MwanzoContactsEmail
Home Makala Siasa ‘Licha ya migogoro lakini upinzani nchini unaimarika’
BOOKMARK THIS PAGE
‘Licha ya migogoro lakini upinzani nchini unaimarika’  Send to a friend
Wednesday, 01 February 2012 13:22

Na Joyce Mmasi
HALI ya kisiasa katika kambi ya upinzani nchini imekuwa ya kupanda na kushuka. Hii inatokana na migogoro inayoonekana kuvikumba baadhi ya vyama vya upinzani. Migogoro iliyopelekea kufukuzana na hatumaye kupelekana mahakamani.

NCCR-Mageuzi ni mojawapo ya Chama kilichokumbwa na dhoruba ya kujikuta katika mshike mshike na baadhi ya wanachama wake ambao hatimaye kilifanya kile kilichoyaita maamuzi magumu ya kuwavua uanachama baadhi yao akiwemo aliyekuwa mgombea urais wake wa mwaka 2010 pamoja na mmoja wa wabunge kati ya wanne pekee iliyo nao.

Sio NCCR pekee iliyofanya maamuzi hayo, CUF nao wamekuwa na migogoro ya namna hiyo na kufikia maamuzi ya kumvua uanachama mbunge wake wa jimbo la Wawi Hamad Rashid Mohamed huku Chadema nao wakiwahi kufanya maamuzi kama hayo kwa kuwafukuza madiwani wake watano wa Manispaa ya Arusha.

Matukio hayo ya kufukuzana uanachama kwa vyama hivyo vikubwa vya siasa, ndio yanayosababisha kuwepo kwa maswali yanayokosa majibu kuhusiana na nafasi ya kambi ya upinzani nchini, Je upinzani unakua au unadidimia.

Je, mfululizo wa matukio na migogoro hiyo inaleta mtazamo gani kwa wananchi dhidi ya kambi ya upinzani nchini?
Moses Machali, ni mbunge wa Kasulu Mjini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi anasema matukio yote yanayotokea ama kufanywa na vyama vya upinzani nchini, ni matukio ya kawaida licha ya kuwa yanaleta picha isiyokubalika miongoni mwa jamii.

Machali anasema migogoro ndani ya vyama vya siasa ni vitu visivyokwepeka na kwamba ni sehemu ya uhai ndani ya vyama husika kwani vinaweka msisimko wa wahusika kujitazama upya na kujitambua.

Anasema kwa kawaida hakuna Chama cha siasa ambacho kinakuwa shwari mwaka mzima iwe nchini ama nje ya nchi na kwamba kutofautiana miongoni mwa watu wanaokaa pamoja ni mambo ya kawaida licha ya kukiri kuwa baadhi ya migogoro inatofautiana na kuwa mingi inasababishwa na mitazamo ama maslahi binafsi ya wanayoianzisha.

 Hakuna wakati utafika ukute hakuna mgogoro/kutofautiana ndani ya jumuiya au makundi fulani ya watu, haya ni mambo endelevu…, jambo la msingi ni kuhakikisha kunapokuwa na kutofautiana utatuzi ufuate kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa na jumuiya husika, anasema.

Anatolea mfano hali ya mtafaruku iliyokuwa ndani ya Chama chake ambayo anasema kwa kuzinatia kanuni, sheria na taratibu Halmashauri ya chama ilifanya tathmini ya kina, ikaridhika na kufanya maamuzi kwa nia ya kukinusuru licha ya kuwa yalikuwa maamuzi magumu..

Anasema hakuna ubaya wowote kumfukuza mwanachama au kiongozi katika nafasi yake ndani ya Chama endapo taratibu zitakuwa zimefuatwa…kama inagundulika mtu fulani ni tatizo ndani ya chama fulani…, hakuna utakachofanya endapo kanuni zitataka afukuzwe.

Kufukuza sio tatizo kama haki imetendeka, utaratibu umefuatwa na tahtmini imefanyika…, Watanzania wasitake kwenda na upepo…, watu wasiangalie umaarufu wa mtu, waangalie je ni muadilifu, je, anaheshimu sheria, kanuni na misingi waliyojiwekea…, ni sawa na mgonjwa wa Kisukari au Kansa kama dawa ya kupona ni kuukata mguu inabidi uukate mguu wako ambao unaupenda sana, ili upone, anasema

Machali ambaye vile vile ni msemaji wa NCCR Mageuzi nafasi aliyoteuliwa baada ya kumvua aliyekuwa akiishikilia kabla ya uchaguzi, David Kafulila anasema hali ya kisiasa ndani ya NCCR baada ya maamuzi waliyofanya ni shwari kabisa, na kuwa mambo yote yanaenda vizuri.

