MwanzoContactsEmail
Home Makala Siasa Tanzania yaweza kushitakiwa The Hague?
BOOKMARK THIS PAGE
Tanzania yaweza kushitakiwa The Hague?  Send to a friend
Wednesday, 01 February 2012 10:55

Elias Msuya
HIVI karibuni Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) imewatia hatiani watuhumiwa wanne kati ya sita waliofikishwa katika mahakama hiyo,  hivyo watakabiliwa na kesi ya mauaji na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika mwaka 2007.


Watuhumiwa hao wanne ni Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura, pamoja na Mtangazaji wa Redio, Joshua Arap Sang.


Watuhumiwa hao wamekutwa na hatia mjini The Hague, Uholanzi baada ya jopo la majaji chini ya uongozi wa Jaji, Ekaterina Trendafilova kuwasilisha uamuzi wao kwa watuhumiwa baada ya maelezo ya awali ya pande zote.
Wakati hayo yakitokea Kenya, hapa Tanzania Chama cha Wananchi CUF kimeadhimisha miaka 11 tangu yatokee mauaji na mateso kwa viongozi na wanachama wake baada ya kufanya maandamano makubwa katika miji ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba ili kupinga matokeo ya uchaguzi ya mwaka 2000.


Maandamano hayo yaliyofanyika Januari 27, 2001 yalikabiliwa na polisi na kusababisha vifo na majeruhi. Hadi sasa idadi ya vifo inayotajwa na serikali ni watu 34, lakini kuna madai kuwa waliokufa ni wengi zaidi ya hao. Wengine walipoteza mali zao na mbaya zaidi, Tanzania ilizalisha wakimbizi baada ya baadhi ya wananchi kutoka kisiwani Pemba kukimbilia Mombasa.
Kutokana na tukio hilo wapo baadhi ya Watanzania wanafikiria kuishitaki serikali ya Tanzania ICC kama ilivyofanyika kwa Kenya.


Kwa sasa tunakusanya ushahidi ikiwa ni pamoja na kuwahusisha viongozi waliokuwepo kama vile aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Seif Khatib na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Omar Mahita. Vielelezo vitakapo kamilika tutapeleka kesi mahakamani anasema mmoja wa Watanzania ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini ili kulinda ushahidi wake.


Hata hivyo kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Haki za binadamu ndani ya CUF Salum Bimani anasema kuwa chama chake kinasubiri maamuzi ya Bunge ili kuhakikisha kuwa madhila yaliyowapata wanachama na viongozi wake yanapatiwa ufumbuzi.


Kwa sasa tunasubiri maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, kwasababu tuliahidiwa kuwa suala hilo litajadiliwa na litapatiwa ufumbuzi anasema Bimani.
Akizungumzia suala la kuishitaki serikali ICC, Bimani anasema kwa sasa chama chake hakina mpango huo, ila kama kuna watu watajitokeza kufanya hivyo chama kitawaunga mkono.
Kwa sasa hatuna mpango huo, lakini kama kuna watu wamejitokeza kushitaki, sisi tutawaunga mkono katika hilo.

Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Sheria katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam Profesa Peter Chris Maina anasema, kuna tofauti kubwa kati ya yaliotendeka Dar es Salaam, Unguja na Pemba Januari, 2001 na yale yaliyotokea nchini Kenya Desemba, 2007 na Januari, 2008.


Ni kweli kwamba katika hali zote mbili kulikuwa na machafuko ambayo yalihusiana na Uchaguzi ingawa yalikuwa machafuko ya aina tofauti na ukubwa tofauti, anasema Profesa Maina na kuongeza,
Nasema kwamba ni machafuko ya aina tofauti kwa sababu Dar es Salaam na Zanzibar ilikuwa ni vyombo ya maguvu vya Dola (Coercive State Apparatus) vikipambana na wananchi waliokuwa wanadai haki yao ya kukusanyika na kuandamana kama Katiba inavyoruhusu kwa upande mmoja lakini huko Kenya ilikuwa wananchi wanapambana wenyewe kwa wenyewe na kuuana kwa kuchochewa na wanasiasa.


