na vyakula vyao havina virutubisho vya msingi vinavyohitajika kujenga mfumo imara wa kinga za mwili na kuwafanya wawe na afya, anaongeza Irenei.
Mbali na idadi hiyo jumla watoto 600,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano hapa nchini wamefariki dunia kutokana na utapiamlo uliosababishwa na lishe duni katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na kwamba ugonjwa huo ni moja kati ya sababu kubwa ya magonjwa na vifo vya watoto na wajawazito hapa nchini. Tathmini ya Afya na Demografia ya Tanzania iliyotolewa mwaka jana imeonesha kuwa watoto watano katika kila 100 hufa kabla ya kutimiza mwaka mmoja na watoto wanane kati ya 100 hufa kabla ya kutimiza miaka mitano. Sanjari na hilo Utapiamlo ni chanzo kikubwa cha vifo na ulemavu ambapo kila sekunde sita, mtoto hufa kwa njaa na matatizo yanayoambatana na njaa.
Kadhalika watoto wanne kati ya 10 wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa kwa sababu ya Utapiamlo sugu huku watoto sita kati ya kumi wenye umri chini ya miaka mitano wana upungufu wa damu. Hata wajawazito nao huathiriwa na utapiamlo, watano kati ya 10 wana upungufu wa damu na ni asilimia nne tu ya wanawake hutumia dozi ya madini ya chuma na foliki kwa kiwango kinachopendekezwa cha vidonge 90 wakati wanapokuwa na ujauzito.
Meneja wa Ushirika wa Lishe kutoka shirika la Kimataifa la Save Children Tanzania Joseph Mugyabuso, anasema Wanawake watatu kati ya 10 hutumia kiwango cha dozi ya vitamin A kilichopendekezwa kwa ajili ya kuwasaidia kujikinga wao na watoto wao dhidi ya magonjwa mara baada ya kujifungua.
Meneja huyo anasema tatizo la njaa na utapiamlo barani Afrika yamekuwa ni miongoni mwa mambo yaliyoenea kwa kasi barani Afrika ambapo watu wapatao milioni 240 wana tatizo la lishe duni, huku watoto 50 milioni barani Afrika wanatatizo la Utapiamlo sugu.
Utapiamlo huchangia zaidi ya asilimia 60 ya vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na asilimia 50 ya wajawazito kila mwaka, huku maeneo mengine ikiwa ni zaidi ya viwango hivyo,alisema Mugyabuso.
Anasema kwa sasa viwango bado vipo juu sana na havibadiliki ambapo asilimia 41 ya watoto bado hawapati chumvi iliyotiwa madini joto ya kutosha jambo ambalo linaongeza hatari ya watoto hao kuwa na matatizo ya akili.
Hata hiyo kwa viwango vilivyopo, UNICEF inakadiria kwamba Tanzania huenda isifikie lengo la Milenia namba moja la kupunguza viwango vya mwaka 1990 vya watoto wenye uzito pungufu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015.
Kwa mujibu wa UNICEF watoto na akina mama wengi maeneo ya vijijini wanaathirika zaidi kuliko maeneo ya mijini na hiyo inasababishwa na ulaji duni wa kutopata chakula cha kutosha na chenye virutubisho vya kutosheleza mahitaji ya mwili.
Mugyabuso anasema utapiamlo ulipungua kiasi kidogo tu kati ya vipindi vya tafiti zilizofanyika mwaka 2004 na 2005 na mwaka 2010 kwa silimia tatu. Anasema tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa watoto wadogo lilipungua kwa asilimia 18 ukilinganisha na miaka mitano iliyopita. Lakini alitaja sababu nyingine zinazosababisha hilo ni magonjwa na lishe duni. Anasema sababu zilizo za msingi zaidi ni pamoja na umasikini, ujinga na mila na desturi potofu katika jamii. Anasema ajenda ya maendeleo ya ulimwengu na juhudi za kukuza wigo wa hali ya lishe, kwa mwaka jana suala la kupambana na utapiamlo nchini limeanza kujitokeza kwa nguvu zaidi katika agenda ya maendeleo.
Kutokana na unyeti huo kila Oktoba 30 ya kila mwaka , nchi mbali mbali huazimisha siku ya chakula na lishe licha ya nchi hizo kukabiliwa na changamoto Anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizomo katika harakati za ulimwengu za Kukuza Lishe na kwamba Kuna hatua nyingi zimechukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kila wizara kuwa na kipengele cha bajeti kuhusu kukuza lishe kuanzia mwaka 2012.
Hata hivyo Uwazi-Twaweza, Asasi za Policy Forum na Sikika, kwa pamoja wanasema vifo vya utapiamlo vinaweza kuepukika kwa jitihada na kujituma kwa mamlaka za lishe. Aidha ilielezwa kuwa zipo njia ambazo zinaweza kupambana na utapiamlo ikiwa ni pamoja na kuanzisha urutubishaji vyakula na unyonyeshaji kikamilifu kwa watoto maziwa ya mama.
Hata hivyo Tanzania inafanya vibaya, kwani ni asilimia 13.5 tu ya watoto wachanga ndio wanaonyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi minne hadi miezi mitano wanapozaliwa, wakati kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani watoto wanapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita. Kama Tanzania ingeanzisha urutubishaji unga na mafuta ya kupikia, vifo 6,700 vya watoto vingeepukika kila mwaka na kuleta faida ya Sh153 bilioni kwa mwaka.
|
Comments