|
Elias Msuya WAKATI Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ukielekea kufikisha miaka 48, tayari kumekuwa na chokochoko kati ya pande hizo mbili hasa katika matumizi ya rasilimali, hali inayotishia uwepo wake.
Hivi karibuni Tanzania imetangaza kuwasilisha maombi Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), jijini New York, nchini Marekani, kudai umiliki wa eneo la ziada nje ya maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi Baharini (EEZ) katika Bahari Kuu ya Hindi, ili iweze kulifanyia utafiti zaidi kuhusu rasilimali zilizoko chini ya bahari kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, rasilimali hizo ni pamoja na mafuta, gesi na madini.
Eneo hilo linatokana na ongezeko lingine tena la maili 150 na hivyo kufanya jumla ya mpaka hadi maili 350, ambazo ni sawa na kilomita 560 kutoka kwenye ‘baseline’.
Waziri Tibaijuka anasema maombi hayo yanatarajiwa kupelekwa na jopo la wataalamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wajumbe wawili kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, litaongozwa na Waziri Tibaijuka.
Kwa mujibu wa Andiko la Kitaalamu lililowasilishwa Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusiana na maombi hayo na ambalo liliwasilishwa rasmi tarehe 18 Januari, 2012, eneo hilo la ziada lililoombwa litakuwa sawa na kilomita za mraba 61,000 katika ukanda wa bahari kuu.
Lakini hatua hiyo imepata upinzani mkali kutoka kwa Wazanzibari ambapo Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe na Naibu Katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Ismail Jussa ametoa hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi kuhusiana na hatua hiyo akisema haikuzingatia maazimio ya baraza la wawakilishi ya mwaka 2009.
Akinukuu Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 1, Jussa anasema, Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
“Ukiangalia ramani ya eneo lililoombwa ambayo inapatikana kwenye ukurasa wa 13 wa Muhtasari (Executive Summary) ya Andiko hilo, na ambayo kwa faida ya wajumbe wa Baraza lako tukufu, nimeiambatanisha pamoja na maelezo ya hoja hii, utagundua kuwa sehemu kubwa mno iliyoombwa ni eneo la bahari kuu ambalo kimsingi liko upande wa mashariki wa visiwa vya Unguja na Pemba. Ndiyo kusema mwenye haki ya kuomba eneo hili na kufaidi rasilimali zilizomo (ikiwa zimo) ni nchi ya Zanzibar” anasema Jussa.
Anakumbusha kikao cha Baraza la Wawakilishi cha tarehe Aprili 08, 2009, ambapo mjadala mzito wa siku tatu mfululizo kuhusu ‘Taarifa ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Ripoti ya Mshauri Muelekezi juu ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia’ uliibuka.
Katika mjuadala huo, Jussa anasema, wajumbe 49 wakiwemo Mawaziri wengi wa wakati ule na pia Mawaziri wengi tulio nao sasa walichangia mjadala huo, tena kwa hisia kali za kizalendo na Spika aliwahoji Wajumbe kuhusiana na maazimio matatu yaliyowasilishwa na Serikali.
Baada ya kuwahoji, wajumbe walikataa kuwa suala hilo lishirikishwe na Jamhuri ya Muungano. Badala yake waliweka pendekezo la eneo la Bahari Kuu katika suala zima la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi liwe katika mikono ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Inaeleweka kwamba baada ya Baraza kupitisha azimio hilo na yale mengine mawili yaliyolitangulia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa aliyekuwa Waziri Kiongozi wakati huo, Shamsi Vuai Nahodha, iliiandikia rasmi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuiarifu juu ya msimamo wa Zanzibar na kutaka hatua zichukuliwe kuyaondoa masuala hayo katika orodha ya mambo ya Muungano. Hilo halijatekelezwa hadi sasa ingawa kutokutekelezwa kwake hakubatilishi maamuzi ya Baraza lako tukufu” anasema Jussa.
Jussa ameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuiandikia rasmi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitaka isimamishe mchakato huo hadi hapo suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi wakati wa mjadala wa Katiba Mpya.
Amesema iwapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitochukua hatua za kusimamisha mchakato huo, basi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipeleke ujumbe wake na barua rasmi Umoja wa Mataifa kuutaka usimamishe kushughulikia maombi hayo hadi hapo suala la mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano utakapomalizika na kukubaliana maeneo ya ushirikiano na maeneo ambayo kila upande utayasimamia wenyewe. Kwa upande wake Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameshangazwa na kauli iliyotolewa na Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa (CUF), kuhusu hoja hiyo akisema haoni sababu ya kugombana wakati ombi hilo liliwasilishwa kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano na wakati wa mchakato wa kuandaa, wananchi wa Zanzibar walishirikishwa.