Vyombo vya maguvu vya Dola (isipokuwa Jeshi) badala ya kuzuia machafuko vilishiriki kikamilifu, vikachagua upande wa kuunga mkona na kuzidisha machafuko. Kwa hiyo, wakati katika Zanzibar tunashughulikia suala la kisiasa moja kwa moja kwa upande wa Kenya ilikuwa ni suala la mapambano ya kikabila.


Anasema machafuko hayo mawili ni ya ukubwa tofauti kwa sababu wakati Dar es Salaam na Zanzibar kulikuwa na vifo vya watu kati ya 34 (kwa mujibu wa Tume ya Mbita na 60 (kwa mujibu wa CUF) kwa upande wa Kenya vilitokea vifo zaidi ya 1,200 na watu kuchomewa kila kitu na hadi leo wanaishi katika makambi ya wakimbizi wa ndani (internally displaced persons – IDPs) na hawawezi kurudi nyumbani kwao.

Akiizungumzia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) Profesa Maina anasema ilianzishwa na Mkataba wa Roma wa 1998. Mahakama hii inatakiwa ishughulikie aina nne za makosa (Ibara ya 5) Kosa la Uangamizaji (Crime of Genocide), Makosa dhidi ya Ubinadamu (Crimes Against Humanity), Makosa ya Kivita(War Crimes) na Kosa la Uchokozi(Crime of Aggression).


Kama unavyoona, haya makosa na hasa Makosa dhidi ya Ubinadamu yanakaribiana sana naya yale yaliokuwa yametendeka Kenya na ndiyo maana waliotiwa hatiani wamehusishwa na makosa haya. Kwa upande wa Tanzania Januari 2001 yalikuwa machafuko ya kawaida ndani ya nchi na siyo rahisi kuyahusanisha na makosa yaliotajwa katika Ibara ya 5 ya Mkataba wa Roma wa 1998.


Kwa mujibu wa, Ili kesi kupelekwa ICC Profesa Maina anataja  masharti makubwa mawili ambayo ni kwamba, siyo kila mtu anapelekwa kwenye Mahakama hii. “Wanapelekwa wale Wakuu wanaopanga na kuhamasisha jamii kutenda haya makosa (the planners and brains behind the attacks). Wengine wote wanashughulikiwa nyumbani.


Watu wanapelekwa ICC pale tu ambapo nchi imeshindwa kushughulikia makosa haya. Kama nchi ikishughulikia haya makosa hakuna haja ya ICC kuingilia, anasema.
Anasema Kenya walipewa mwanya wa kushughulikia makosa yanayohusiana na machafuko baada ya Uchaguzi Mkuu wakapuuza.


Akizungumzia upande wa Tanzania, Profesa Maina anasema, baada ya mambo kutulia kisiasa, iliundwa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Matukio ya Januari 26 na 27, 2001 ambayo ilitoa Ripoti yake  Novemba 4, 2002.
Anawataja wajumbe wa Tume hiyo kuwa ni pamoja na Mwenyekiti Brigedia Jenerali (Mstaafu) Hashim I. Mbita, Katibu wa Tume alikuwa Philip Mcamanga Wajumbe Masauni Yusuf Masauni, Ali Abdalla Suleiman, Salama Kombo Ahmed, Profesa Hasa Mlawa, Bruno Mpangala, na Kassim Ali.


Hivyo, kwa maoni yangu siyo rahisi kulinganisha hali hizi mbili – yaani Dar es Salaam, Unguja na Pemba Januari 2001 na ile ya Kenya Desemba 2007 na Januari 2008 iliyofanya baadaye watuhumiwa wapelekwe Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) huko The Hague, Uholanzi”.


Vilevile Profesa Maina anatoa angalizo kwamba, Ibara ya 11(1) ya Mkataba wa Roma, 1998 inasema wazi kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) itashughulikia tu makosa ambayo yatakuwa yamefanyika baada ya Mkataba huu kuanza kutumika [The Court has jurisdiction only with respect to crimes committed after the entry into force of this Statute].


Mkataba huu ulianza kutumika tarehe 1 Julai, 2002. Hivyo, machafuko yaliotokea Dar es Salaam, Unguja na Pemba Januari, 2001 hayawezi kushughulikiwa na ICC kwa sababu ya Ibara hiyo hapo Juu, yaani Ibara ya 11(1)”

anasema Profesa Maina.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner