MwanzoContactsEmail
Home Makala Uchumi Saohill Industries; Kiwanda cha malighafi za misitu kinachosaidia kukuza uchumi wa Mufindi
BOOKMARK THIS PAGE
Saohill Industries; Kiwanda cha malighafi za misitu kinachosaidia kukuza uchumi wa Mufindi  Send to a friend
Thursday, 02 February 2012 08:40

Na Tumaini Msowoya, IUCo
WILAYA ya Mufindi miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Iringa ambazo, uchumi wake unakua kwa kasi na hivyo kuwa moja ya wilaya zinazochangia kiwango kikubwa cha pato la nchi. Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2008 wilaya ilichangia asilimia 26.7 ya pato la taifa.

Hata hivyi mafanikio ya kiuchumi yanayoonekana katika wilaya ya Mufindi hayakuja kwa bahati mbaya au kwa kubahatisha bali kumetokana na uwekezaji mkubwa katika sekta za misitu na mazao yake pamoja na kilimo cha mazao ya biashara ya chai, pareto na chakula pia.

Kutokana na uwekezaji huo, pato la wastani la mwananchi wa wilaya ya Mufindi limepanda kutoka Sh924,953 mwaka 2006 hadi Sh1.2 millioni mwaka 2008 na kwamba kiwango cha pato kinaendelea kuongezeka. Aidha uwekezaji huo umefungua ajira kwa wananchi wa huko pamoja na watanzania wengine kwa ujumla.

Wakati viwanda katika mikoa mingi nchini vimekufa, Mufindi ina viwanda kadhaa tena vikubwa vikiwemo vya mazao ya misitu, viwanda vya kusindika chain a kiwanda cha kuzidua pareto. Hivi vyote licha ya kufungua ajira pia cvinaongeza thamani ya mazao na hivyo kuing’arisha zaidi wilaya hiyo ambayo pia inasitawisha mazao mengine mengi.

 Iringa kwa mwaka 2006-2008, Wilaya ya Mufindi inachangia asilimia 26.7 ya pato la taifa ikiwa ndiyo wilaya ya kwanza kwa Mkoa wa Iringa wakati wilaya ya Mwisho ambayo ni Kilolo ikichangia asilimia 4.8.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu anasifu uwekezaji katika wilaya yake na anaitaja kampuni ya Green Resources Limited (GRL) inayomiliki kiwanda cha mazao ya misitu cha Sao Hill Industries ambayo pia inajishughulisha na upandaji wa miti kuwa ni miongoni mwa kampuni zinazochangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Mufindi. Kampuni hii pamoja na kutengeneza mbao  pia inazalisha nguzo za umeme ambazo nyingi zinatumiwa na Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO.

Kalalu amesifu GRL wakati wa uzinduzi wa mtambo maalum na wa aina yake yake Tanzania wa kukaushia mbao ikiwa ni sehemu ya mkakati wa uwekezaji wa kampuni hiyo. Mtambo huo utaifanya Tanzania kuuza mbao katika soko la kimataifa na pia kuviwezesha viwanda vya ndani kutumia mbao hizo kutengenezea samani zenye ubora wa hali ya juu. Mtambo utakomesha uingizaji wa samani kutoka nje.

Mtambo huo una lenga kufungua soko la mbao nje ya nchi pamoja na kuvipatia viwanda vya kutengeneza samani mbao bora zaidi kwa ajili ya kazi zao jambo ambalo litaiwezesha Tanzania kutengeneza samani za viwango vya hali ya juu kuliko hata hizo zinazoi9ngizwa nchini kwa sasa kutoka nje.

Mkurugenzi mkuu wa GRL kanda ya Afrika, Mads Aspren anasema uwekezaji wa mtambo huo umefabyika baada ya kubaini kuwa mbao za Tanzania zinashindwa kupenya kwenye soko la nje kutokana na kutokuwa na ubora unaotakiwa. Anasiitiza kuwa  “kama mbao inayovunwa itakaushwa kitaalamu na mtambo huu inaweza kuingia kwenye soko la kimataifa na kuhimili ushindani, tofauti na mbao zinazokaushwa kienyeji”.

Aspren, anasisitiza kuwa uingizaji wa samani kutoka nje kwa madai ya ubora utakwisha kwani viwanda vya samani vya ndani sasa vitapata malighafi bora zaidi. Kwa sasa kiwango kikubwa cha mbao za ndani zinatumika zaidi kwa ujenzi kuliko kutengenezea samanai. Amebainisha pamoja na kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya misitu lakini haifaidika vya kutosha kutokana na mazao ya misitu.

Mtambo huo, utaweza kuzalisha mbao bora zilizokaushwa ipasavyo zitakazo fanikisha kutengeneza fenicha za kisasa na bidhaa nyingine hivyo, kupunguza matumizi ya fenicha zinazoingizwa toka nje.

Mkurugenzi wa GRL, ambaye kampuni yake pia imewekeza katika nchi za   kadhaa barani Afrika ikiwemo Sudani kusini, Uganda na Msumbiji anasema mtambo huo una uwezo wa kukausha meta za ujazo 30,000 za  mbao kwa mwaka.Anasema kuwa uwekezaji kwa Tanzania, ulianza miaka mitatu iliyopita huku Mufindi ikiwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za misitu kwa Afrika Mashariki.

Anadai kuwa, kampuni hiyo haitakuwa ikizalisha fenicha ila itahakikisha inazalisha malighafi za kisasa ambazo zitaisaidia sekta ya ufundi kutengeneza bidhaa ambazo zinaweza kushindana kwenye soko la Afrika mashariki na dunia kwa ujumla.

 Hata hivyo fedha zilizotumika kujenga mtambo huo, ni mkopo toka mfuko wa Norload wa nchini Norway. Mkurugenzi mkuu wa Norfund, Kjell Roland anasema ni jukumu la makampuni, kubuni miradi ya kisasa na kuomba fedha toka kwao, ili waweze kusaidiana katika mapambano dhidi ya umaskini.

Ajira kiwandani hapo!
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha Sao Hill wanakiri kiwanda kimesaidia kupunguza tatizo la ajira.
 “Umaskini umepungua si kwa wafanyakazi peke yetu, bali hata kwa familia nzima. Kiwandani kimeajiri watu 800 ambao wameongeza mzunguko wa pesa kwa kutumia huduma kama za chakula na chai kutoka kwa mama ntilie,” anasema John Alex mmoja wa wafanyakazi.

Upandaji miti!
GRL imepanda zaidi ya hekta 14,660 za miti ya mbao toka mwaka 2005 hadi sasa kwa ajili ya kulisha kiwanda chake.Meneja wa mradi wa kupanda miti wa GRL Alon Raiza, anasifu ushirikiano ambao kampuni inapata kutoka kwa wananchi na vijiji vinavyozunguka mashamba ya miti ikiwa ni pamoja na kutoa ardhi kwa ajili ya kuanzisha vitaklu vya miche na mashamba. Anakitaja kijiji cha Idete pekee yake kwa kutoa hekta 11,660.

Aidha mradi wa upandaji pia umekuwa unatoa ajira kwa wanavijiji kati ya 250 na 450 katika kila msimu wa kupanda miche. Kampuni pia inachangia kuboresha huduma za jamii ikiwa ni pamoja na kujenga madarasa na ujenzi wa zahanati.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner