MwanzoContactsEmail
Home Makala Siasa Akitanda: Tumeunda CCK kuziba ufa wa kukosekana chama cha wananchi
BOOKMARK THIS PAGE
Akitanda: Tumeunda CCK kuziba ufa wa kukosekana chama cha wananchi  Send to a friend
Wednesday, 01 February 2012 11:11

Joseph Zablon
IPO dhana kuwa nchini kuna utiriri wa vyama vya kisiasa hivyo hakuna haja ya kuanzishwa chama kipya, hoja ni kuwa vilivyopo vinatosha.


Tanzania inavyo vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu. Lakini bado vio vingi vilivyowasilisha maombi na vingine vilivyopewa usajili wa muda.


Kuongezeka kwa idadi ya vyama vya siasa kunachangia na mifarakano inayoibuka katika vyama vyenye usajili ambapo baada ya kufarakana na kugawanyika huzaa makundi ambayo hitoka na kwenda kuanzisha vyama wanavyoviita vyao.


Chama cha Kijamii (CCK), ni miongoni mwa vyama vilivyo katika orodha ya vyama vinavyoomba usajili wa kudumu. Tofauti na vyama vingi vinavyoanzishwa kutokana na migogoro katika vyama vikubwa, hiki hakijazaliwa kutoka chama chochote kati ya 19 vilivyopo.


Mwenyekiti wa CCK Constastine Akitanda anasema bado Tanzania inahitaji kuwa na vyama vingi vya siasa ili wananchi wachague chama wanachokitaka.


Anasema chama hicho kimeanzishwa na wananchi wa kawaida na ni tofauti na vingine ambavyo vimezaliwa kufuatia kumeguka ama kuhitilafiana kwa viongozi wa vyama vingine.


Chama lazima kitoke kwa wanachama wenyewe na CCK ni chama cha wanachama na ni cha Watanzania,    anasema Akitanda
Akitanda anasema licha ya kuwepo kwa utitiri wa vyama vya kisiasa nchini lakini  CCK wana sababu tatu za msingi za kuanzisha chama hicho ambazo ni pamoja na ukweli kuwa nchini hakuna chama kingine cha upinzani chenye itikadi na msimamo kama CCK.


Anasema hadi sasa toka kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hakuna chama ambacho kinawaridhisha watanzania.


Mwenyekiti huyo kijana anasema ukweli wa jambo hilo unathibitishwa na mwenendo wa wananchi katika upigaji kura ambapo anadai kuwa walio wengi zoezi hilo wamelisusia na wamebaki kuwa wapiga kura wa kuangalia upepo wa kisiasa.


Sababu ya tatu anaitaja kuwa CCK ni chama ambacho kinaitikia changamoto za milenia mpya pamoja na vizazi vyake na kwamba ni chama kilichojipanga kukipokea kijiti CCM na wanaamini kuwa wana uungwaji mkono mkubwa na makundi ya vijana na wazee.


Akitanda anasema hata jina ambalo wamelichagua linaakisi makusudio ya chama chenyewe ya kuwa na mchango wa maana kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuinua hali za maisha ya watanzania wa kawaida, kujenga uchumi imara na shindani wenye kutoa fursa zawa za kufanyakazi na ajira kwa watu wake.


Tunaamini kuwa sera za chama kilichopo madarakani na hasa ndani ya kipindi cha miaka 20 iliyopita zimekuwa kinyume na matarajio ya Watanzania walio wengi, anasema.


Anaendelea kusema kuwa kauli mbiu ya baada ya uhuru ni kuunda jamii ya watu walio sawa na huru dhana ambayo haijatimia na zaidi inatoweka.


Anasema watu ambao ni sawa na huru ni wachache tena ni wale ambao wana nguvu za fedha, ujanja wa kisiasa na madaraka na msukumo wa pamoja kama taifa wa kupigania jamii haupo tena na baadala yake kila mmoja anaangalia maslahi yake binafsi na wale ambao wamemzunguka.


"Msisitizo wa kupigania jamii yetu haupo tena na ndio maana tumeunda CCK ili kuziba huo ufa" anasema na kuongeza kuwa sera za chama hicho ni kujenga jamii ya kisasa ya watanzania yenye utu, heshima na mchango kwa taifa badala ya kuwa kama ilivyo sasa.


Anasema itikadi ya chama chao hicho ni uhafidhina wa kijamii na kiuchumi na msingi wa itikadi ya namna hiyo ni historia ya Taifa ambayo ni kujenga jamii iliyo sawa na haki ambapo serikali imekuwa na matumizi makubwa kuliko vipato vya wananchi wake.


CCK ni chama cha wananchi wote na sio kikundi fulani cha watu kama ilivyo kwa baadhi ya vyama, anasema Akitanda na kuongeza kuwa chama hicho kinataka kupendekeza sera ambazo zitakuwa na majibu tofauti na ilivyo sasa hususani katika suala la uchumi.


Anasema CCM imeshindwa kutengeza uchumi wa kisasa na badala yake umekuwa wa watu wachache ambao wananufaika huku wananchi wa kawaida hali zao zikizidi kuwa mbaya kwani mkazo kwa chama kilichopo madarakani ni kukopa badala ya kutafuta njia za uzalishaji.


Tumeshindwa kufuata dira za waasisi wa Taifa hili ambao ni Rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Amani Karume na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anasema Akitanda.


Anaongeza kuwa CCK itapitia njia walizopita waasisi hao ili kufikia malengo na matarajio ya Watanzania.
Akitanda anasema chama chake ambacho kimepata mapokezi mazuri toka kwa wanachama na watanzania kwa ujumla wake, anasema hakina uadui na chama kingine chochote cha upinzani na hasimu wao mkubwa ambaye ni wa kudumu ni CCM.


Hatuna urafiki na CCM na ni maadui zetu wakubwa lakini tupo tayari kuwa karibu na chama kingine chochote cha siasa ili mradi tuwe tunaafikiana katika masuala ya kisera, anasema
Anasema miongoni mwa malengo ya chama chake ni kuona CCM ikidhoofu na hatimaye kutoweka katika ulimwengu wa kisiasa kutokana na mateso ambayo wameyasababisha kwa watanzania.


Anasema Chama chake kinatembea na kauli mbiu ya 'mabadiliko ni sasa, mabadiliko ni sisi'. Na kuwa katika kuihitimisha kaulimbiu hiyo, wapo tayari pia kumuunga mkono mgombea wa chama kingine endapo ataonekana kuleta mabadiliko.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner