
| Nyanzige: Mtunzi wa hadithi anayechipukia,anaiomba jamii imsaidie kompyuta | Send to a friend |
| Tuesday, 24 January 2012 12:03 |
|
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kiwanja Cha Ndege iliyoko Manispaa ya Dodoma, Nyanzige Lazaro (18) amekuwa kivutio kikubwa mkoani Dodoma kwa kuwa na kipaji kikubwa cha utunzi wa hadithi zilizoanza kuwavutia wasomaji wengi. Anasema alianza utunzi akiwa darasa la saba akifanya kazi hiyo kama sehemu ya kujifurahisha kabla ya baadaye kutambua kuwa hicho ni kipaji chake ambacho kwa sasa kimempa umaarufu mkubwa. “Nilianza nikiwa darasa la saba katika shule ya Msingi Mlimwa A’ ambapo nilisoma kitabu cha Eric Shigongo kiitwacho ‘Rais anampenda mke wangu.’ Niliwaza mengi juu ya hadithi ile nikaona lazima na mimi niandike kitu,’’anasimulia mwanzo wa utunzi wake. Anasema baada ya kusoma kitabu hicho, alitafuta kisa cha kuandika na ndipo alipopata wazo la kuandika kisa kuhusu rafiki yake anayemtaja kwa jina la Vero. “Niliandika mkasa kumhusu Vero na nikawapa wanafunzi wenzangu na walimu, walinisifia kweli wakasema ninaweza…. ile hadithi ilipendwa sana ingawa niliweka mambo mengi kwa ajili ya kuinogesha,’’anaeleza. Baadhi ya hadithi anazokumbuka kuziandika ni pamoja na Maisha yangu, hadithi inayomhusu Vero. Nyingine ni Kuvunja, Kutekeleza ahadi, na Watawala. Kwa maelezo yake, anasema kuwa hadithi hizo zimejaa visa na mikasa ya kusisimua ambayo imebeba ujumbe mzito na mafundisho kwa jamii. Kuhusu hadithi hizo kukidhi vigezo vya kitaalamu, anasema: ” Naomba kusema ukweli, hadithi zile hazikuwa na vigezo vya kitaaluma, lakini namshukuru sana Mungu kuna mtu alimpa hadithi zangu ndugu Pius Nyange ambaye alinitafuta na kuamua kunisaidia namna bora ya kuandika hadithi.” Baada ya kufundwa na Nyange ambaye ni mtunzi maaarufu na mahiri nchini, anaeleza kuwa alianza kutunga kazi bora zaidi ambazo baadhi kwa sasa zinatumika kama tamthilia hususan kwa vijana. Nyanzige ambaye kwa sasa anakamilisha hadithi ya ‘Wapelelezi’ anasema hutumia muda wa mapumziko ya juma kwa ajili ya kutunga hadithi zake, huku akijisifu kuwa hadithi anayotunga hivi sasa itakuwa nzuri kuliko zote alizowahi kuzitunga. “Siwezi kusifia sana, lakini nimejaribu kutulia katika hilo maana nimeona waandishi hamuwazungumzii sana wapelelezi, hivyo nimeamua kuwatungia hadithi kuhusiana na kazi yao nikihusisha na rushwa,’’anafafanua. “Wateja wangu wakubwa ni kina dada na vijana ambao wanapenda kununua kazi zangu na kusoma kwa ajili ya kujiliwaza, lakini kumbuka naandika kwa mkono, halafu wao ndio wanaochapisha.Kweli wanalalamika lakini sina cha kufanya,’’anasema. Kuhusu taaluma shuleni anasema anayapenda na kuyamudu masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Historia. Ndoto yake ni kuwa mwanahabari na anataka kuisomea fani hiyo mara tu amalizapo kidato cha nne. Pia Nyanzige anayetamani sana kuja kuwa msanii wa michezo ya kuigiza, anaiomba jamii kumsaidia vifaa vya kuandikia na kuchapa ikiwa ni pamoja na kompyuta. |



Na Habel Chidawali










