|
NA Charles Kayoka Nilipokuwa ufukweni mwa bahari mbele ya mji wa Mikindani, Mtwara niliona kundi la vijana wakiyapiga maji kwa mateke na vijana wengine wamesimama kulia na kushoto mwa hao vijana wapiga mateke wakishikilia nyavu. Walichokuwa wakifanya hao wapiga mateke maji ni kuwafukuzia dagaa na samaki kwenye nyavu ili wanase.
Niliwasubiri hapo hadi walipokamilisha kazi na kuwatoa samaki kutoka kwenye nyavu. Walikuwa wamejaa kwenye mfuko mdogo wa plastiki na walipowekwa kwenye sinia hawakuweza kufikia hata robo ya ujazo.
“Hao samaki ni Sh9,000 kwa bei ya jumla,” aliniambia mmoja wa vijana hao wavuvi. Niliwauliza walianza kazi saa ngapi, wakasema waliwahi mapema sana asubuhi na kuutandaza wavu wao. Imewachukua kama saa nne kuusubiri unase samaki na baadaye kuuvuta kwa mtindo wa kokoro. Lakini hata pale palipowkwa nyavu palikuwa na maji machache kiasi kwamba huwezi kutegemea kupata samaki wengi na wakubwa. Uvuvi wa kuwafukuzia samaki kwenye nyavu kwa mateke sio kwamba tu ni wa zamani, bali hauna tija ya kutosha. Mvuvi hutumia nguvu nyingi na muda mwingi kwa kupata kipato kidogo. Kwa idadi hiyo ya samaki, unajiuliza kama watarudisha gharama ya muda, vifaa vilivyoharibika vya uvuvi, na nguvu walizotumia. Huu sio uvuvi endevelu kwao na kwa taifa.
Ufukweni kulikuwa na akina mama waliokuwa wakisubiri samaki kutoka kwa wavuvi hao ili wapate kitoweo na samaki wa biashara. Wavuvi wote walikuwa wamerudi na bei ya samaki ilikuwa imepaa kwa siku hiyo kwani hapakuwa na samaki wengi. Nilimuona mwanaume mmoja mtu mzima ndiye pekee aliyekuwa na beseni lililojaa samaki.
“Sikupata samaki leo,”alinieleza na kuongeza, “wavuvi wamerudi na samaki wachache na hivyo wenzetu wenye mitaji mikubwa ndio wamefanikiwa kuwanunua, sisi wengine tumekosa tena hadi kesho.”
Mwanaume huyon alisema aliwanunua samaki wote kwa Sh100,000 kiasi ambacho wafanyabiashara wenye mitaji midogo, wengi wao wakiwa wanawake walirudi mikono mitupu. “Wanawake bwana mitaji yao midogo sana, wengi huishi mitaji ya Sh40,000 au Sh50,000, na biashara yao huwa kwa ajili ya kujikimu, “ alisema Bi Somoe Abdallah ambaye aliungwa mkono na mmoja wa wavuvi aliyejitaja tu kwa jina la Ustadhi Abdul. Nyavu zenyewe zinazotumika kwa kweli ni chakavu, na baadhi hutumia vyandarua, na mitumbwi inayotumiwa ni ngarawa, na sio ile inayotumia mashine. Mvuvi huyu alisema kuwa tatizo kubwa linalowapata wavuvi kuwa na mitaji midogo ambayo inawafanya kushindwa kupata vifaa bora na vya kisasa vya uvuvi.
“Hapa Mikindani au hata Mtwara hakuna duka la zana za uvuvi. Ukitaka kuvipata uende Dar-es-Salaam, maana hata Lindi sina uhakika kama utavipata,” aliniambia. Lakini anasema wavuvi wengi kwa kukosa mtaji wa kutosha kununulia nyavu na zana zingine huwa ni mtihani mkubwa. Wanahitaji kama Sh1,500,000 kama mtaji wa kununulia nyavu. Lakini hiyo bado haitoshi kwa sababu ngarawa wanazozitumia ni duni, za kusukuma kwa makasia na hivyo sio rahisi kufika kwenye maji marefu.
“Ninakwambia hata kuvuka pale mlango bahari wa PembaMnazi hatuwezi kwa ngarawa hizi unazoziona hapa, iwe kufika kule kwenye bahari kuu. Ndio maana unatuona tunagaragara hapa karibu na ufukwe tu, “ alieleza.
Mji wa Mikindani unapakana na ufukwe mkubwa wa bahari ambao unaweza kuwapatia wananchi hawa ajira ya uhakika kama uwekezaji katika sekta ya uvuvi ungekuwa mkubwa na makini zaidi. Lakini hatuoni kama jambo hili linafikiriwa, kwani tungetegemea kuwa kwa sababu hawa wananchi wanapakana na bahari juhudi kubwa za watunga sera na wasimamizi wa miradi ya maendeleo kitaifa na kimkoa, zingekuwa kuwahimiza kuzitumia rasilimali zipatikazo huko kwa ajili ya kujikimu na kujiendeleza.
Serikali ingeweza kuhimiza wafanyabiashara kuwekeza katika sekta hii, au hata kujenga mfumo wa kusaidia kupatikana kwa zana za uvuvi ili hawa wavuvi wadogo wadogo waweze kujikwamua. Tunashauri hivi kwa sababu mikoa hii ya kusini ina rasilimali nyingi mbali na kilimo, lakini rasilimali hizo, na hasa hizi za baharini, zinahitaji mitaji mikubwa ili kuweza kuzivuna kwa uhakika.
Lakini licha ya kuwa na kampeni ya kilimo kwanza kasoro unayoweza kuiona ni kuwa kampeni hiyo inawafikiria zaidi wakulima na sio wavuvi na wafugaji. Kama kilimo kinahusisha na uvuvi pia, na kwa sababu kuna kundi kubwa la wananchi wanaoweza kujikimu na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uvuvi, basi ingekuwa jambo jema kama Kilimo Kwanza kuhusisha kila sekta ya kilimo kwa uzito uleule.
Lakini la muhimu ni kuwa unapoona vijana wengi wanajaribu kujituma kwa kutaka kujiingiza katika ajira binafsi kama hii ya uvuvi, ni vyema basi serikali ikawaunga mkono kwa kuwekeza katika miundo mbinu husika.
This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
, 0766959349
|