Mikakati ya NCCR kujiimarisha:
Akizungumzia mikakati ya chama katika kujijenga na kujiimarisha? baada ya matukio yaliyotokea anasema “Ipo mikakati mingi lakini kubwa ni kushinda viti vingi vya udiwani, ubunge na hata katika serikali za mitaa.

Anasema NCCR hailengi katika kushinda nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, na badala yake malengo yake ni kuongeza viti vingi zaidi vya uwakilishi wa wananchi.

Anasema mikakati waliyoiweka kama chama katika kutimiza malengo yao ni pamoja na kuendelea na mkakati wa kawaida wa kunadi sera za chama kwa kuelimisha wananchi mambo mbalimbali, kutoa elimu ya uraia, na kuhamasisha kuhusu kuwasilisha maoni yao katika mchakato wa kupata katiba mpya.

Hatutaki na wala hatufanyi siasa uchwara….tunataka siasa ambazo zitaleta matumaini, ukwel na ambapo watu watatuunga mkono…tayari idara ya tumeanza mpango ya kufanya ziara mbalimbali mikoani, sasa tumeanzia mkoa wa Mwanza nab ado tunaendelea anasema Machali

Nafasi ya NCCR – Mageuzi katika siasa nchini  
Anasema chama chake kimeweza kupata mafanikio makubwa kwa muda mfupi tangu kilipoanza mpango mkakati wa kujijenga upya ambapo anasema ndicho chama cha tatu, cha siasa chenye nguvu nchini kwa sasa.

Sisi tunashika nafasi ya tatu sasa kwa nguvu ya kisiasa nchini, ukitoka CCM na Chadema ni sisi NCCR ndio tunafuata ingawa CUF wana wabunge wengi lakini kwa siasa za TZ sisi ndio tutachukua nafasi ya tatu kutokana na tunawafikia watanzania…..kuhakikisha wananchi wanaujua ukweli kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii anasema.

Je, anaizungumziaje hali ya kambi ya upinzani nchini? Je, vyama vya upinzani vinakuwa au vinadidimia? Machali anasema vyama vya upinzani vimekuwa na kujijengea heshima kutokana na viongozi wake waliochaguliwa na wananchi kuwa makini katika kufanya kile walichoagizwa na kuaminiwa na wananchi.

Anasema ishara ya kukua huko inaonekana katika mafanikio iliyoyapata kambi ya upinzani katika kuongeza idadi kubwa ya wawakilishi wa wananchi ambapo idadi ya wabunge wa kambi ya upinzani imekuwa kubwa na inayofanya kazi nzuri kuliko kipindi cha nyuma.

Mwenyewe ni shahidi wa hoja nzito zinazoibuliwa bungeni na wabunge, uwakilishi mkubwa wa wabunge na uongozi wa halmashauri nyingi unaofanywa na vyama vya upinzani, yote haya ni mafanikio ya kambi ya upinzani na ni ishara na kielelezo kuwa upinzani nchini unakuwa kwa kasi kubwa, anasema Machali.

Anasema kumekuwa na tofauti kubwa baina ya wawakilishi wa wananchi waliochaguliwa na wananchi kutoka kambi ya upinzani na wale wanaotoka CCM ambapo anasema wale wa upinzani wamekuwa wakijadili na kuibua mijadala yenye tija kwa taifa tofauti na wenzao wa chama tawala.

Anasema hata hivyo bado ipo changamoto kubwa wa wabunge wa upinzani ambao anasema wengi wamekuwa sio wakweli hasa katika masuala madogo kama ongezeko la posho ambapo licha ya wananchi kupiga kelele wamekuwa wakisimama kutetea ongezeko hilo wakiwa ndani ya vikao na wakiwa mbele ya wananchi kujifanya kuwa miongoni mwa wanaopinga.

Natoa wito kwa wabunge wenzangu…tusiwe vipofu, tufanye kile ambacho wananchi wanataka tuyafanye….tusiwe waongo waongo kama baadhi ya wabunge wenzetu…vile vile tuache tabia ya kupigana vita…..unakuta wabunge tunapondana wenyewe kwa wenyewe, hatuna umoja, tushikamane, tuache tofauti zetu…… kuchafuana kwasababu binafsi…itasababisha upinzani uchelewe kukua, tuache ubinafsi, tuweke mambo binafsi tunapofanya siasa zenye mwelekeo, anasema Machali.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner