|
Fidelis Butahe NOVEMBA 29 mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alisaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 na hivyo kuifanya kuwa sheria. Hatua hiyo ya kutia saini Muswada huo ilikamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali katika kikao kilichopita cha Bunge. Kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka 2010. Pamoja na kutiwa saini hiyo bado serikali iliendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau, vyama vya siasa na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo. Baada ya watu wa kada mbalimbali kuiponda sheria hiyo, hatimaye serikali ilisikia kilio hicho na kuandaa rasimu ya muswada unaopendekeza marekebisho ya katiba hiyo.
Pamoja hatua hiyo Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba wakati akitoa maoni juu ya muswada wa marekebisho katika sheria ya mabadiliko ya katiba namba 8 ya mwaka 2011 anasema rasimu hiyo imelenga kurekebisha vifungu viwili tu wakati sheria hiyo ina mapungufu katika vifungu zaidi ya kumi.
Anasema muswada huo unatarajia kuwasilishwa katika kikao cha Bunge kilichoanza jana mjini Dodoma na kwamba vifungu vitakavyofanyiwa marekebisho ni kifungu cha 6 (5) na kifungu cha 18.
Anasema kifungu cha 6 kinachozuia wanasiasa kuteuliwa kama wajumbe wa Tume ya Katiba kingebaki kama kilivyo na kwamba kuingizwa kwa wanasiasa katika tume hiyo kutawafanya waingize maslahi ya vyama vyao katika Katiba.
Vifungu vyenye matatizo havijaguswa katika rasimu ya muswada huo ili vifanyiwe marekebisho badala yake wanataka kubadilisha vifungu visivyo na matatizo, anasema Kibamba.
Anasema katika mjadala wa katiba hoja nzito zilikataliwa kwa sababu tu ya kutolewa na upande fulani wa siasa na hoja zingine hafifu zikiungwa mkono kwa kutokea upande wa wanaotawala.
Anasema kuwa Tume ikishateuliwa inatakiwa kubaki kama chombo cha kitaalam na kusiwe na kigezo cha uwakilishi wa makundi katika upatikanaji wa wajumbe.
Tume hii iwe na watalaam wa masuala mbalimbali mfano, Katiba, Sayansi ya siasa, uchumi, sheria kama ilivyopendekezwa awali, tume sio chama cha uwakilishi wa vyama au chombo kinachoundwa kwa misingi ya taaluma anasema Kibamba.
Anasema vyama vya siasa vitawakilisha vyema kwenye bunge maalum la Katiba pamoja na ukusanyaji maoni, kama ilivyo kwenye sheria kifungu cha 22 cha sheria ya mabadiliko ya katiba namba 8 ya mwaka 2011.
Kazi ya tume ibaki kuwa ni kutoa mwongozo wa kitaalam na namna katiba itakavyoandikwa ikiwa ni pamoja na namna ya maoni yatakavyokusanywa” anasema Kibamba.
Anasema kifungu cha 18 ambacho kinatoa uhuru wa watu wa kada mbalimbali kuandaa mikutano kwa ajili ya kujadili mchakato wa Katiba kinatakiwa kubaki kama kilivyo.
Kifungu hiki kinatakiwa kubaki kama kilivyo kwa kuwa kikibadilishwa kinaweza kuharibu mchakato mzima wa kukusanya maoni, tume inaweza kushiriki katika mikutano ya ukusanyaji maoni itakayoandaliwa na asasi na vikundi vya wadau, anasema Kibamba.
Anasema zaidi ya vifungu hivyo viwili, Jukwaa hilo linapendekeza kuwa kunahitajika maboresho mapana zaidi ya sheria nzima katika awamu hiyo ya marekebisho, badala ya kuleta mapendekezo ya kubadili vifungu viwili.
Anavitaja vifungu vya sheria ya mabadiliko ya Katiba ambavyo havifai na serikali inasita kuvifanyia marekebisho kuwa ni kifungu cha 1, 4 na cha 6,“ Vingine ni kifungu cha 13, 17,20, 21, 24 na 31”.
