
| Vijana:Nguvukazi ya kiuchumi iliyosahaulika | Send to a friend |
| Thursday, 02 February 2012 08:37 |
|
NYUMA ya Kituo cha Polisi Msimbazi jijini Dar es Salaam gari za doria za polisi zinawakusanya vijana wanaokamatwa toka katika vichochoro, vibaraza na majumba mabovu yaliyopo katika maeneo mbalimbali katika kata tano za Kariakoo.Shughuli hiyo ambayo imeanza toka mapema alfajiri hadi kufika kunako saa tatu asubuhi zaidi ya vijana 400 wanatiwa mbaroni katika operesheni hiyo maalum ya kusafisha kata za Kariakoo ambazo zinatajwa kushamiri matukio ya uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na aina nyingine za wizi. Vijana hao baada ya kuandikishwa maelezo yao wanaandaliwa kwa ajili ya kufikisha mahakamani ambako wanaweza kufunguliwa mashtaka ya uzembe na uzururaji, kosa ambalo adhabu yake ni faini isiyozidi Sh10,000 au kifungo cha miezi sita. Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Kariakoo, Renata Mzinga anasema operesheni hiyo inafanyika kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu vya wizi wa mifukoni, ukabaji, wizi wa vifaa vya magari na ujambazi hasa dhidi ya raia wa kichina wanaofanyabiashara eneo hilo. Vijana hao ni sehemu ya maelfu ya wengine nchi nzima ambao hawana shughuli za kueleweka na wamekuwa wakikimbilia miji mikubwa wakitarajia kupata ustawi lakini wakati mwingine wamejikuta wakijitumbukiza katika vitendo vya uhalifu. Tanzania ambayo inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu 43 milioni kulingana na sensa ya Idadi ya Watu ya Mwaka ya 2002, asilimia 35 ya hao ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 na ni asilimia 60 ya nguvukazi ya Taifa. Hata hivyo nguvukazi hiyo kwa mujibu wa sera ya taifa ya vijana asilimia 60 kati yao hawana kazi maalum na ndiwo wanajiingiza katika wizi, ujambazi, uvutaji wa bangi, uzururaji, utumiaji wa dawa za kulevya na ukahaba na kibaya zaidi baadhi yao wanaendelea kuwa tegemezi kwa wazazi wao. Sera ya vijana ya taifa inabainisha kila mwaka vijana wanaohitimu elimu ya msingi ni zaidi ya 800,000 kwa mwaka wakati wa sekondari ni zaidi 300,000 na wahitimu kutoka vya kada mbalimbali wako karibu 400,000. Vijana hao wanaingia katika soko la ajira ambalo limejaa pomoni. Kutokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa ambapo kunahitajika watendaji wachache na hivyo kuongeza ugumu wa vijana kupata kazi. Aidha hata mipango mbalimbali ya kiuchumi ukiwemo wa kilimo kwanza haijatoa nafasi za ajira za kutosha kwa vijana. Ramadhan Ngoyo, mchuuzi wa vitu mbalimbali eneo la Kariakoo anasema amekuja jijini Dar es Salaam kutafuta maisha kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ambayo inawakabili kijijini kwao mkoani Kigoma. “Huko vijijini kwetu hali si nzuri, maisha magumu kila kijana anatoka, kuja mjini” anasema na kuongeza kuwa hata hicho kilimo kwanza kwao ni hadithi isiyoeleweka kwani kinaonekana ni kwa ajili ya wakulima wakubwa. Anasema wakulima hao wakubwa ndio ambao wanapewa nafasi ya kukopa matrekta, power tiller na vifaa vingine lakini si kwa mkulima wa jembe la mkono kama yeye. “Vijana wengi vijijini ambao wamebahatika kupata mitaji hivi sasa ni wachuuzi wa vyombo vya plastiki, nguo za mitumba na vitu vingine katika magulio yanayofanyika kwa nyakati tofauti katika vijiji mbalimbali” anasema Ngoyo. Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwlaimu anakiri kundi la vijana kusahaulika hali ambayo inawafanya baadhi kuingia katika vitendo viovu badala ya kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi. Anaitaka jamii kusaidia juhuidi za serikali katika kuhakikisha kuwa kundi hilo kubwa linatumika katika kazi za uzalishaji mali kwa faida ya nchi kwa jumla. Mkurugenzi wa taasisi ya kiraia ya Ubalozi wa Vijana Tanzania, Charles Mgendi anasisitiza kuwa sera zote za uchumi zimewatenga vijana na hakuna mkakati wa kulishirikisha jeshi hili katikam uejnzi wa uchumi. Anasema vijana ambao ndio nguvukazi ya taifa lolote duniani wanazidi kuhamia katika miji mikubwa ili kufanya uchuuzi wa vitu vidogovidogo kama kahawa, maji ya kunywa,tai au jozi moja au mbili za viatu. “ Vijana hawana dira kabisa, haiingi akilini kijana mwenye nguvu wa kati ya miaka 20 na 35 anazunguka kutwa nzima na shati mbili, tai au hata jozi moja ya kiatu cha mtumba kuwa naye anachangia uchumi? Hapana tunajidanganya. Mgendi anasema machafuko na ghasia zinazotokea katika nchi za Afrika ya Kaskazini na hata Nigeria inatoka na kundi la vijana kutokuwa na ajira za kueleweka. Matukio machache hapa Tanzania ya mapambano kati ya polisi, mgambo na wamachinga huko Mbeya, Mwanza, Dar es salaam na katika miji minginine mikubwa ni matokeo ya ya kundi la vijana kutaka kupewa haki ya kufanya biashara kwa kuwa hawana kazi rasmi. Vijana wanatakiwa kuwekewa mikakati na sera maridhawa zitakazosaidia kupunguza ukosefu wa ajira nchini. Kwa sasa sina hakika kama kuna jitihada hizo. |