Sioni sababu ya kugombania fito wakati nyumba tunayoijenga ni moja, siku zote tukipima mipaka huwa tunapima kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi husika, hakuna siku tuliyopima mipaka ya Tanzania Bara wala visiwani peke yake kwenye suala hili,” anasema Profesa Tibaijuka na kuongeza, “Hivi inakuingia akilini, mimi niliyepewa kazi ya uwaziri na Rais niende Marekani kudai ardhi bila watu kujua, ni suala la kusikitisha siwezi kukurupuka kwenda kudai eneo la nchi bila ruhusa ya viongozi, watu wanadai nijiuzulu nitakuwa wa kwanza kuondoka madarakani kama nikijua kosa nililolitenda.
Amesema madai ya Jussa kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) haikushirikishwa katika mchakato huo, hayaendani na yaliyojiri kutokana na wajumbe na viongozi wa SMZ kushiriki na kufanya kazi kwa bidii katika mchakato wa kudai eneo hilo. Kwa mujibu wa Mwandishi mkongwe wa Zanzibar Ally Saleh, hoja za Waziri Tibaijuka na Jussa zinazungumzia vitu viwili tofauti.
Alichosema Jussa na anachokisema Professa Tibaijuka ni vitu viwili tofauti, na kama Professa Tibaijuka alipita baina ya mstari kwa mstari wa Tamko la Jussa basi kwa hakika wao walipaswa kuilaumu Serikali ya Zanzibar na sio Jussa. Lakini hata hilo la kuilaumu Serikali ya Zanzibar halipo, anasema Saleh.
Anasema kwamba kujadili suala hilo ni kitu haramu kwa kuwa mwaka 2009 Baraza la Wawakilihsi lilipitisha Azimio la Baraza kwamba mambo yote kuhusu mafuta na suala la bahari na mipaka yake litoke au litolewe na kusimamiwa na Zanzibar wenyewe. Anaongeza kuwa mabadiliko ya Katiba ya Muungano ni Katiba mama na kwa hivyo mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar hayawezi kukiuka matakwa ya Katiba ya Muungano, lakini hilo ni kosa kuamini hivyo kwa sababu katiba hizo mbili ni sawa katika ukubwa wake,” anasema na kuongeza;
Profesa Tibaijuka ni Waziri wa Ardhi, Makazi na Nyumba mambo ambayo yote si ya Muungano, anapataje haki na uwezo wa kwenda kuiwakilisha Tanzania na kuisemea Zanzibar wakati katika wizara yake suala la bahari halimo. Hata kama lingekuwemo basi bahari si suala la Muungano na kwa hivyo pande hizi mbili zingebidi zikae upya kuamua kufikiria iwapo ipo au hakuna haja ya kulitia suala hilo katika Mambo ya Muungano.
Au kwa wakati huu kwa kuwa si la Muungano pande hizi mbili lingelikabili vipi suala hilo kama ajenda ya Muungano. Kwamba mawaziri wameshiriki na Serikali kutoa wajumbe hakulifanyi jambo hilo liwe halali kama ambavyo hakulifanyi jambo hilo liwe la Muungano. Naye mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ally anasema muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utavurugwa na viongozi wenyewe. “Ni hatari kwa viongozi kujifanya wanawakilisha mawazo ya wananchi bila kuwashirikisha. Muungano huu siyo wa wananchi, hata kero zinazojadiliwa kila siku siyo za wananchi. Ni viongozi tu wanakaa na kujadili mambo yao kisha kuyaita hivyo,” anasema Bashiru na kuongeza;
Ni lini wananchi waliulizwa kuhusu mambo ya muungano wakatoa maoni yao? Haya ni malumbano yenye maslahi ya viongozi wenyewe na hayana tija kwa wananchi. Ni vyema mijadala kama hii ipelekwe kwa wananchi wa pande mbili waamue kwanza ndipo maamuzi makubwa viongozi yachukue nafasi.
|
Comments
Jussa mshauri rais wa zanzibar afanye kura ya maoni na tibaijuka mshauri rais kikwete aitishe kura ya maoni.
Au kwa kauli ya Pinda zanzibar sio nchi.
Lakini la kushangaza kuna rais.
Uwazi unahitajika vyenginevyo donda sugu.