Anasema kifungu cha 1 kinachosomeka, Jina la Sheria(Sheria ya Mabadiliko ya Katiba), kinatakiwa kisomeke kama, sheria ya kuweka utaratibu, mchakato na vyombo vitakavyohusika kuandika katiba mpya Tanzania, 2011.
Anasema kifungu cha 4 ambacho hakijaonyesha dhumuni kuu la kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya kinatakiwa kisomeke kama, dhumuni kuu la sheria liwe ni kuweka utaratibu wa mchakato wa kuandika katiba mpya.
Anasema kifungu cha 6(1) kinachosomeka, wajumbe wa tume wanaoteuliwa na rais, kinatakiwa kisomeke kwamba, wajumbe wateuliwe na rais lakini wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu cha 6(3)(d) kimetaja neno jinsia tu hakijataja uwiano, sisi Jukwaa tunapendekeza jinsia kwa wajumbe wa tume iwe asilimia hamsini kwa hamsini” anasema Kibamba.
Anasema kifungu cha 7 kinaeleza nafasi ya mwenyekiti na makamu wa tume, pendekezo lao ni kwamba endapo mwenyekiti atakuwa mwanamke, basi makamu awe mwanaume.
Anasema kifungu cha 13 kinanaeleza kuwa ni lazima Katibu wa sekretarieti awe mtumishi wa serikali na kwamba pendekezo lao ni kwamba nafasi ya katibu wa sekretarieti ya tume itangazwe kwa umma na mchakato wa uajiri wake, na kwamba masharti yasimamiwe na Tume ya Utumishi wa Umma ili kupunguza majukumu ya rais.
Anasema kifungu cha 17 (8) kinachosema, asasi iwe imesajiliwa na kueleza chanzo cha fedha kwa tume, hakipendezi kuwa hivyo na kwamba hakuna haja ya kuripoti kwa tume kwa kuwa kuna sheria nyingine zinazohusika na mienendo, kazi, vyanzo vya fedha vya asasi za kiraia.
Anasema kifungu cha 21(3) kinatakiwa kufutwa kabisa kwa kuwa kitazuia wananchi kushiriki katika mchakato wa kupata Katiba yao na kinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu hicho kinazungumzia hatua atakazochukuliwa mtu yoyote ambaye atakwamisha na kuzuia kwa makusudi(mjumbe wa sekretarieti) kutekeleza majukumu ya tume, kutoa maoni kwenye tume, kukusanya na kuratibu maoni, kujifanya kuwa mjumbe wa tume au sekreterieti na kuendesha elimu juu ya mabadiliko ya katiba, adhabu yake ni faini na kifungo.
Anasema kwa mwenendo huo kuna kila dalili kuwa wapo viongozi wa Serikali wenye nia ya kukwamisha kuandikwa kwa Katiba mpya.
Kuna kundi linalotaka marekebisho ya Katiba na si kuandikwa kwa Katiba mpya kwa kuwa linajua litabanwa katika mianya ya ukiukaji wa haki za wananchi, anasema Kibamba.
Anasema madhara ya kupotea kwa matumaini ya Watanzania kuwa na Katiba mpya yanaweza kusababisha umma kususia mchakato mzima na kuendelea na taratibu za kutafuta haki kwa njia mbadala. Anaongeza kuwa Serikali ilifanya makosa kuharakisha kuipitisha sheria hiyo kwani hakukuwa na jambo lolote la dharura.
Matokeo yake ni kuingia katika hasara ya kupoteza rasilimali ikiwemo muda wa kuanza kurudisha tena mchakato huu Bungeni ndani ya miezi miwili tangu kutungwa kwa sheria yenyewe, alisema.
Anaongeza kuwa, haya ni matumizi mabaya ya fedha za wananchi, walikuwa na haraka gani ya kupitisha sheria hii na baada ya miezi miwili wanataka kuifanyia marekebisho?
|
Comments