MwanzoContactsEmail
Home Makala Maarifa Tahadhari ya wadau wa elimu kuhusu mtihani wa kidato cha pili
BOOKMARK THIS PAGE
Tahadhari ya wadau wa elimu kuhusu mtihani wa kidato cha pili  Send to a friend
Tuesday, 24 January 2012 12:07

Na Fredy Azzah
KILIO cha muda mrefu cha wadau wa elimu  kutaka makali ya mtihani wa kidato cha pili yarejeshwe, kimejibiwa .
Mapema mwaka huu, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo  alitangaza uamuzi wa Serikali  kuupa tena meno mtihani huo.

Mulugo  akitangaza uamuzi huo wa serikali anasema kuwa “Kuanzia mwaka 2012 mwanafunzi atakayepata wastani wa chini ya asilimia 30 katika Mtihani wa Kidato cha Pili hataruhusiwa kuendelea na Kidato cha Tatu. Atatakiwa kukariri Kidato cha Pili na fursa hii itatolewa mara moja tu,” Anasema na kufafanua:

“Mwanafunzi atakayekariri kidato cha pili na kushindwa kufikia wastani wa asilimia 30 ataondolewa katika mfumo rasmi wa Elimu.”

Pamoja na msimamo huo wa serikali, wadau wa elimu wanatoa maoni yao mbalimbali juu ya uamuzi huo wa serikali, wengi wao wakiupongeza lakini wakitoa baadhi ya kasoro zinazotakiwa kufanyiwa kazi.

Dk Marcelina Chijoriga Mkuu wa Shule ya Biashara,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Uamuzi wa kurudisha makali ya mtihani wa kidato cha pili ni wa msingi kwa kuwa unawapa wanafunzi sababu ya kusoma.

Hata hivyo, tatizo lililopo katika mfumo wa elimu  Tanzania ni mkanganyiko wa uamuzi.
Wakati ule ambapo Mungai (Joseph Mungai) akiwa Waziri wa Elimu, alifuta masomo ya biashara shuleni, athari zake zinaonekana  sasa hivi kwa wanafunzi wanaokuja vyuo vikuu.

Yale masomo yalikuwa yanamwandaa mwanafunzi kwa  masomo ya chuo kikuu, sasa mtu anakuja akiwa hana maandalizi ya awali, hili  ni tatizo.

Mgongano wa maamuzi kama hayo, ndiyo pia uliofanya kufutwa kwa mtihani wa kidato cha pili na matokeo yake wanafunzi wakawa wanaona hakuna sababu ya kusoma.

Kuhusu mtihani huu, ingekuwa vema mtoto kurudia darasa pale anaposhindwa mtihani, lakini siyo kufukuzwa shule kwa sababu amerudia mara mbili na kufeli.

Wale watoto bado ni wadogo, siyo vizuri kufukuzwa shule lakini wakiwa wanarudia darasa, itawasaidia kujitahidi na kuhakikisha wanafanya vizuri.

Dk Kitila Mkumbo Mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na Masomo ya Mitalaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuondoa makali ya mtihani huo haukuwa sahihi hata kidogo, kwa hiyo kuurudisha ni jambo la msingi na muhimu kwa msitakabali wa  elimu yetu.

 Kurudisha mtihani huo na kuwataka wanaoshindwa warudie darasa, ni moja ya mambo  yatakayowafanya wanafunzi wasome hata kama hawapendi.

Kwa kawaida watoto wadogo hawasomi kwa malengo kama watu ambao wapo vyuoni, kwa hiyo ili kuhakikisha hawa watoto wanasoma lazima kuwe na sababu ya kuwafanya wapende ama walazimike kusoma.

Lakini kwenye hili jambo la kusema wanaofeli wanapata nafasi moja ya kurudia na wakishindwa wanaondolewa katika mfumo rasmi wa elimu, nadhani haijakaa sawa.

Kufanya hiyo ni sawa na kuwatupa hawa vijana, tunaweza kusema kuwa serikali inawakaanga kabisa.

Mtoto anaweza kushindwa mfumo wa sekondari, lakini akaweza kwenye vyuo vya ufundi, kwa hiyo badala ya kusema kuwa wataondolewa katika mfumo rasmi wa elimu, ni vyema tukaangalia njia nyingine ya kuwasaidia.

Kwa mtazamo wangu, ingekuwa vizuri wale wanaoshindwa, wapelekwe katika vyuo vya ufundi na siyo kuwaondoa kwenye mfumo rasmi wa elimu.

Lengo ni kumfanya huyu mtoto awe na stadi za maisha, aweze kujitegemea asiwe ni mzigo kwa wazazi wala serikali.

Aloyce Eliakim (Mwalimu Shule ya Sekondari Rafiki iliyopo Tabata,Dar es Salaam)
Hiyo ni hatua ya busara. Wanafunzi wengi wa kizazi hiki wanasoma kwa ajili ya mitihani, sasa unapomwambia mwanafunzi akiingia sekondari hatofanya mtihani wa mchujo mpaka atakapofika kidato cha nne, unamfanya asione sababu ya kusoma.

Huu mtihani  unafanya wanafunzi wasome kwa bidii, lengo na maisha. Wataona  aibu  kuachwa na wenzao kidato cha pili, hivyo watajitahidi kusoma ili wasirudie darasa.

Lakini suala la kusema watapata nafasi moja ya kurudia mtihani wala watakaofeli kisha waondolewe kwenye mfumo rasmi wa elimu, sikubaliani nao.

 Kwa mtazamo wangu, ni vyema wakapewa angalau nafasi mbili za kurudia wakishindwa sasa ndiyo serikali iangalie jinsi nyingine ya kuwasaidia ili baadaye wasije kuwa mzigo.

Kwa huu msimamo wa kuwapa nafasi moja tu, nadhani itaongeza idadi ya vijana wa mtaani, hilo litakuwa ni tatizo na siyo suluhisho.

Wanafunzi wanafeli mtihani kwa sababu nyingi, siyo kuwa wote wanaoshindwa mtihani hawana akili, ni vyema serikali ikajihakikishia kwanza kuwa, mwanafunzi anayeondolewa kwenye mfumo wa shule ya sekondari kweli hawezi.

Mariam Adam (Mwanafunzi wa sekondari)
Kurudishwa kwa mtihani  huo, kutawapa wanafunzi changamoto ya kusoma hata kama hawapendi kufanya hivyo.
Utawakuta wanafunzi wengi wanacheza tu hawajali kusoma kwa sababu wanajua kuwa  mtihani watakaofanya hauna madhara kwao.

Huu  mtihani sasa utafanya wanafunzi wengi wasome kwa bidii.

Pia mimi nadhani kusema wanaoshindwa mtihani waondolewe kwenye mfumo rasmi wa elimu ni sahihi pia.
 Omari Yunus (Mwanafunzi)

Kufeli na kurudia darasa na wanafunzi ambao walikuwa nyuma yako ni aibu, huu mtihani utakuwa ni changamoto kwa wanafunzi kusoma ili wafaulu.

Mchujo wa mtihani huu pia utaepusha kuwapo kwa wanafunzi wanaofika hadi kidato cha nne wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

Usishangae baadaye kunakuwa na watu wamefaulu, wapo kazini lakini hawajui kusoma wala kuandika. Mtihani wa kidato cha pili una maana kubwa  kwenye mfumo wa elimu.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner